The Chant of Savant

Wednesday 6 August 2008

Ndoto ya majuha wawili

TAZAMA niko nimejilaza. Mama Ndiza amelala ngomani. Hivyo niko na baridi yangu nikiwaza hili na lile. Ila pamoja na yote nitalala.

Kwanza naota. Eti niko kwenye jumba la kifalme huku Mama Ndiza akiwa na bonge la NGO ya ulaji; nisijue niko kwenye ubavu wangu wa mbwa, tena wa mama mzaramizi! Siwezi kujilisha pepo kama majuha.

Namuona mama aliyenawiri akidaka mipesa kama hana akili nzuri. Yeye hajali wampao hata wawe vyangu na vibaka, yeye anasunda tu! Hayo tuyaache niliyatongoa wiki iliyopita kiasi cha kuwaudhi bibi Anna Tamaa Makapi na Zahma Kishweshwe.

Tazama. Naona ombaomba wawili majnuni. Mmoja mkubwa na mwingine mdogo akiwa ameshikilia magongo aliyochongewa na huyu wa kwanza. Wanataka kutoana macho wakigombea umaskini badala ya utajiri! Wanabishania ujinga eti urafiki wao unawaletea umaskini wakati unaletwa na ujuha wao!

Mmoja anaitwa A-mini Karum Keng na mwingine Njaa-kaya Kikwekwe. Hawa ombaomba wavivu waliachiwa urithi na wazazi wao mzee Zenj Bai na Tang Nying-ka. Ebo! Wana majina utadhani Wachina na si Wamakonde!

Majuha wetu hawa waliachiwa ardhi tele hasa kwa huyu mkubwa mpenda sifa. Huyu wa pili, yaani mdogo mwenye magongo, yeye kaachiwa kipande cha kiamba. Hana ardhi wala mali. Humtegemea huyu mkubwa ambaye naye ni juha kiasi cha kushindwa kutumia akili na mali lukuki aliyoachiwa na marehemu wazazi wake.

Wao bila aibu wameshikilia kuombaomba huku wakijisifu kuwa familia zao zimetulia kwa sababu watoto na wake zao nao majuha hawalalamiki kwa ugumu wa maisha utokanao na kutotumia akili kwake.

Watalalamikaje iwapo kila mtu anaiba atakacho wakati atakao? Watalalamikaje iwapo wake zao wanajifanyia kila ufuska, wao wasijali? Nao wako kwenye ufuska wao. Kila mtu fuska na ufuska wake awe mkubwa au mdogo.

Na ufuska huu umefanya watu washindwe kudai haki zao na wengine kutotimiza majukumu yao. Mbona kwa majirani moto unawaka kutokana na makosa hata madogo kuliko hii zahama wanayofanya majinuni hawa ngulumbili?

Majuha hawa wawili ambao baba zao walikuwa maarufu na marafiki si chochote bali kero kwa familia zao. Kutokana na huyu mkubwa kuachiwa urithi mwingi lakini akawa hamnazo, amekuwa akimtumia hamnazo mwenzake kama kikaragosi chake kufanya upuuzi wao. Humpangia alale saa ngapi, ale nini na avae nini.

Maana kila saa wako wote kwenye upuuzi wao wauitao maisha! Watoto wa huyu gendaeka wa pili wengi wanaishi kwa huyu juha mwenzie mtepetevu.

Pamoja na wote kujaliwa kuwa marafiki wakiufaidi utajiri wa juha mkubwa ambaye naye anaanza kuishiwa, wamefuja kila kitu kiasi cha kuanza kusababisha ugomvi pande mbili.

Watoto wa juha mkubwa wanalalamika. Haki zao zimezidi kuibiwa na kupewa watoto wa juha mwenye magongo. Kisa? Eti juha mkubwa kwa kutoa masharti kwa juha mdogo ameridhika aendelee kukondesha wanawe ili kulinda ushufaa uchwara huu.

Watoto wake wanashangaa. Mbona wengi wana elimu hata mali kuliko huyu juha mdogo ambaye kimsingi utajiri alio nao ni wa mawazo?

Wapo wanaodai: kama baba yao ataendelea na ujuha wake basi urafiki uvunjike. Maana huyu juha mdogo kalianzisha. Eti baadhi ya watoto wake vizabizabina wanasema naye ni mwanamume.

Hivyo hapaswi kupangiwa maisha na juha mkubwa wasijue alikomtoa zama zile! Kwao wanadhani mwanamume ni kuota ndevu na kuvaa suruali, wasijue mengine mengi!

Ila wamesahu kitu kimoja. Juha mkubwa akicharuka akawatimua watoto wa juha mdogo, kijumba chao cha fito hakitawatosha. Isitoshe baadhi ya watoto hawajui kuwa bila ya juha mkubwa kuendelea kumtawala juha mdogo angeishapigwa na watoto zake zamani.

Maana wale watoto aliozaa na mama wa Kimanga halafu akawatosa wana hasira naye. Kama si huyu juha mkubwa kutumia misuli yao juu ya baba yao, mbona alishalizwa zamani gani! Wamesahau walivyo vizalia vya watwana waliotawaliwa na mmanga zama za zama!

Kinachokera ni ile hali ya majuha wawili kila mmoja kujifanya mjanja wakati wote majuha. Juzi juzi juha mdogo kapata ushawishi wa baadhi ya watoto wake eti anataka adai uhuru kutoka kwa juha mkubwa, asijue uhuru gharama!

Majuha huwa hayakosi vituko. Yanatapanya mali yaliyorithi halafu yanaenda kuombaomba kwa majirani. Nasikia juha mkubwa yupo kwenye majadiliano kufanya urafiki na jamaa wengine wajanja ilhali huu wa majuha, tena juha mdogo umemshinda! Kweli ujuha ni mbaya kuliko hata ndwele, maana ndwele yaweza pata mganguzi.

Mwambie anapotea. Utatukanwa na kupewa majina utadhani nawe juha kama wao! Kinachokera cha majuha hawa ni ile tabia ya kuombaomba wakapewa halafu wakawaibia watoto wao.

Majuha hawa ni wapenda matanuzi. Kuadhimisha siku za kuzaliwa kwao ni sikukuu na mapumziko, huku maelfu ya pesa yakitumika kwenye upuuzi huu. Wamejizungushia wapambe na kupeana utawala ndani ya utawala wasijue wao ni omba omba vichaa na majuha.

Jamani hata juha alindwe na walinzi wenye ‘mapurendi’, bado juha ni juha. Tena juha huyu huwa juha zaidi kwa vile hupofuka asione mambo kama yalivyo, bali aambiwavyo kama walivyo wetu majuha wakuu. Kutwa kucha wako ngomani wakitembea hata miji ya mbali kubomu na kutangaza ujuha wao!

Juzi juha mdogo kagundua akiba ya madini kwenye kipande cha ardhi alichoachiwa na wazazi wake. Wacha aanze kumgeuka yule juha mkubwa akisema kuanzia sasa kila mtu asimjue mwenzake.

Anadhani kapata utajiri asijue kuwa na akiba ya madini si dili, bali kutia akili!

Mbona juha mkubwa ana vitu kama hivyo kwenye mashamba ya marehemu baba yake lakini havimsadii zaidi ya kuachia wenye akili wajifaidie yeye akiendelea kufaidiwa na aibu ya kubomu?

Majuha kweli yana mambo. Yaani juha mdogo hajui kuwa juha mkubwa akiamua kuvunja uswahiba huu wa majuha, muathirika wa kwanza atakuwa yeye. Kiardhi chake kidogo hata hakitoshi kuzalisha chakula cha kulisha utitiri wa watoto aliowazaa kama panya.

Kitu kingine, yeye hana mabaunsa wa kumlinda likizuka vagi. Maskini kasahau kuwa hata alipotaka kurithi ukuu wa ukoo wake ni juha mkubwa aliyemuokoa kwa kutuma mabaunsa wake kusimamia wizi uliofanywa kupatikana mkuu wa ukoo!

Juha mkubwa anajisifia kitu kimoja. Watoto wake wengi wamekula unga na kuvuta mibangi kiasi cha kugeuka makondoo. Wenye akili lau kiduchu kawamaliza kwa kuwakatia chumo la wizi kwenye fuko la familia. Juzi kulikuwa na wizi wa EPA yaani ‘Ewe Pakua Achana-nami.’

Mitoto yake mijambazi mbona imejizolea pesa ile ya kuomba na kuishia kuwa na utajiri lukuki!

Wengi wanaojua utajiri wa juha mkubwa wanashangaa ni kwanini anang’ang’ania usuhuba na juha, tena maskini, wakati anao uwezo wa kulisha familia yake bila kumtegemea mtu!

Na wale wanaojua uchovu wa juha mdogo wanashangaa anakopata jeuri kudai anavyodai. Au ni hivi viakiba kidogo vya madini vilivyogunduliwa kwenye kiamba chake?

Ama kweli juha kweli juha.

Ananikumbusha kipindi fulani. Watoto wa juha mdogo walikuwa wakipita mitaani wakijidai kuwa kuna siku watakuwa wakwasi kutokana na wajomba zao wa kimanga kuwatupia mabaki!

Watu wazima mnategemea vya wajomba au ni yale ya mtoto wa nyoka ni nyoka? Mbona mababu zenu hawakuwa omba omba? Au ni yale ya simba kumzaa mbwa? Majuha yatamalizana vipi, nani anajua japo waweza bunia? Akili kichwani. Waambiwa walo juu, walo chini wataambua wenyewe.


Source: Tanzania Daima Agosti 6, 2008.

No comments: