The Chant of Savant

Monday 21 April 2008

Mihimili ya uovu yaanza kumomonyoka bado wa Kikwete mwenyewe

Iliangushwa Babeli itakuwa mhimili huu wa kujuana kulindana katika jinai?

Mihimili wa utawala wa rais Jakaya Kikwete yaani marafiki na washirika wake inaanza kumomonyoka kwa kasi na ari ya ajabu!

Alianza baba lao, Edward Lowassa na wenzake, Nazir Karamagi, Ibrahim Msabaha. Walifuatia Basil Pesambili Mramba, Kingunge Ngombale Mwiru, Rostam Aziz na wengine waliokumbwa na shoka la Mwakyembe.

Sasa tunashuhudia, Andrew Chenge akiwekwa uchi hadharani kama ishara ya unafiki, uroho, roho mbaya ufisi na upanya wa watawala wetu.

Tulionya na kusema. Tulionekana wachochezi na wambea. Yako wapi? Bado mhimili babu lao. Huu ni Benjamin Mkapa, Fredrick Sumaye, Anna Mkapa, Daniel Yona, Juma Ngasongwa, Abdallah Kigoda na wengine ambao mikono na saini zao vimeiweka nchi yetu utumwani.

Na bado. Kuna mhimili muungu wa mihimili yote ambao si mwingine ni Jakaya Kikwete, Lawrence Masha, Yusuf Makamba na wengine.

Mhimili wa kwanza ulisifika kwa kuwa king maker kwa maana ya kuchangisha pesa ya kumuwezesha muungu wa mihimili kukaa kwenye kiti cha enzi baada ya kutembeza takrima aliyokuja kuifuta baada ya kufanikisha malengo yake.

Mhimili wa pili unasifika unajulikana kwa kujenga mazingira ya kukusanyia ngawira ya kumwezesha muungu wa mihimili kwa makubaliano ya kuulinda pale ulipotoka kwenye kiti cha enzi ulichokiacha kimejaa uchafu hakuna mfano.


Kwanini nimeamua kumuita Kikwete muungu wa mihimili ya waovu wanaoipeleka Tanzania kuzimu? Si kwa chuki wala chuku bali kumuonyesha umma unavyomuona baada ya kutamka wazi wazi kuwa hatamchunguza wala kumfungulia mashitaka rais mstaafu Benjamin Mkapa anayetuhumiwa karibu kuwa nyuma ya kila wizi alioozoea kuuita ubinafsishaji tusijue ni ubinfsi na ufisi-Ufisadi.

Sasa kumekucha. Ngoma hii siyo ya watoto. Ni ngoma ya wakubwa na wakubwa hasa.

Umma ulionya kuwa serikali ya Kikwete licha ya kujaa makapi ya serikali iliyopita, umesheheni kila aina ya mapanya, fisi na mapapa wanaoitumia nchi yetu kwa faida binafsi. Bahati mbaya sana. Kikwete hakustuka. Bado wachambuzi wanajiuliza kwanini? Je naye ni mshirika wa mihimili hii? Wapo wanaosema huwezi kugusa kidevu bila kugusa shavu. Wanasema wazi jinsi Kikwete na chama chake cha Mapinduzi-CCM wanavyotajwa karibu katika kila jinai ya kuliibia taifa. Hajakanusha wala kutoa maelezo. Kwanini? Nani anajua?

Kikwete amekuwa utata wa ajabu. Alipokuwa akiingia madarakani alijionyesha kama mkombozi tusijue kilichokuwa nyuma yake!

Kuna kisa kimoja cha askari wa kimarekani. Waliingia kwenye nchi moja wakiwa wamevalia fulani zilizoandikwa kifuani Messenger of peace. wakati wakiingia wananchi wa nchi ile walifurahi sana kuona walivyokuwa wamepata walinzi wa amani.

Baada ya kuingia kwenye malango makuu ya mji mkuu wa nchi ile, umma ulichanganyikiwa na kuanza kujilaumu kwa kutokuwa makini. Kwanini fulana zile zile zilikuwa zimeandikwa mgongoni Lincenced to kill au tunaruhusiwa kuua!

Ebo! Wenye akili walianza kustuka kuuingia mkenge.

Ukiangalia kauli mbiu ya Kikwete ya kasi mpya nguvu mpya na ari mpya na kuwapeleka wananchi Kanani unamuona messenger of development. Lakini ukiangalia kinachoendelea hasa masuala ya kuachiwa na kubadilishiwa kesi ya mauaji ya best wa Kikwete aitwaye Ditopile Mzuzuri, kutorejeshwa kwa nyumba zetu zilizoibiwa na Mkapa,kutotimiza ahadi hata moja ya zile alizoahidi, kufumka kwa kashfa kama Richmonduli, EPA na sasa ya Chenge na pauni zaidi ya 500,000 unaanza kujua nini maana ya lincenced to steal. Ndiyo. Kwanini isiwe hivyo iwapo Kikwete amekuwa kama kasri la wezi?

Tumkumbushe. Alipoingia madarakani tulimtahadharisha na kumteua rafiki yake Edward Lowassa kuwa waziri mkuu baada ya kuzagaa uvumi kuwa angemteua. Alitudharau kwa sababu anazojua na kumteua.

Tulionya kuwa alivitumia vyombo vya habari malaya kumpamba na kumlazimisha kwa wananchi. Alitudharau pia akamteua kiranja mkuu wa kundi hili shawishi, Salva Rweyemamu.

Baada ya siku 100 ikulu Kikwete alianza kujifunua. Tulianza kupata kihoro kama wananchi wa nchi ya kwenye mfano. Tulianza kumuona mtu asiye makini wala msimamo. Mara tukaona mambo yaliyokuwa yametuchusha na kutukera chini ya utawala wa Mkapa.

Hakuna ubishi kuwa Mkapa alijikuta alipo baada ya kupewa tunda na mama. Mama alianza na kampuni ndogo iitwayo Economic Opportunities For The First Lady. Mara mama wa sasa naye akaja na sumu ile ile ya kuanzisha MAWA au Maulaji ya Wake wa wakubwa.

Tulihanikiza. Mambo si mambo. Mwenye mapenzi haoni. Mara tukasikia mke na mtoto wa Kikwete wakigombania vyeo chamani! Lahaula! Waliosali wakaanza kusali, wa kulalamika tukalalamika, wa kumkumbuka Nyerere wakaanza kumkumbuka. Na mwisho wa yote tukajikuta hatuna nchi kitu bali jina. Niambie iko wapi Tanzania ya watanzania zaidi ya Tanzania ya mafisadi?

Nchi ya mafisadi: kwanini ufisadi hauishi Tanzania?

Tukirejea kwenye mhimili muungu wa mihimili, ukweli ni kwamba nao utamomonyoka. Kwanini? Kwa sababu utasababisha nchi kutotawalika wala kuaminika kwa washitiri kiasi cha kuamua kuuporomosha. Na ushahidi katika hili uko wazi. Tunaambiwa Uingereza imeamua kumchunguza na kumuanika king maker mwingine wa Kikwete, Chenge. Hii maana yake ni kutaka kuusutua umma wa watanzania kufanya kweli.

Hili ni suto la kiutu uzima. Je watafuata wangapi? Time will surely tell.

kitu ambacho wahusika wanashindwa kuelewa ni kwamba huwezi ukapendwa na kulindwa na wafadhili kama huna ubavu wa kulinda maslahi yao. Rejea juzi juzi wananchi kuvamia mgodi wa Buzwagi na kuporomosha ukuta mgodini.

Hii ni ushahidi kuwa wafadhili hawa imani na usalama wa mali zao hapa nchini. Na kweli hakuna usalama. Ukitaka kujua nchi inakwenda wapi, soma maoni ya watanzania mbali mbali wanaposoma makala zenye kupiga kwenye donda. Wapo wanaodiriki hata kuomba silaha waingie msituni. Japo hili si jibu lakini wapo wenye hamu ya kufanya hivyo baada ya kugundua wamesalitiwa.

Leo Tanzania inaongoza kwa kuwalangua wananchi na watumiaji umeme. Kisa? Mkapa na akina Chenge walileta Net Group solution kuihanithi Tanesco. Je hapa wafadhili wataridhika na jinai hii inayogusa maslahi yao moja kwa moja?

Laiti Kikwete angekubali yaishe akawasulubu mafisadi hata kama ni marafiki zake angeweza kunusuru utawala wake. Lakini inavyoonyesha hana mpango huo. Anaogopa wasimsulubu maana wanamjua kuliko tunayemjua sisi. Je ataendelea na kigugumizi hiki wakati mambo yanaharibika hadi lini? Ni suala la wakati.

Kikwete amekuwa kibri tu. Amepewa mifano ya akina Bingu wa Mutharika walioingizwa madarakani kwa mbinu chafu wakaamua kujifua na kujiosha kiasi cha kuwavutia wamalawi. Hata Levy Mwanawasa aliingizwa na Fredrick Chiluba akitegemea amfanyie yale anayofanya Kikwete kwa Mkapa.

Baada ya kuchemsha bongo na kuona hawezi kushindana na umma akashinda, aliamua kumtosa Chiluba na kurejesha heshima ya nchi yake na yake.

Kikwete yote haya hayaelewi. Asiyesikia la mkuu? Je umefika wakati wa wananchi kurejesha hadhi, mali na nchi yao hata kama ni kwa migongano?

Inawezekana. Maana wamejitahidi kuwa wavumilivu. Sasa wanaendelea kulishwa mbovu. Je wataendelea kuwa majuha hivyo? Thubutu!

Tumalizie kwa kumtaka Kikwete afanye kile waingereza huita U-turn vinginevyo baada ya mihimili yake mikuu kumomonyoka naye atamomonyoka. Maana wahenga walisema; mwanzo wa ngoma lele. La Chenge laweza kuwa kifyatuzi (trigger) cha hasira za watanzania kapuku wanaokula mlo mmoja kama komba. Kwa ufupi umaskini wa Tanzania siyo wa kuumbwa na Mungu bali wa kuchongwa na waroho wachache wanaoanza kuumbuka mmoja mmoja. Kutegeua kitendawili ni kumchunguza baba wa mihimili, Benjamin Mkapa kabla umma haujaamua kuwashughulikia wote mbebwa na mbebaji.

1 comment:

Anonymous said...

Ee bana ndiyo!! I feel you mayn!!