The Chant of Savant

Wednesday 23 July 2008

Kikwete chaguo la Mungu ingawa......


HAKUNA ubishi kwa hali ilivyo katika nchi yetu hasa hali mbaya ya Chama Cha Mapinduzi, kuna uwezekano ukawa mwanzo wa mwisho wa zama na enzi zake.

Kuna kisa maarufu cha mtoto wa mchonga na muuza sanamu wa huko Ukaldayo. Huyu bwana mdogo alichukia masanamu. Yalikuwa yakiabudiwa wakati ule. Ilikuwa ni kufuru kwake na Mungu.

Katika jitihada za kuwaelimisha watu wa kwao, kijana huyu kwa makusudi alipanga kuyavunjilia mbali masanamu hayo.

Wanazuoni hudai kijana huyu shupavu alitumwa na Mungu kuwafungua macho ndugu zake na kuangamiza kufuru na machukizo yaliyokuwa yakifanyika kwa kuabudia sanamu hizo.

Siku moja wakati wazazi na ndugu zake wametoka, kijana huyu aliamua kuyavunjilia mbali masanamu yote isipokuwa kubwa lao. Baada ya kumaliza kazi ya kuyasambaratisha, alichukua shoka alilotumia na kulivisha sanamu kubwa na akaondoka.

Baba yake alipofika na kukuta zahama iliyoyakuta masanamu yake yaliyokuwa miungu wake, alishangaa na kumuita yule kijana aeleze kulikoni. Yule kijana alipofika alimwambia baba yake aliulize lile sanamu lililokuwa limevaa shoka!

Baba mtu alishangaa jibu hili na kuhoji sanamu lisilo hai lingewezaje kuyavunja mengine? Kijana alimjibu: Kama sanamu halina uwezo, hivyo ni kwanini walikuwa wakiyaabudu? Huo ulikuwa mwisho wa ibada za masanamu na ukombozi.

Tukija kwenye mada yetu kuwa Kikwete ni chaguo la Mungu, tunakuta kuwa kwa staili yake ya kutawala, uwezekano ni mkubwa wa chama tawala CCM kusambaratika na kuondolewa madarakani kama upinzani utajipanga vizuri.

Laiti kama kutakuwa na upinzani wenye lishe na mikakati hai na inayowezekana, Tanzania kwa mara ya kwanza inaweza kushuhudia kishindo walichosikia Wakenya mwaka 2002 ilipoangushwa KANU.

Kazi ya kusambaratisha CCM imeishaanza na aliyeianzisha na atakayeifanikisha ni Kikwete, ingawa ni jambo la bahati mbaya sana kwamba ‘kijana wetu’ huyo halijui hilo na pengine anaweza akadhani hizi ni hadithi za kufikirika.

Ingawa waliomsifia Kikwete kuwa alichaguliwa na Mungu walifanya hivyo kwa kubembeleza maslahi na kujikomba, walishindwa kujua upande wa pili kuwa alichaguliwa kubomoa si kujenga. Rejea serikali yake kukumbwa na utitiri wa kashfa na isizishughulikie. Rejea hali za Watanzania kuzidi kudhoofu vibaya sana hata kufika hatua yeye mwenyewe kukiri kwamba mambo ni magumu na watu wanapaswa kuvumilia.

Rejea mafisadi kuwa na nguvu kwa serikali yake hata kuliko umma.

Kikwete ama kwa kujua au kutojua amekuwa akitawala kwa mtindo wa bahati nasibu. Amekuwa mgumu wa kujifunza hata kubadilika. Bahati mbaya hakujifunza toka kwa mtangulizi wake Rais mstaafu Benjamin Mkapa wala hali iliyopo sasa na nchi jirani ya Kenya.

Hii ni heri kwa wapenda mabadiliko na msiba kwa CCM ambayo kwa kiasi fulani licha ya kuzeeka imechusha na kuchoka. Imeishiwa mvuto, ikapoteza sera na kisha kukwama kimikakati. Imegeuka dude kubwa linyonyalo damu za Watanzania.

Rejea kuhusishwa kwake na ufisadi wa EPA chini ya kampuni yake ya Deep Green Finance. Rejea kushinda uchaguzi kwa kutegemea takrima huku Zanzibar ikitegemea mtutu wa bunduki na ukandamizaji mkubwa. Rejea kuibuka kwa mitandao ya ndani kwa ndani ya chama inayotishia kukisambaratisha. Rejea ukosefu wa sera, falsafa na visheni vya kutawalia. Rejea mtindo mchafu wa kulindana na kufadhiliana bila kujali maslahi ya taifa.

Wakati wa utawala wa awamu ya kwanza chini ya Mwalimu Julius Nyerere tulizoea siasa za vuguvugu za ukombozi wa umma na nchi jirani. Tulikuwa na chama kilichokuwa kimebobea kwenye ukombozi wa kweli. Kwa hakika CCM na kabla yake TANU ya Nyerere si hii tunayoiona leo kwa Kikwete na jeshi la wanasiasa wenzake.

Baada ya kung’atuka na hatimaye kufariki dunia kwa mwalimu, chama alichokiasisi kilitekwa na wachuuzi wa roho za watu, kiasi cha kubobea kwenye jinai hii ya kuiibia umma. Rejea ubinafshishaji kichaa uliofanywa na awamu mbili zilizofuatia kabla ya hii ambayo hata baada ya Nyerere mwenyewe kulia sana wakati akiwa hai hakuna hata mmoja aliyesikia kilio chake.

Rejea wakubwa wa serikali na chama kuanza kutumia nafasi zao kuuibia umma na kujitajirisha huku umma ukitopea kwenye lindi la umaskini wa kunuka. Hapa mfano wa karibu ni kadhia ya Mkapa na familia yake; hata kinachoendelea chini ya Kikwete na jinsi familia yake inavyoanza kuiranda ya Mkapa. Rejea NGO ya mke wa rais ambayo ameonywa aifute na akakaa kimya.

Badala ya CCM kuendelea na siasa za ukombozi, imejiingiza kwenye siasa nyemelezi na angamizi!

Nani angetegemea wala kuamini kuwa nchi kama Msumbiji na Uganda ambazo licha ya kuzikomboa hazina rasilimali nyingi kama zetu zingetuzidi kiuchumi?

Huu ni ushahidi tosha wa ukosefu wa mipango na unyemelezi wa CCM kama chama. Ingawa ni aibu, huu ndiyo ukweli. Hebu angalia nchi kama Kenya ambayo ikiunganishwa na Uganda bado haifikii ukubwa wa Tanzania hata kwa rasilimali, inavyotuhenyesha kiasi cha kuiogopa na kuitegemea. Ni aibu ya mwaka.

Tukirejea kwa Kikwete, yeye kama kijana mvunja masanamu, badala ya kuyabomoa masanamu, ameyapa mashoka yabomoane yenyewe kwa yenyewe yeye akiangalia na kuchekelea!

Tofauti na kijana mvunja masanamu, yeye hana baba wa kumgombeza wala umma wa kutishia usalama wake, kwa kusababisha masanamu kuvunjika. Kikwete ana faida moja katika hili. Kama kazi yake ikifanikiwa italeta ukombozi bila manung’uniko na mabishano kama ilivyokuwa kwa yule kijana.

Wanafanana katika moja. Kazi zao zitaleta mwanga na kufungua mboni za kaumu zao.

Nje ya mada, hakuna jambo limenikera kunisikitisha, kunichefua na kunihuzunisha kama kugundulika kwa wizi unaofanywa na kampuni ya Mama Anna Mkapa dhidi ya walimu maskini.

Sasa umefika wakati kwa serikali kuacha mchezo na maisha yetu. Imshughulikie Mkapa na familia yake. Maana karibu kila uchafu nyuma yake kuna jina Mkapa ama kushiriki kwake, mkewe, watoto wake au marafiki zake.

Inakera kiasi cha kuanza kuhoji nia hasa ya Rais Kikwete kwa Watanzania. Aeleze kama yuko kulinda ufisadi au umma uliomchagua kwa kishindo.

Tuhitimishe. Ingawa Kikwete si chaguo la Mungu kwa maana ya kuwa rais wa nchi. Anaweza kuwa chaguo la Mungu kwa maana ya kupigilia msumari wa mwisho kwenye jeneza la CCM. Mungu ana njia zake za kutenda. Hakika Kikwete ni chaguo la Mungu ingawa si kwa kujenga bali kukibomoa chama chake.

Source: Tanzania Daima Julai 23, 2008.

No comments: