The Chant of Savant

Wednesday 2 April 2008

CUF hiyo ndiyo CCM na huyo ndiye Kikwete tangazeni uasi mtakatifu

Anguko la Butiama kuhusiana na muafaka na hali ya mambo nchini linakatisha tamaa, kutisha, kusikitisha na kuchukiza. Chama Cha Wananchi-CUF, kwa mara nyingine, kimekula mbichi tena kwa aibu na fadhaa.

Kwa wanaoijua CCM vizuri na mwenyekiti wake, Jakaya Kikwete, hawakustushwa na kilichotokea baada ya CUF kujipiga kifua na kutoa tamko kuwa sasa mambo safi.

Kimsingi ambacho kimekuwa kimefanyika ni gereshabwege na kupoteza muda ili hatimaye tufikie kipindi cha uchaguzi mkuu wa 2010. Bahati mbaya CUF hawakulijua wala kulibaini hili mapema.

Sasa mambo si mambo. Kilichofanyika ni kutaka kuigawa CUF ionekane ya ovyo kwa wapenzi na wanachama wake. Ni mkakati wa makusudi wa kuzima madai ya haki ya CUF.

Kama CUF hawatatia akilini na kubadili mikakati na shinikizo dhidi ya hujuma na dhuluma ambayo wamekuwa wakifanyiwa takribani miaka zaidi ya kumi sasa, itabakia kuwa historia, hata kama ni chungu, kuwa kilikuwapo Chama Cha Wananchi.

Kwa anayejua jinsi Salmin Amour alivyowadhalilisha na kuwahadaa CUF, bado ataendelea kushangaa ni kitu gani kilikuwa kikiwafanya CUF waiamini CCM tena chini ya uongozi uliobainika kukosa bongo zinazochemka, nia na utashi wa kumaliza mpasuko wa Zanziba.


Kikwete, tulisema. Hana jipya na wala hatakuwa nalo. Hana nia wala uwezo wa kutatua mpasuko uliopo. Hawezi. CCM haiwezi. Watawezaje iwapo wanaitawala Zanziba kwa kutumia kibaraka wao kwa ajili ya maslahi ya chama na siyo nchi? Anayeshuku hili ajiulize Karume anapata wapi jeuri ya kukataa mchakato mzima na yaliyokuwa yamefikiwa.

Kitu kingine cha CUF kutia akilini ni kuangalia namna ya majadiliano yalivyofanyika. Siyo uzushi. Mimi nilikosa imani tangu mwanzo ilipotangazwa tume ya CCM ya majadiliano. Nilishangaa. Mtu kama katibu mkuu wa CCM, Yusuf Makamba anaweza kuwa na jipya gani zaidi ya mipayuko na hadaa za wazi?

CUF ilipoteza kete yake ilipoburuzwa kwenye mjadala baina yake na CCM bila kuwapo msuluhishi mwenye kuheshimiwa kama ilivyofanyika nchini Kenya baina ya Mwai Kibaki na Raila Odinga. Bahati mbaya, CUF na watanzania walidhani wangefikia kile kilichofikiwa na Kenya bila kuangalia namna walivyokuwa wakifanya majadiliano ambayo kimsingi hayakuwa majadiliano kitu bali mkenge. Hapa ndipo unapoona uzembe wa kumpoteza chifu Anyauko Emeka, katibu mkuu wa zamani wa jumuia ya madola.

Sasa kuchele. CUF iachane na kulaani na kutishia. Itafute jibu sahihi hata kama ni kwa machungu. Bila kufanya hivyo muda utapotea na itafika 2010 na CCM itapeta kama kawaida chini ya nyenzo zake za wizi wa kura na vurugu.

Hapa ndipo Maalim Seif anapopaswa kutofautisha ahadi za midomoni na masuala ya kisheria. Masuala mazito kama haya hayawezi kuendeshwa kwa kuaminiana na kauli tamu kama ambayo imekuwa. Na isitoshe, CUF wanachezea kwenye nyavu za wataalamu wa mizengwe, hadaa na jinai. Kama wataendelea na kujipa matumaini ya paka kukalia mkia akaamini yuko kwenye kochi, chama chao kitavurugika na kusambaratika.


Wasi wasi wangu mkubwa ni uongozi wa CUF kugeukwa hata na wanachama ambao kwa muda mrefu wamepewa matumaini yasiyo na tija wala matokeo yaliyokusudiwa. Kinachoendelea ni utoto na upuuzi. Haki haiji kupitia meza ya mazungumzo kama mazungumzo yenyewe yanafanyika kienyeji. Na hapa ndipo CUF ilipobanwa ukutani. Maana haina pa kukimbilia hasa mahakamani kutokana na mahakama zetu kutumika kisiasa.

Kumuamini Kikwete na CCM ni makosa makubwa. Utamwaminije mtu asiyejiamini wala kuaminika? Rejea anavyojipinga kila uchao kwenye maamuzi na ahadi zake. Rejea anavyogeuza mambo mazito kuwa mepesi na mapesi kuwa mazito. Nani alitegemea, kwa mfano, serikali na chama vilivyokithiri kwa ufisadi kujipeleka Mwitongo kuaibika kama ilivyotokea? Mwalimu alizoea kusema: kitu kama hiki kinahitaji roho ya mwendawazimu. Na kweli inahitaji roho ya chizi kufanya yanayofanyika Tanzania. Nani angedhani kuwa CCM na serikali yake vingediriki hata kuwasafisha mafisadi? Wamefanya hivyo bila hata wasi wasi kuwa umma unaweza kuasi. Na bahati yao umma haukuasi. Hivyo basi, kwa mtaji ambao CUF iliishaukusanya Pemba, kinachotakiwa kupata suluhisho na haki ni kuasi kweli kweli bila kujali nani atasema nini.

Bila kuasi CUF watakuwa sawa na fisi wanaofuatilia binadamu anayetingisha mkono wake wakidhani utaanguka wenyewe. Dawa hapa ni kuurukia mkono na kuukata ndipo fisi aule vinginevyo fisi atakula ujuha wake.

Wananchi na wanachama wa CUF, bila shaka watakuwa wamechoka ahadi zitolewazo na uongozi wa CUF. Hesabu miaka iliyopita na mara ambazo ahadi na matumaini vimetolewa. Nini kimetokea zaidi ya taarifa kwa vyombo vya habari huku CUF ikifanya waingereza waitacho to go back to the drawing board? Kweli umma wa wanachama, mashabiki na wananchi wataendelea na kuanza na alifu na ujiti kila mwaka kila msimu kila uchaguzi? thubutu!



CCM Zanziba wako wazi. Waliwahi kusema tena mchana kweupe kuwa hawawezi kuachia madaraka (ulaji) kwa vipande vya karatasi-kura! Hawa ni vichwa ngumu na mahabithi wasiopaswa kuaminiwa hata kwa sekunde moja. Kuwaamini ni sawa na kujidunga kisu tumboni ukidhani ndiyo unamkomoa mbaya wako.

Kwa sasa Kikwete na kundi lake watakuwa wanachekelea walivyofanikiwa kuwalamba CUF chenga la kisigino. Leo tunaambiwa kura ya maoni! Ebo! Ni kura gani ya maoni iliwahi kuheshimika na kupitishwa kwa haki Tanzania? Rejea white paper ya Sumaye zama zile za imla ya Mkapa. Rejea maoni ya kuanzishwa kwa mfumo tasa wa vyama vingi visivyo vyama vingi kitu. Rejea matokeo mbali mbali ya tume ukiondoa tume moja tu ya Mwakyembe. Sasa CUF ni nani hadi CCM ijipinge na kujihujumu? Hata hili la Richmond limewezekana kutokana na ugomvi wa kimaslahi wa mitandao ndani ya chama kwa manufaa ya CCM yenyewe. Hivyo tusifanye makosa kudhani kuwa hata ikipitishwa kura au kuundwa tume itakuja na kile tulichotarajia.

Yote haya yakichanganywa na uwezo mdogo wa Karume na Kikwete ndiyo basi tena.

Vitu vingine vilivyochangia anguko hili ni ile hali unafiki na ujuaji wa pande zote. Kikwete anaona fahari kusuluhisha ya Kenya lakini haoni aibu kushindwa ya nyumbani kwake!

Kwa upande wa CUF uongozi uliteka majadiliano huku ukipuuzia ushauri na mawazo vya wanachama. Nambie ni wapi wanachama wameshirikishwa. Hakuna! Rejea vijana wa CUF walipotaka kuasi pale alipotangazwa Karume mwaka 2005 uongozi ukawazuia ukiwataka wawe na subira. Subira sasa imezaa nini zaidi ya mparaganyiko na kukata tamaa?

Tuhitimishe kwa kuitaka CCM iache dana dana na unafiki na mizengwe. Nchi inaweza kutumbukia kwenye maasi kiasi cha kutotawalika.

Kwa upande wa CUF ni kuachana na mbinu na mikakati ya kizamani ya kutaka umaarufu. Badala yake ni kutia ngumu na kufanya visiwani kusitawalike ili CCM watie akili na kusalimu amri. Simbuliko halisimbuliki ila kwa mikukuliko. Wahenga waliasa. Na ni mpumbavu ang’atwaye na nyoka kwenye tundu moja. Na isitoshe ni upumbavu kuweka mayai yote kwenye pakacha moja. CUF wameona hasara ya kukinzana na hekima hii.

Umefika wakati wa maasi matakatifu dhidi ya kichwa ngumu, mizengwe na jinai za CCM na watawala wake wanaoichukulia nchi kama mashamba yao binafsi. Alluta continua.

No comments: