The Chant of Savant

Wednesday 28 May 2008

Mkapa tutajie hao uliokataa kuwapendelea

Angalau rais mstaafu Benjamin Mkapa ameanza kuvunja ukimya na kuelekea kuweka mambo hadharani ingawa ni kwa njia rahisi na inayokosa ukweli. Hivi karibuni alikaririwa alipokuwa akihutubia wananchi kijijini kwake Lupaso akisema, "Msisikilize uongo huo kwa sababu hauna msingi wowote isipokuwa ni chuki …hasa inayotokana na watu ambao walifikiri nitawapendelea … sikuwapendelea,"

"Sina uwezo wa fedha ingawa najua mnasikia na kusoma mengi …naishi kwa pensheni yangu kutoka serikalini kutokana na kuwa kiongozi kwa miaka 10 ambayo hata Mzee Mwinyi anaishi hivyo maana sisi sote ni wastaafu. Huo (uvumi) ni uongo …uongo ….uongo ….uongo …uongo….uongo….uongo," aliendelea Mkapa.

Hivi kwanini wanasiasa wetu tena watu wazima na heshima zao wanafanya mambo ya kitoto halafu na kutaka watendewe kiutu uzima? Mkapa ili usionekana muongo tafadhali wataje hao uliokataa kuwapendelea ukajipendelea wewe mkeo, wanao na marafiki zako.

Hivi kweli inaingia akilini Mkapa kusema kuwa yanayodaiwa kufanywa naye ni uongo? Ni ajabu! Mbona kwa mfano ukweli uko wazi kuwa Mkapa familia yake na marafiki zake walijitwalia Mgodi wa kuchimba makaa ya mawe wa Kiwira? Je na ANBEN, Tanpower na Fosnik nao ni uongo?


Mkapa ninayemheshimu sana anaendelea kutugeuza majuha kwa kusema eti anaishi kwa pensheni! Ebo hivi Mkapa anajua maana ya kuishi kwa pensheni au ameamua kujisemea? Mbona inajulikana kuwa Mkapa ni mjasiriamali mwenye makampuni ya familia yaliyotajwa hapo juu?

Na kwanini Mkapa ajibie kwenye mkutano wa kisiasa badala ya kuandaa mkutano maalumu na vyombo vya habari kama alivyofanya Hayati Mwalimu Julius Nyerere aliposhutumiwa na marehemu Oscar Kambona kuwa alikuwa na pesa nyingi kwenye akauti zake kwenye mabenki ya Ulaya?

Shutuma zinazomkabili Mkapa mkewe mwanae, mkamwana, kivyele na rafiki yake Daniel Yona ni kubwa kiasi cha kutopaswa kujibiwa kwa hotuba ya mistari mitatu. Mbona Mkapa anafanya mzaha kwenye ukweli tena unaonuka?

Mkapa amekuwa na kiburi hata kabla ya kuingia madarakani na baada ya kuondoka madarakani. Je nini kinampa kiburi Mkapa kiasi cha kuanza kutukejeli na kututafutia sababu?

Mwandishi wa makala hii hajawahi kwenda kwa Mkapa kuomba hisani yoyote. Na kama Mkapa anaona wanaodai alitumia vibaya madaraka yake kuwa wenzake aliokataa kuwapendelea kama anavyosema, ajue siyo wote. Sisi wengine hatujawahi kutaka hisani wala msaada wowote toka kwa Mkapa zaidi ya kutekeleza wajibu wetu kwetu na kwa taifa letu.

Madai ya Mkapa kusema ukweli ni matusi zaidi ya majibu. Wanaodai Mkapa alitumia vibaya ofisi ya rais siyo wanasiasa wenzake bali watanzania wenye Tanzania yao.

Kwa mtu anayemjua Mkapa kama bingwa wa kujenga na kubomoa hoja, anashangaa ameingiwa na balaa gani hadi kutoa majibu uchwara yasiyolingana na uwezo wake aliowahi kuuonyesha. Au ni yale kuwa mwizi akitiwa kamba hujikuta akiwa mwizi tu hata kama angekuwa mwanasheria?
Je majibu ya Mkapa ni majibu ya kuingia akilini, kejeli au matokeo ya kihoro cha kubanwa na kushushwa heshima?

Nadhani Mkapa alipaswa kuingia kwenye undani wa madai yanayotolewa dhidi yake.

Kwa mfano alipaswa kukiri kuwa hana kampuni ya ANBEN yaani Anna (mkewe) na Benjamin (yeye mwenyewe) wala Fosnik inayomilikiwa na mwanae (Nicholas) na mkewe (Foster).

Mkapa pia alipaswa kueleza anachojua kuhusiana na kampuni la kiwizi la Tanpower na utwaliwaji wa mgodi wa makaa ya mawe wa Kiwira.

Je majibu ya Mkapa ni tahadhari kuwa mambo jikoni yameisha wekwa sawa kwa kuchomoa kumbukumbu kwa msajili kiasi cha makampuni husika kutokuwapo?

Kama Mkapa amesahau au anata umma usahau madai yanayomkabili wacha tumkubushe.

Anadaiwa kuiingiza nchi kwenye mikataba ya kiwizi yenye kulitia hasara taifa ya uwekezaji. Arejee kugundulikwa kwa mshauri wake mkuu kisheria mwanasheria mkuu wa zamani waziri wa zamani wa miundo mbinu Andrew Chenge na wengine wanaoendelea kuchunguzwa.

Pia Mkapa arejee kutamka wazi kwa serikali kuwa mikataba iliyoingiwa wakati wa utawala wake ina mazingira yote ya rushwa. Na haya yalitamkwa hata na rais Jakaya Kikwete ambaye sijui kama kuna hisani aliyomnyima zaidi ya kumpa uwaziri wa mambo ya nchi za nje kwa miaka kumi.

Pia anaweza kurejea kukiri hivi karibuni kwa rafiki na msaidizi wake mkuu waziri mkuu wa zamani Fredrick Sumaye aliyesema wawekezaji ni wezi wa raslimali zetu. Huyu atakuwa ana chuki gani iwapo alipewa uwaziri mkuu licha ya kupwaya kwa miaka kumi?

Mkapa pia arejee madai ya kumiliki jumba la kifahari kule Lushoto na Dar es salaam.

Pia Mkapa ataje sababu iliyomfanya kutaja mali zake wakati wa kuingia madarakani akashindwa kufanya hivyo wakati alipoondoka ikulu kimya kimya bila hata kukabidhi.

Mbona makosa ya Mkapa yako wazi hata kwa kipofu?

Kama kuna waliomshauri Mkapa kujibu hoja kijuu juu na kiutani, basi wamezidi kumuingiza kwenye matatizo. Huenda Mkapa hachelei lolote kutokana na rais Kikwete kumkingia kifua ingawa hili nalo lina warakini kama maneno ya hivi karibuni ya waziri mkuu Mizengo Pinda yatakuwa na ukweli na siyo danganya toto.

Hapa napo kuna mshkeli. Watu wanauliza kauli ya Pinda itaanza kufanyiwa kazi lini?

Mkapa kama mtawala mstaafu anayehusishwa na ufisadi anaonekana kupitwa na wakati kiasi cha kuamua kuzidi kuwakejeli watanzania aliozoea kuwaambia wana uvivu wa kufikiri asijue naye ni mtanzania!

Mkapa badala ya kuanza kutafuta sababu za uongo na ukweli ama angesema ukweli na kutubia ili asamehewe huku akirejesha mali za umma anazomilki kama vile mgodi wa Kiwira na kuvunja makampuni yanayotia shaka anayomiliki.

Kama Mkapa anaamini hao ‘wanaomzushia’ wanasema uongo kwanini basi asiwashitaki mahakamani ili kusafisha jina lake?

Na kwanini Mkapa amekuwa kimya muda mrefu kiasi cha kujenga dhana nzima kuwa yanayodaiwa ni kweli? Naomba nisisitize kuwa hata majibu aliyotoa Mkapa si majibu bali madai tu. Maana njia aliyotumia na namna alivyoyatoa siyo sahihi.

Kama Mkapa anataka tumuelewe, basi afanye yafuatayo:
Mosi, ataje mali zake na namna zilivyopatikana.
Pili, awashitaki wanaomzushia ili kusafisha jina lake.
Tatu, atoe maelezo juu ya utata unaotokana na mikataba iliyoingiwa na serikali yake kiasi cha kuilazimisha serikali ya sasa kufanya mazungumzo upya na wawekezaji ili kuingiza vipengelee vyenye maslahi kwa taifa.

Nne, atoe taarifa ya jumla ya utendaji wa serikali yake ambayo alipaswa kuitoa siku alipoondoka ikulu.

Tano, akubali kuchunguzwa ili ukweli ujulikane haki itendeke na kumuweka huru.

sita Mkapa atoe mwanga juu ya kupendelea na kutopendelea. Awataje aliowapendelea na alikataa kuwapendelea ili isijengeke dhana kuwa utawala wake ulikuwa wa kupendeleana na kulipizana visasi. Maana ukiangalia madai ya Mkapa kuhusiana na hili ni mazito na yanaweza kuchukuliwa kuwa kweli.

Ili umma umuelewe, awataje hawa wanaomchafulia jina ili wajulikane. Na inavyoonekana Mkapa anawajua wabaya wake hata sababu za kufikia kutoa shutuma nzito hivi.

Mwisho Mkapa aelewe yeye siyo mtu wa kawaida. Hivyo na anachosema lazima si cha kawaida.
Mwisho kabisa tunamtaka Mkapa ajibu hoja (madai) badala ya kuzitafutia uhalali katika visingizio na kinachoonekana kuwa uongo hata kutapa tapa.

Kwa ajili ya gazeti la Tazama.

No comments: