The Chant of Savant

Wednesday 7 November 2007

Jicho la Kijiweni

Laiti kama tuzo ya ‘Mo’ ingetua kijiweni…
Mpayukaji Msemahovyo
BAADA ya mkuu mng’atufu kujibu mapigo kwa uoza, kijiwe kimekutana ghafla kutoa msimamo.
Tunashangaa na kuhuzunika, tunalaani kitendo cha jamaa huyu kusema hawezi kujibu eti ni mambo ya kisiasa!
Pili, tunashangilia kukosa tuzo ya mabilioni ya Mo. Ingekuwa aibu na pigo kwetu: ungekuwa msiba na angejidai jamaa yetu.
Mpemba aliyerejea kutoka Nzega kuzomea analianzisha. “Yakhe mmesikia Nkapa alivo jeuri? Eti asema hawezi jibu shutuma kwa vile za kisiasa! Huu ujambazi mpya walahi, asema alindwa na katiba. Walahi hii ati!”
Machungi hangoji. “Mgosi unashangaa! Mzee husema kaya inaiingiwa. Kwei inaiingiwa sana. Tisipoamka na kupambana na hawa titajikuta hatina hata nchi, wataiuza hawa mafisi.”
Kachokoza nyuki! Kapende anadanda na mic. “Tuni tuni lazima aambiwe laivu huu ni ujambazi na uhuni hata kama wa wazito. Mbona wakati tukiweka na kuchukua alijifanya mtu wakati fisi? Tuandamane kumlaaani hata kumzomea kama tulivyofanya kwa wezi wenzie.”
Mkurupukaji anaikurupukia mic. “Hakuna kitu kimenikuna kama jamaa kunyimwa tuzo ya Mo. Angejidai na kutuzodoa. Angepewa, ingekosa maana. Ingekuwa sawa na kumpa mlevi tuzo ya utauwa. Wenzetu kimataifa wameishastuka. Unacheza na mtandao nini?”
Mzee mzima singoji kukaribishwa. Nalamba mic.
“Kama wanakaya wamemuogopa sasa ajue nitamfungulia mashitaka binafsi. Akishinda yeye, mkewe na mwanawe na Alter ego yake YonaeDan, nitawapata. Wao watajificha kwenye nini: hawakuwa wakuu?”
Mzee utamshitaki wapi: “Mapilato wote ni wateuliwa wake? Naona tungemtokea na mawe tukafunga mitaa na kumsaka popote alipo ili dunia ijue kaya imeamka. Kibaka ni kibaka hata awe mfalme.”
Mchunguliaji anakuja na mpya. “Wananchi ndiyo hakimu. Kwanza acha nimtapikie asikie. Tunituni ulipayuka, kuropoka, kutapika na… nasi hatukukopeshi tunakupa laivu kuwa wewe si safi, tena chovu. Naomba Mungu hiyo mali ikutokee puani. Kumbaff! wote wanaoshabikia upuuzi na ufisadi.”
Kijiwe hakina mbavu kwa anavyopayuka.
Mzee Maneno hajivungi anakwanyua mic. “Hapa lazima tutoe tamko rasmi kuwa tunalaani wizi wa Tunituni, nkewe na washirika wake wote wawe wameishang’atuka au wanaendelea kuiba inshallah Mungu yupo atawaamsha wanakaya wawasulubu,” alisema.
Katia mafuta motoni! Makengeza anavyotukuta akimnasa Tunituni au nkewe anaweza kufa na mtu. Analamba mic. “Mwenzenu mie lazima niende kwa akina mgosi lau nitupe jiwe moja kwenye hekalu lake.”
Kapende naye hataki apitwe: “Nyie mnamlaumu Tunituni bure. Namshukuru kwa kutufumbua macho. Isingetokea hii nani angejua kuwa huyu naye na kundi lake wana mpango wa kukwapua? Huoni amechukua mafisi na uoza wote aliokuwa nao Tunituni. Kimsingi hawa ni mapacha.”
Mzee Mdomo naye anapoka mic atugune. “Mijizi kweli haina adabu na aibu. Ulimuona yule jambazi wa kike mwenzie na kibaka Tunituni eti anachangisha pesa ya misosi! Tutamwaminije wakati tunamdharau kwa kuwa kibaka na familia na mashoga zake?
Msomi anajilisha upepo. Mbona akina Suharto, Estrada, Fujimori na Chiluba walikuwa wakiota kinga mfu kama yeye: wemefikishwa pakanga.
Katiba hailindi ulafu ila makosa yatokanayo na ofisi, si familia. Wasitufanye hatujui sheria. Nimesoma Constitutional jurisprudence bwana. Anajidanganya sharti arobaini yake ifike.
Tusipomnasa yeye tutamnasa mkewe, mtoto au mashoga zake kama alivyosema mzee mzima pale. Tusitegemee mkuu au mapilato kutusaidia bali sisi wenyewe ambao ni mahakama tosha. Warumi husema ‘vox populi vox Dei’.
Kabla ya kuendelea naona mzee Maneno anataka kupinga kuchanganya kimombo. Msomi keshaliona anakula tena mic. “Nitafsiri wazee. Maana yake ni sauti ya wengi ni sauti ya Mungu, je, wao ni nani wapingane na Mungu? Lazima tuwaambie Ikulu ni yetu si ya mama zao waitumie kutuibia.
“Tunituni Makapu asidanganywe na utetezi mfu wa kina Walioboa wala Cheka cheka mzururaji.
“Wanakaya lazima tuamke tuwaonyeshe kuwa kaya hii ni yetu, si ya wazazi wao, narudia.
“Kama tumeweza kuwazomea wenzao tunashindwa nini kuchukua mabango kufanya kweli?”
Anainua kombe lake na kupiga busu kutuliza usongo na kukusanya mapwenti.
Kuonyesha kijiwe hiki hakimuogopi yeyote hata awe na magwanda, leo tutoe tamko la kuwalaani Tunituni na Mzuraraji mtalii na yule Lwasha na Rasta Azoza.
“Wanakaya tumeanza na kuzomea. Tutamalizia kwa kufanya kweli. Tazameni yaliyojiri kule Tanga na Tandahimba.”
Kabla ya kuendelea kuzoza Mgosi anaingilia. “Je, ya Tanga iikuwa cha mtoto. Azima tufanye kwei. Kwanini kaya nyingine wameweza sisi tisiweze? Timeogwa na nani, nyie wanakaya kia kitu kiko wazi mbee yenu?”
Watu hatuna mbavu anavyokandamiza kisambachi!
Msomi anaendelea. “Kwenye kitabu kipya cha tajiri wa Marekani, Donald Trump anasema. Hili ni tusi kubwa. Tajiri anasema ikibidi hubidika, usitafune maneno. Nami niseme we’ill kick their …." Kabla ya kuendelea kadi nyekundu inaashiliwa na mzee Ndomo. Anasema. “Msomi najua umechukia. Ila ung’eng’e umezidi ndugu yangu.”
”Okay mzee wangu, sina tafsiri ya hili. Halafu jamaa huyu Trump ana njuluku kama hana akili nzuri. Ila alisema kuwa lipi tusi kusema au kutenda?
“Nikija kwenye tuzo ya Mo. Ingekwenda kwa kakumba wetu ingekuwa aibu ya mwaka. Basi kwa taarifa mie ndiye Uvuruge. Nilimtwanga e-mail Mo mwenyewe asifanye ushoga na Tunituni.”
Kabla ya kuendelea kijiwe hakina mbavu kwa anavyotuvunga utadhani msanii na wanakaya au jambazi wake wa dege! Anadhani hatujui kama wanavyodhani majambawazi wetu!
Anaendelea: “Kama kuna tuzo ya kibri basi na apewe tutamuunga mkono wakati tukipanga kumtia adabu na wenzake.
“Kwanza niwachekeshe.” Anageukia wanakijiwe na kuendelea. “Nimecheka kusikia eti jamaa ana Ngo ya kupambana na ukimwi! Hivi kuna ukimwi kama kuuza na kuiibia nchi yetu? Yeye Ngo mkewe Ngo bado kijana wake. Hii kwangu ni miradi ya kuzidi kuwamaliza watu. Finish.”
Mzee Maneno naye anaongezea. “Kweli. Kama anatupenda atueleze kwanini alichezea patakatifu pa patakatifu petu.
Huu nao ni usanii kama wa jamaa zake wanaomlinda badala ya kulinda kaya. Jamani, tutoe tamko la kumlaani jamaa huyu na wenzake.
Wasituhadae na miradi ya kijamii wakati wanaibia jamii halafu wanajitia kiburi kuwa hawawezi kuongelea siasa. Huu ni udokozi siyo siasa wala nini. Nalaani vitendo hivi. Naomba kutoa hoja.”
Kijiwe kinalipuka na kusema. “Walaaaniwe walaaniwe wazomewe wazomewe na mwishowe wapigwe na kutimuliwa.
Taarifa Mbwa Mwitu hajarudi toka Tandahimba alipokwenda kuhamasisha kuwashughulikia mafisadi ambao wameishaonja joto ya mwamko wa wanakaya. Yaelekea ndiye alilitia kibiriti lile hekalu la jamaa.
Hii ndiyo hasara ya vyombo vya kaya kukosa imani kiasi cha kulazimisha wanakaya kuchukua sheria mikononi.
Tukiwa ndiyo tunaanza kutanua kwa sana, mara gari la polisi lilipita, tukaanza kulimwagia maji machafu.
nkwazigatsha@yahoo.com

No comments: