The Chant of Savant

Thursday 31 July 2008

Ndoto ya malkia walafu wawili

BAADA ya kuongea kwenye simu na Mgosi Machungi, ambaye Kijiwe kilimtuma kwenda sehemu sehemu kusikiliza vikao vya wenzetu, naamua kujilaza kidogo kwenye kitanda changu cha kamba.

Namalizia ugolo wangu na kujipumzisha lau nipate hili na lile niwafunulie baada ya kufunuliwa.

Mara naanza kuota ndoto ya malkia habidhi na walafu wawili wa nchi ya kusadikika ya Tanzia.

Ni nchi inayostawi kwa nje kuliko taifa lolote lakini iliyofisidika na iliyofilisika kulihali. Hakuna mfanowe duniani! Wazungu hupenda kuiita No Man’s Land au NML.

Mmoja anaitwa Neema, mke wa mfalme Shweshwe. Lakini ana matendo na machukizo kiasi cha jina lake kubeba ujumbe hasi na kinyume na maana yake. Huyu kwa tamaa ni balaa badala ya neema. Waweza kumuita Malkia Balaa binti Sheshe huko tuendako.

Ana uchu wa mali sina mfano. Ingawa yu mke wa mfalme, ni msasi wa ngawira tena toka kwenye maweko ya umma na wasasi wa ngawira wachafu wakwepa kodi na wezi!

Naona mama mwingine naye malkia. Anaitwa Anatamaa mke wa mfalme Makapikapi. Kichwani hana taji.

Ni malkia wa zamani aliyesifika kwa uroho, roho mbaya na sura mbaya. Anaonekana umri unaanza kumuacha huku na aibu ya matokeo ya jinai zake vikianza kuchukua nafasi yake kwenye mwili wake usio na shukrani.

Nawaona wajoli wakimzodoa na kumzomea yeye, mumewe na wanawe na marafiki zao walioshirikiana nao kuliua taifa la Tanzia.

Hata huyu wa pili mwenye taji kichwani si mzuri wa kuitwa mzuri. Kwani ana umbo lililopigwa pasi na macho makubwa kidogo na weupe wa mkorogo. Mambo yake na matendo yake ni mkorogo mtupu. Kama mumewe, amejaliwa kujikomba na kughilibu wajoli waliomzunguka.

Wajoli wanajifanya kumpenda kumbe taji! Naye kwa ujuha anashabikia akizidi kuhanikiza apendwa! Hilo! Laachwa ladhani langojewa! Linaanguka ladai limesimama! Ngoja muda uishe na taji limponyoke aenda aliko malkia Anatamaa.

Kwa uzuri hata mumewe ni bomba kuliko yeye. Lakini haya tuyaache.

Malkia wa pili asiye na taji ana sura ya ukatili na ni mweusi tii, asiyepambwa akapambika. Anaonekana kama mjoli kiasi cha kuzidiwa na wasaidizi wake. Kama humjui akitokea utamwamkia mtumishi wake ukidhani ndiye malkia na malkia akiishia kuwa mtumishi wa mtumishi.

Tazama naona malkia hawa wanaoonekana safi kwa nje huku ndani ni mbweha na uoza mtupu. Kama makaburi yapambwayo kwa minara na misalaba, wameoza kwa ndani sina mfano!

Neema ambaye ni balaa tofauti na jina lake.

Anae asiye na kitu bali ulafu.

Japo hawa malkia ni tofauti kwa nyakati na enzi zao na sura zao, wana kitu kimoja au viwili vinavyowaunganisha-uroho na kupenda vya mteremko.

Ingawa wamefikia umalkia kupitia migongoni mwa wafalme wapumbavu waliowaachia wawachafue kwa tamaa na roho mbaya zao, bado wao wanajiona ndio watawala.

Wanajiona wajanja wasijue huko mbele waweza kuishia korokoroni baada ya kuuhujumu umma. Wangekuwa ni malkia wa utawala wa zamani wa Kirumi, kwa uchafu na mbaya yao wangeishiwa kunyongwa. Lakini kwa vile wana bahati kuzaliwa na kutawala kwenye nchi ya kufikirika ya Tanzia, wanapeta na kutesa kiroho mbaya.

Sifa nyingine inayowaunganishi malkia hawa wezi na wapumbavu ni kujikomba na kujipendekeza. Pia ni mabingwa wa unafiki. Maana ukiwaona wakienda kwenye misiba na kujulia hali wagonjwa maskini utadhani wanawapenda kweli.

Pia hupenda kusafiri safiri na mfalme hasa kwenye nchi za mbali. Kila alipo wapo. Huyu wa pili ambaye ni wa kwanza hana bao siku hizi baada ya taji kumhama. Amehamwa hata na wafanyabiashara wezi ukiachia mbali kuzongwa na nzi na harufu mbaya vitokanavyo na roho na matendo yake.

Kitu kingine kinachowafananisha ni ile hali ya kuanzisha vigwena viitwavyo ngwe wavitumiavyo kuuibia umma wa watawaliwa wa falme hii ya Tanzia.

Kwa vigwena vyao wamejitengenezea utawala ndani ya utawala.

Ni utawala wa kuwala watawaliwa waliwao kama nyanya na maparachichi! Wao marafiki zao mashoga zao na watoto wao nao wana utawala wao ndani ya utawala msonge uliochoka na kuchafuka na kunuka ufisadi hakuna mfano.

Tazama naona Malki Anatamaa akisukwa sukwa baada ya kugundulika kuwa ana kigwena cha kutoza ushuru na kuchezesha upatu.

Inasemekana anawakamua wajoli si kawaida. Akikupa kibaba kimoja cha mtama alioupora kwenye ghala la wajoli chini ya ufalme wa mumewe, unamlipa vibaba zaidi ya sitini! Ni mama mroho hata fisi ana nafuu.

Baya zaidi shutuma hii imetolewa na mzee wa makuhani kwenye mkutano wa makuhani! Sawa na mfalme Makapikapi mumewe, naye aliwahi kushutumiwa na mzee wa makuhani aliyetaka kura za vijiti zipigwe afungwe hata kunyongwa kutokana na kuwaibia wajoli alipokuwa mfalme.

Na kama si mfalme kibaka Shweshwe, Makapikapi angekuwa lupango akinonihino kwenye debe.

Yeye na Malkia Anatamaa wanaishi kama mijibwa iliyoiba siagi wasijue mwisho na majaliwa yao vitakuwaje!

Tazama naona tufani kali ikilikumba taifa linaloangamia la Tanzia. Naona mawingu meusi mazito yakijikusanya juu ya taifa hili. Hasira za Mungu zinabainika kutokana na uchafu unaofanywa na wafalme wa Tanzia.

Ajabu wingu hili licha ya kutanda juu ya nchi nzima, upepo unalielekeza kwenye kisiwa kiitwacho Walionacho, ambacho ni makazi ya watawala na wenye nacho wakila kila waonacho mbele zao bila kijicho.

Naona mijitu yenye sura za watu lakini nyamaume ikijichana huku wajoli wakizidi kuteketea kwa ulofa!

Badala ya wajoli wa Tanzia kuogopa na kuomba wingu lipite, wanashangilia, kwani mvua itakayotokana na wingu hili ni neema kwao.

Watapata maji ya kunywa, kufulia na kulisha mazao, baada ya kipindi kirefu cha ukame ulioathiri sana hasa vichwa vya watawala wao.

Naona tufani kali ikialika kusi, kaskazi, mashariki na magharibi. Ajabu linatokea! Naona kondoo waliogeuka ghafla kuwa mbuzi wakizipiga na mbwa waliolala kwenye majani yao!

Kumbe mbuzi na kondoo wakitambua wakatumia vizuri pembe zao na kwato wanaweza kuwashinda mbwa na mbweha na mbwa mwitu!

Kweli, umoja ni nguvu na kujitambua ni hatua muhimu ya kujikomboa!

Onyo, kunga hili ni kwa wenye taamuli. Maamuma na mbumbumbu yaweza kuwa kero maudhi na matusi.
Source: Tanzania Daima Julai 30, 2008.

No comments: