The Chant of Savant

Wednesday 7 May 2008

JK, kwanini unakosa usingizi kwa dhambi za Mkapa?

UFISADI uliotikisa nchi yetu wa BoT ni mkubwa na wa kutisha barani Afrika. Hauufikii hata ule uliofanywa na Gavana wa zamani wa Benki ya Kenya (CBK), Eric Kotut, akishirikiana na rais wa zamani wa nchi hiyo, Daniel arap Moi, na maofisa wengine wa serikali yake.

Kama ada, kwenye ufisadi wa Kenya ambapo uchumi wa nchi hiyo ulikuwa almanusura kusambaratika, uliwezeshwa na uongozi wa juu, yaani rais mwenyewe. Rais akiwa ananufaika na kujua kilichokuwa kikiendelea, alimtumia gavana na waziri wake wa pesa, Profesa George Saitoti ambaye pia alikuwa makamu wa rais kufanikisha jinai hii.

Kadhalika, ili kuwaziba midomo Wakenya na kuwapumbaza, mfanyabiashara tapeli wa Kihindi ajulikanaye kama Kamlesh Pattni, alihusishwa. Hali hii ilivutia wachezaji wengi kwenye mchezo huu mchafu. Watoto, kama ilivyo kwa Kampuni ya Fosnik ya Mkapa mdogo, na marafiki wa Moi nao hawakukaa kando.

Kampuni maarufu kama Goldenberg ya Moi, Kotut na Biwott (kama alivyo Yona) na Saitoti (kama alivyo Mramba) na mkuu wa zamani wa usalama, Joseph Kanyotu, iliingia baharini kunasa samaki wa bwerere.

Tukiachana na ufisadi wa Kenya, ngoja tuurejee wa Tanzania ambapo ule wa Kenya unaweza kutupa mwanga wa ni nani wanahusika, licha ya gavana aliyeko matatani, Daudi Ballali.

Kabla ya kuzama kwenye tafakuri tujiulize, ni nani alimtengeneza Ballali na kwa nini? Habari kutoka Washington alipokuwa akifanya kazi Ballali zinadai aliunganishwa laini hii na rafiki yake wa kike aliyekuja kuwa mkewe baadaye.

Hivyo bila kumung’unya maneno aliyemtengeneza Ballali ni rais, yaani Mkapa, aliyemtoa Washington na kumteua kuwa gavana wa BoT.

Iwe alijua au la, hawezi kulikwepa hili. Na isitoshe Ballali alikuwa akifanya kazi kwa niaba ya rais chini ya dhana ya uwajibikaji.

Kwa hiyo, hakuna ubishi: kazi ya Ballali ni ya Mkapa na kama isingekuwa hivyo asingeendelea kumuamini na kumuacha madarakani.

Mtu wa pili kwa mujibu wa kilichotokea Kenya atakuwa ni waziri wa fedha wa wakati ule, Basil Pesambili Mramba, ambaye ni rafiki mkubwa wa Mkapa. Naye akiwa waziri mwenye dhamana hakuna shaka, alijua kilichokuwa kikiendelea na alikubaliana nacho.

Yupo pia waziri wa mipango na uchumi ambaye kwa wakati ule alikuwa Dk. Abdallah Kigoda. Huyu naye alikuwa karibu na Wizara ya Fedha, hivyo na BoT.

Kwa upande wa wachezaji kutoka kwenye kada ya biashara, hakuna shaka kuwa Jeetu Patel na wengine watakaotajwa baadaye, hawezi kukwepa kuwa nyuma ya dili hili. Ukitaka kujua anaingiaje na kufiti, angalia uhusiano wake na ikulu wakati ule.

Nchini Kenya mkuu wa usalama alihusika. Je, mkuu wetu wa usalama wakati ule hakuhusika iwapo kilichokuwa kinafanyika kilikuwa kinatishia usalama wa nchi, hivyo kuangukia chini ya idara yake? Kama hakujua, alikuwa akilinda usalama gani na alilipwa kwa nini?

Ukitaka kujua kuwa wahusika hapo juu walihusika na kunufaika vipi, chunguza mali zao. Utakuta wengi ni matajiri wa kutupwa.

Wakati Mkapa akiingia Ikulu aliitwa Mr. Clean. Je, alikuwaje wakati akitoka? Hakuna ubishi kuwa kwa kugundulika zana zake kama ANBEN, Fosnik na Tanpower, hakuwa tena Mr. Clean .

Kitu kingine kinachomuunganisha Mkapa moja kwa moja ni ile staili yake ya kushughulikia ufisadi. Tukikumbuka alivyokemea vyombo vya habari akiwa mkutanoni mkoani Singida, tunajituka tukisema bila shaka kuwa alijua na kuridhika na kadhia hii. Maana alisema: vyombo vya habari vinavyodai serikali yake imeoza kwa ufisadi, navyo vijiangalie na kueleza vilivyopata mitaji ya kuanzishwa kwake.

Kitu kingine kinachoonyesha kuwa serikali ya Mkapa ilijua na kuridhia kilichokuwa kikiendelea, ni maneno ya aliyekuwa waziri wa biashara na viwanda wakati ule, Idd Mohamed Simba.

Alidai kuwa wafanyabiashara wa Kihindi wapatao kumi walikuwa wakimiliki uchumi wa Tanzania. Je, hapa serikali haikujua walivyokuwa wakihomora pesa yetu wakishirikiana na watendaji wa serikali yenyewe?

Na kuonyesha kuwa yaliyosemwa hayakuwa uzushi, hakuna aliyejitokeza kuhoji wala kukanusha ukweli huu mzito! Nani angekanusha iwapo kama Moi, Mkapa alikuwa akitetemekewa na watendaji wake waliomuogopa sana?

Sasa turejee kwa Rais Jakaya Kikwete. Japo hakumteua Ballali, aliridhika na kazi yake kwa miaka miwili mizima kabla ya kushinikizwa kutengua uteuzi wake wenye utata.

Wachambuzi wengi wanakataa kukubali kuwa Kikwete amemchukulia hatua Ballali zaidi ya Ballali mwenyewe kugundua maji yamezidi unga.

Maana kabla ya kutenguliwa uteuzi wake, zilizagaa habari kuwa alikuwa ameandika barua ya kutaka kujiuzulu.

Na huu ni ukweli. Maana ukiangalia mazingira ya kutoroka kwa Ballali kwenda Marekani kutibiwa ‘ugonjwa’ usiojulikana na hospitali isiyojulikana wakati ni mtumishi wa serikali, unagundua janja nzima.

Je, kama Kikwete hakujua wala kuridhika na kazi ya Ballali, kwanini alimbakiza ofisini hadi alazimike kutengua uteuzi na si kumfukuza? Kunani hapa?

Kikwete ama ana masilahi au anaponzwa na washauri wake. Maana ukiangalia hata watu kama Bazil Mramba, Andrew Chenge - mwanasheria mkuu wa zamani wa serikali aliyeitia nchi matatani kiuchumi kwa kuridhia kusainiwa mikataba bomu, unabaki kushangaa ni kwanini watu hawa bado wanaachwa uraiani hadi leo!

Tukirejea kwa Rais Kikwete, kwanini anakubali kukosa usingizi kwa makosa yaliyotendwa na mtangulizi wake na asiseme ukweli kuwa aliyarithi? Au ni kwa vile alipoingia madarakani na kukuta uchafu huu naye alijikalia kimya?

Kwanini kama hakuwa na jinsi alivyokuwa akinufaika au hata wale waliomzunguka? Ieleweke kuwa huu ni uchambuzi na si kumuingiza moja kwa moja rais. Tunafanya hivyo ili kupata jibu ambalo laweza kuwa msaada kwa nchi yetu.

Kwa upande wa Mkapa, najua hatajihangaisha na kukanusha au kutoa maelezo kwa vile Kikwete alikwisha kumhakikishia usalama kwa sababu wanazozijua wenyewe. Je, hatua ya Kikwete kuendelea kusulubiwa na kadhia ya BoT inaweza kuwa nayo sehemu ya kumlinda Mkapa kwa kila jambo na kila hali?

Kuna haja ya Watanzania kujua kinachoendelea na kilichosababisha wizi huu. Maana iliyoibiwa ni pesa yao, si ya Kikwete, Mkapa Mramba, Ballali wala watawala.

Hakika Kikwete atajikuta matatani zaidi kama hataamua kupambana na ufisadi vilivyo badala ya kugusa gusa. Leo kwa mfano mawaziri kama Nazir Karamagi, Dk. Ibrahim Msabaha, Chenge na hata Edward Lowassa, wamejiuzulu kutokana na kashfa za ufisadi, lakini kwanini wasiachie na ubunge? Wameshindwa kuaminika kwenye uwaziri, wataaminikaje kwenye ubunge?

Tunamshauri rais achukue mfano kutoka kwa Thabo Mbeki, Rais wa Afrika Kusini. Ilipogundulika msaidizi wake na makamu wake, Jacob Zuma, alidaiwa kufanya ufisadi na jinai ya ubakaji, hakumlinda, bali kuacha sheria ichukue mkondo wake baada ya kumwajibisha kwa kumfurusha.

Kikwete watimue mafisadi waliobaki, maana bado wako wengi ndani ya baraza lako, lakini pia waliojiuzulu wasiachwe waendelee kutafuna vijisenti vyetu. Hawa ndio wanaokuponza.

Source: Tanzania Daima Mei 7, 2008.

No comments: