The Chant of Savant

Tuesday 12 August 2008

Kuna uwezekano tukamkumbuka Mkapa ingawa…..

Ingawa inasikitisha, tuendako watanzania wanaweza kumkumbuka rais mstaafu Benjamin Mkapa licha ya kushutumiwa kujineemesha kupitia mamlaka huku akiiuza nchi kwa wawekezaji. Analaumiwa yeye mkewe familia na marafiki.

Hawatamkumbuka kwa vile alikuwa mwema na mwenye kufaa. Watalinganisha masahibu yao ya sasa na yale ya wakati wa Mkapa halafu wapate hitimisho hata kama ni la aibu na kuchukiza.

Mkapa, angalau kwa miaka mitano ya mwanzo alionyesha organizaisheni na umakini. Katika kipindi hiki yeye na watu wake hawakuwa wameishaanza kujichotea na kugawiana mali ya umma ili kujinufaisha.

Je utawala wa sasa wenye miaka mitatu umeishafanya nini katika hili? Una zigo la kashfa-EPA, Richmond, TICTS, Twin towers, Meremeta, Deep Green Finance,TANESCO (uliyorithi kwa Mkapa) na nyingine nyingi. Imani ya wananchi imeshuka kuliko wakati wowote. Rejea ripoti ya RIDET yenye kulalia upande wa serikali.

Hata ukiangalia namba ya walaji na ulaji utakuta kuwa Mkapa angalau hakuwa na walaji wengi kama sasa. Hakuwa na mtandao ukiachia ile ya mkewe kupitia NGO yake ya ulaji na shughuli nyingine za kutia mashaka.

Je serikali ya sasa kwa hili ikoje. Kuna mitandao karibu katika kila kitu. Ipo mitandao ya kichama na ya kitaaluma hasa waandishi wa habari. Wapo waandishi wakereketwa wa nchi na wale wa kulamba matapishi ya watawala wakiwasifia kwa kila upuuzi. Hawa ni wengi. Hata vyombo vyao vya habari vinajulikana. Vingine vimepatikana kwa pesa za EPA na Richmond.

Leo utasikia majina kama Rostam, Lowassa, Karamagi na mengine mengi hasa baada ya wahusika kuhusishwa na Richmond na wakabaki na ushawishi mkubwa chamani na serikalini. Hapa ndipo tofauti kati ya Mkapa na Kikwete inapozaliwa.
Ingawa hakukuza uchumi, Mkapa alisifika kubana mzunguko wa pesa kiasi cha kuipa thamani na kuleta nidhamu katika baadhi ya mambo kama vile ukusanyaji kodi ingawa kodi ilitumika vibaya. Hata matumizi mabaya ya serikali, awamu ya sasa inaongoza. Rejea kugundulika kwa matumizi hewa zaidi ya shilingi trilioni moja kwenye wizara.

Mkapa alibinya mzunguko wa shilingi kiasi cha kuipa nguvu.
Hakuiba pesa nyingi sawa na zilizoibiwa chini ya utawala wa Kikwete.

Mkapa hakurithi watendaji toka kwa mtangulizi wake Ali Hassan Mwinyi ambaye alimkandia sana. Kikwete alirithi karibu kila kitu toka kwa Mkapa. Rejea baraza lake la mawaziri kuundwa karibu na wale wote waliokuwamo kwenye utawala wa Mkapa. Bado hujaongelea NGO za wake wa wakubwa.


Mkapa aliingia kwa mgongo wa Nyerere wakati Kikwete kwa ule wa Takrima. Haya ni madai ambayo hayajapingwa na utawala wa Kikwete na Kikwete mwenyewe!

Kuna mambo ambapo Mkapa na Kikwete wanafanana. Mkapa hakupambana na rushwa zaidi ya kupoteza pesa ya watanzania kwa kuunda tume ya Warioba. Kikwete kwa upande wake hataki hata kuongelea rushwa ukiachia mbali kutoa matumaini na kutafuta sababu za kusingizia kama ambavyo juzi alilaumu kuongezeka bei za mafuta kuwa chanzo cha masahibu ya watanzania. Jambo hili si kweli. Maana watanzania walianza kuumia hata kabla ya mafuta kupanda bei.

Wataalamu wa uchumi wanasema ufisadi hasa wa EPA na Richomond ndivyo vyanzo hasa vya masahibu haya.

Kitu kingine kinachofananisha Mkapa na Kikwete ni ile hali ya kujizungushia marafiki na wana familia katika kuendesha nchi. Rejea kuundwa kwa NGOs tata za WAMA na EOTL. Katika hili Kikwete amempiku Mkapa kwa kuruhusu mwanae na mkewe kujiingiza kwenye siasa za chama cha mapinduzi hasa walipogombea na kutumia jina lake na kupita.

Je sasa ni kwanini watanzania wanaweza kumkumbuka Mkapa wakimuona kuwa bora kuliko Kikwete?

Kwanza Mkapa alikuwa akijibu tuhuma zilizokuwa zikiukabili utawala wake kitu ambacho Kikwete anakiogopa na kukikwepa kuliko kitu chochote. Makapa alipobanwa na vyombo vya habari kuhusiana na rushwa, alijibu alipokuwa Singida. Ingawa majibu yake hayakuwa majibu kitu zaidi ya kuwataka wenye vyombo vya habari nao kueleza walipokuwa wamepata mitaji ya kuvianzisha, angalau majibu yake ya hovyo yalionyesha msimamo wake.

Wakati wa utawala wa Mkapa ingawa aliwaridhisha wawekezaji na mataifa ya nje, angalau alikuwa na la kuonyesha. Kwa sasa Kikwete hana chochote cha kuweza kuonyesha zaidi ya rundo la kashfa alizozikalia bila kujulikana atazishughulikia lini.

Mkapa alipoingia hakutoa ahadi zozote zaidi ya Marehemu baba wa taifa kuwaaminisha kwa maneno tu kuwa Mkapa alikuwa Mr. Clean na angewatumikia vyema. Ingawa haikuwa hivyo, alikuwa hadaiwi sana kama Kikwete aliyeahidi pepo chini ya kile alichokiita kuwapeleka watanzania Kanani kwenye nchi ya maziwa na asali toka Misri (kwa Mkapa) jambo ambalo hajatekeleza zaidi ya kuwapeleka Misri zaidi ya alipowakuta.

Tukija kwenye uchumi, Mkapa anaweza kuonekana bora kuliko Kikwete. Ingawa aliuza mashirika ya umma kwa bei ya kutupwa ili kukidhi matakwa ya wanunuzi waliomkatia chake, ingawa alikuwa na ushawishi wa kuweza kupata misaada hata kama siyo mingi.

Kwa sasa kila uchao, Kikwete anapata mashinikizo toka kwa nchi fadhili kuwa kama hatashughulikia ufisadi watakata misaada yao. Rejea onyo kama hili la hivi karibuni lililotolewa na nchi kumi na nne fadhili zikiongozwa na Denmark.

Mkapa alisifika kwa kujenga na kubomoa hoja. Kikwete kwa bahati mbaya si kwake binafsi wala wasaidizi wake, hakuna mwenye kichwa kinachochemka kuweza kufanya hivyo. Kama kuna analolimilki si jingine bali kutoa ahadi hewa kila uchao na kuchukulia mambo nyeti kirahisi rahisi. Rejea anavyocheza cheza na ufisadi.

Mkapa ingawa alizidisha matatizo ya Muungono kwa kuwachia Salmin Amour na Amani Karume wafanye watakavyo, hakupambana na upinzani mkali juu ya Muungano kama ilivyo kwa sasa kwa Kikwete ambaye hali inavyoonekana, naye ataliahirisha tatizo la Muungano kama alivyofanya Mkapa.

Tuhitimishe. Ukiwaweka kwenye mizani watawala wetu wawili, ingawa wote hawana manufaa kwa taifa, angalau Mkapa anaanza kuonekana bora kuliko Kikwete. Hii ni baada ya kuangalia muda wa miaka kumi ya Mkapa na mitatu ya Kikwete. Utakuta kuwa Kikwete amechafuka mapema tofauti na Mkapa ambaye angalau kwa miaka yake mitano ya mwanzo hakuwa na kashfa lukuki na kubwa kama hizi za utawala wa Kikwete. Hata katika uteuzi wa watendaji, Mkapa alikuwa makini zaidi ya Kikwete ukiachia kupotoka kwa kumteua waziri mkuu Fredrick Sumaye aliyegeuka mzigo kwake lakini akamaliza ngwe yake tofauti na Edward Lowassa aliyeteuliwa na Kikwete akaishia kumuachia aibu asiyoweza kuifuta hata kwa miaka milioni moja.
Hakika, kwa aibu na hasira tutakuja kumkumbuka Mkapa ingawa hafai na hajajibu tuhuma zinazomkabili za kujipatia utajiri akiwa madarakani kinyume cha sheria. Hapa hatujawadurusu watawala wetu kichama. Je Kikwete atatufikisha wapi? Ni suala la wakati. Je kuna haja ya kungoja hadi tufikishwe huko.

Hili ni changamoto kwa watanzania wote wakubwa kwa wadogo wanaogumiwa maisha kila uchao.

Wito maalumu, namtaka Kikwete akomeshe mauaji ya mazeruzeru haraka kwa kupiga marufuku shughuli haramu za uganga zilizoshamiri hapa nchini.
Chanzo: Dira ya Tanzania Agosti 12, 2008.

1 comment:

Anonymous said...

Peleka makala haya katika gazeti la Mwanachi watanzania waelewe,Manake wapo wajinga wengi sana hawaelewi kwanini tuna hali mbaya kimaisha.Wakidhani ni umaskini wao tu.