The Chant of Savant

Monday 28 January 2008

Mkapa, Kikwete, ufisadi na mainzi.



Jikumbushe makele ya Mainzi wanapokuwa kwenye mzoga halafu akaja Mbweha au Mbwa hata Kicheche kuushambulia mzoga wake. Mainzi uhanikiza na kupiga makelele kama silaha pekee yaliyo nayo.

Hakika makelele ya mainzi huwa hayamzuii mvamizi kula mzoga atakavyo hata wakati mwingine kuyala mainzi yenyewe na yasifanye kitu! Hawa ni hayawani isitoshe wadogo wasio na misuli na vikumbo kuweza kupambana na mvamizi.

Jaribu mfano mwingine wa Vyura pale Tembo avamiapo bwawa kunywa kuoga na kuyachafua Maji. Vyura, kama Mainzi, nao hupiga kelele hadi Mswahili akawazodoa: kelele za Vyura hazimzuii Tembo kunywa maji.

Mswahili huyu huyu bingwa wa falsafa hata mafumbo haishii hapo. Husema: kelele za mMango hazimnyimi Mpangaji usingizi.

Ukiangalia mazingaombwe, usanii, ujambazi na kila hadaa vinavyofanyika "kuwanusuru" watuhumiwa wizi wa mabilioni ya pesa kwenye akaunti ya madeni ya nje (EPA), bila shaka, unaijiwa na picha hizi tatu. Ni somo gani unapata hapa?


Kwanza, ni uhovyo wa mainzi, vyura hata mlango. Pia ni uonevu wa tembo na mbweha, mbwa, vicheche (mvamizi).


Pili ni hekima: tusifanye mambo kama hayawani. Tusiridhike na makalele ilhali "wabaya wetu" wakiendelea kuukatua mzoga, kuchafua na kunywa maji au kuuchapa usingizi. Je nasi tumekuwa wa hovyo kama wao? Je tumekuwa katili kwa vizazi vijavyo kwa kuendekeza woga na makelele ilhali mambo yanazidi kuharibika?

Kujibu maswali haya vizuri, jiulize, mbali na makelele na ngebe, watanzania wamefanya nini kuzuia mzoga wao kushambuliwa na wanyama tajwa wanaojulikana kwa uchoyo na ulafu wao? Wamefanya nini pale waliyemtegemea atende haki kwa kumkabidhi ofisi na zana zote za dola ameamua kuzitumia dhidi yao kuwalinda Mafisadi?

Je kwa msimamo wa rais Jakaya Kikwete kwa mfano kusema wazi hatamchunguza mtangulizi wake, Benjamin Mkapa, siyo kuusaliti umma na viapo vyake vya ofisi? Maaana, wahenga husema: asiyevuta kamba nasi si mwenzetu ilhali waingereza wakisema: show me your friend I shall tell you who you are ama nionyeshe marafiki zako nikwambie wewe ni nani? Je katika hili Kikwete ni nani? Sitaki nimjibie.

Taarifa za vyombo vya habari kuwa uchunguzi wa kashfa ya BoT, jina la rais mstaafu linajitokeza mara nyingi si za kuacha kama taarifa tu bali onyo kuwa watanzania hawajiandaa kupambana na ufisadi wala kurejesha mali zao zilizomo mikononi mwa mafisadi ambao kwa bahati mbaya wengine bado wamo kwenye ofisi za umma wakiharibu ushahidi na kulindana!

Inashangaza udhati wa Kikwete kuweza kulala usingizi hata kujitahidi kuwaridhisha wananchi; atapambana na ufisadi wakati ukweli ni kwamba kinachofanyika na kinachosemwa ni tofauti kama usiku na mchana hata mbingu na ardhi! Je umma haujaona mchezo mzima?

Niliwahi kuuliza: kama Mkapa ana kinga na mkewe, mwanae na washirika kwenye makampuni yao nao wana kinga? Mbona hawakuwa marais hata kwa sekunde moja? Au ni yale yale ya ufalme wa mlango wa nyuma? Au tuseme: ni yale yale; waarabu wa Pemba?

Kwanini hatutaki kuwaambia watawala: hii ni nchi yetu na siyo yao wala mama zao? Kwanini tunaogopa hata kuchukia kama tumeshindwa kuondosha kwa mkono?

Leo ufisadi wa BoT umebebwa na Daudi Ballali, gavana wa BoT wa zamani utadhani alikuwa peke yake! Kwanini tunachezewa mahepe mchana kama watoto wadogo nasi tunaupwakia uongo na matusi haya?

Tuliwahi kuuliza na kudodosa alipopata na alivyopata mali zinazosikika kuwa za Mkapa kama vile majumba ya Lushoto, Upanga na mengine ambayo bado hayajajulikana. Tulidhani umma ungetumia hojaji zetu kudai haki kwanza na kama madai hayasikilizwi basi uchukue mali zake au hatua mujarabu. Lakini wapi?

Tuliwahi kuhoji: nani anamfanya nani bwege? Tulihoji: kazi ya rais ni nini na ipi iwapo anatuzodoa tena hadharani; hawezi kumchunguza Mkapa achilia mbali kumfikisha mbele ya haki? Je hatujawa mainzi tena mafu? Ajabu ya nchi yetu; tuko tayari kuandamana hata kupambana na FFU kwa mambo madogo kama kashfa za kidini na mengine lakini hatuna mshipa wa kusimamia haki zetu zitendeke na kulindwa?

Je rais na watendaji wake wanajua uhovyo wetu kiasi cha kututendea mambo ya hovyo hivi? Je kwa kutenda hivi wahusika nao hawajawa wa hovyo kiasi cha kuwa na nchi hata jamii ya hovyo? Je mwelekeo wa hali hii ni nini kama siyo miaka mitano ijayo kushuhudia makubwa kuliko hata haya ya Mkapa? Je hatujawa kichwa cha mwendawazimu kama alivyowahi kuonya mzee Ruksa? Hatujawa mainzi mafu?


Ajabu ya maajabu, vijana wetu wengi wamegeukia jinai kama ujambazi hata uchangudoa ambayo kimsingi vinaweza kuondoa uhai wao ilhali kudai haki halali kumetelekezwa! Kiongozi na shujaa wa Mau Mau kule Kenya, Dedan Kimathi aliwahi kusema; heri kufa umesimama kuliko kuishi umepiga magoti. Tuko wapi sasa?

Nchi jirani ya Ethiopia kuna kabila la Oromo ambalo kwenye lugha yake ya Oromia kuna methali isemayo: heri kuishi siku moja kama simba kuliko miaka mia kama kondoo. Je sisi hatujawa kondoo tena wa shughuli ya fisi?

Kuna haja ya kuwatolea uvivi Kikwete na swahiba yake Mkapa na kuwaambia: Tanzania siyo yao peke yao:ni yetu sote kwa sawa. Badala ya kunung’unika na hata kumlilia marehemu Mwalimu Nyerere au kuotea; atakuja malaika kutukomboa, tuamke na kurejesha nchi yetu mikononi mwetu.

Inashangaza na vyombo vya dola vyenye watendaji makapuku kama Polisi na idara nyingine vimeridhia uhovyo na uinzi huu!

Kama Kikwete alituahidi kututumikia na siyo kututumia kama ilivyo, basi atutumikie. Kama ameshindwa kwanini tusitafute mwingine ambaye yuko tayari na mwenye uwezo wa kufanya hivyo badala ya kuishi kwenye uinzi?

Tumekuwa tukimuogopa Kikwete hata waziri wake mkuu. Tunawaandika kwa kuzungusha. Tunatumia lugha za kinafiki za mheshimiwa rais angefanya hivi au vile. Jamani, tumwambie hata kama atachukia kuwa anakotupeleka na anavyotuswaga sivyo tulivyokubaliana. Tulimchagua awe mtumishi wetu siyo Bwana wetu kama ilivyo. Anayebishia hili aangalie utendaji mbovu wa serikali ya awamu ya nne tangu iingie madarakani.

Ajiulize ni mangapi tuliyokubaliana yametimizwa zaidi ya dana dana na mazingaombwe kama wengine wayaitavyo. Je kwa Mkapa kuendelea kutuchezea na kutudharau haimaanishi bado anatawala kwa mlango wa nyuma? Je nani anapenda kuwa na hali ya ukatuni (Caricuture). Nani anautaka u-Joice wowowo! Mkumbukeni Joyce Wowowo akinengua baada ya achezeshaye kutia madole kwenye kijisanduku naye akamwaga burudani lakini kwa mikatiko ya matusi. Je tumekuwa wa hovyo kushabikia matusi haya? Namshukuru Mhariri wa Tanzania Daima kwa tahariri yake ya jumapili 26 Januari aliyemtaka Mkapa avunje ukimya. Je atafanya hivyo? Je kama Mkapa na Kikwete wataendelea mchezo huu, utabiri wa mawe kusema kwa namna tofauti na mainzi ya kwenye mzoga unatimia taratibu?

Kwanini Mkapa anaonekana kuwa na kiburi? Je ni kwa kujua uinzi wetu au ukubwa wa kinga ya Kikwete? Je kwanini Kikwete naye anaridhia kadhia hii kama hana mpango wa kuitenda hata zaidi ya hii? Siku njema huonekana asubuhi na siyo jioni. Imetimu miaka zaidi ya miwili tangu Kikwete akabidhiwe nchi. Je kuna ishara gani tokana na matendo ya awamu yake?


Kikwete asijesema nampakazia. Akinipa sababu zenye siha hata mbili za kwanini Mkapa asishughulikiwe na yeye hana mpango wa kuwa Mkapa mwingine miaka ijayo, nitaacha kuuliza swali langu kuu:kwanini Kikwete na Mkapa lao lisiwe moja.

Muda umeisha. Tuachane na uinzi tuuvae usimba tuikomboe nchi yetu toka mikononi mwa akina Mkapa na wenzake ambao wanatucheka badala ya kuomboleza. Yote hii inatokana na makelele ya maizi ilhali mzogo unatafunwa na mbweha.
mpayukaji@yahoo.com

No comments: