The Chant of Savant

Wednesday 3 September 2008

Kijiwe chapanga kum-impeach Mpayukaji

BAADA ya kupokea ripoti ya tume ya WEPA na kuikalia huku mzee mzima nikitembeza sanaa, wana kijiwe wakiongozwa na Mgosi Machungi, Kapende na Makengeza wamekuja na mkakati wa kisiri siri kutaka eti kuni-impeach kama wabunge walivyotaka kumfanyia yule kibaka wa Pakistan!

Hawa watu hawana adabu hata kidogo. Hawajui kuwa wanakijiwe ni wavivu wa kufikiri si kama wale wa Pakistan! Haimpichiwi mtu hapa.

Nitawaimpichi mimi kwa kuwapa takrima na kuwagawana ili waanze kulana kama wanakaya wanavyomalizana kupitia ujambazi, udokozi, rushwa na roho mbaya.

Hivi vyombo vya habari vitakuja kuipasua dunia hasa ile ya ufisadi. Nani angeamini wanywa kahawa wangejua mambo ya Pakistan kiasi cha kutaka kuni-msharafu? Huenda hii ndiyo sababu iliyomfanya rafiki yangu Tunituni kuvibana ili mambo yake yasifichuke.

Lakini hata hivyo ni upumbavu. Alivibana enzi za ujambazi wake. Sasa vinamvua nguo kila uchao kiasi cha kumgeuza juha lisiloweza kujitetea zaidi ya kutegemea hisani ya Chekacheka mlinzi wa mafisadi.

Baada ya kuzinyaka kusema ukweli silali. Hata mama Ndiza wangu ameoneysha kustuka. Ule mradi wake wa kashata tokana na pesa nilizoiba kwa wana kijiwe unaweza kuwa hatarini.

Mwanzoni nilidhani wanakijiwe ni mafala nami ningeendelea kutanua na kuwaibia huku wao wakipiga kelele. Niliwahi kuwambia kuwa kelele za mlango hazimzuii mpangaji kulala.

Sasa naona kelele za mlango zinaanza kunitikisa. Hawa wadudu wanaweza kuvunja mlango nikaabika mzee mzima.

Kwanza nijipongeze. Jinsi nilivyowazima wapika kahawa na kashata waliokuwa wanatishia kuandamana, kweli usanii nauweza. Nisingemuhonga bosi wao Nesta Ngulli, mbona wangenitoa haja ndogo!

Sasa hakuna cha mgomo wala maandamano. Kusema ukweli hawa wanuka jasho ni wavivu wa kufikiri. Eti jitu linawafunga kamba kuwa ngonjera yangu iitwayo hotuba ililikuna hivyo linatoa fursa!

Maskini wanuka jasho hawakujua kuwa kilichomfanya bosi wao awatwishe mkenge si utamu wa hotuba bali maulaji ya sirini tena nyuma ya pazia! Shauri yenu nyinyi endelea na matumaini yasiyokuwapo mtastuka kumekucha.

Kama si huyu mbwa mwitu na tamaa zake za fisi haya yote yasingenifika! Dude lina tama! Juzi walilitimua ulaji kutokana na kashfa ya kununua maji machafu. Sasa limeibuka na kashfa nyingine ya kuiba pesa ya chakula cha watoto!

Halafu huyu kijana Mape au Mapepe kalishika pabaya ingawa anatiliwa mizengwe. Sijui nimfukuze kwenye kijiwe? Ila nikifanya kosa hili vijiwe vingine vitamchukua na kumtumia dhidi yangu. Na alivyo na mapepe kama jina lake anaweza kuzamisha mtumbwi bure.

Mwaka huu kila mtu anakufa kivyake vyake. Hata kama nimetoa msamaha wa kiushikaji kwa akina mbwa mwitu kurejesha pesa ya kahawa waliyoiba wakisingizia ukame wakaleta maji machafu tena kutoka mto wa ng’ombe halafu wakakwanyua pesa ya kijwe eti waliyanunua.

Ila mbwa mwitu anajua siri zangu nyingi. Hivyo nikimtosa kijinga anaweza kuniumbua. Sasa nitampa ujumbe au uwaziri wa mambo ya nchi za nje ili akamalizie tamaa yake huko nje. Lakini je, wana kijiwe watakubali upuuzi huu?

Kutokana na kuzidi kuamka kwa walevi wa kahawa, kuna uwezekano mambo yakawa si mambo. Kwanza licha ya kustukia ujambazi wa akina Mbwa Mwitu, wamestukia pia ushiriki wangu kwenye wizi huu. Ingawa pesa ya kahawa iliyoibiwa niliitumia kuwahonga wana kijiwe kunichagua kiongozi wao, naona mambo yanazidi kuwa mabaya.

Mijitu hii mishenzi sina mfano. Hata ulaji wa mke wangu wanaanza kuuingilia! Hivi walitarajia nini kwa kuchagua mtu kama mimi mvivu na mjivuni? Nakumbuka mzee Busara aliwaonya.

Hawakumsikia. Waliendekeza ujuaji wa kijuha na njaa zao wakapwakia takrima yangu. Sasa wanalia lia utadhani vitoto vichanga! Wapumbavu humchagua mpumbavu kuwaongoza wasijue atawaongoza kuelekea kuzimu.

Mimi nasema wazi. Sipo kwa ajili ya mtu wala mnyama yoyote bali ulaji wangu na watu wangu. Finish. Period. Acha niongee kizungu huenda wanaweza kunielewa badala ya kulewa na sanaa na ngonjera zangu.

Mmeula wa chuya mwaka huu na mkome kuendekeza kiu yenu ya kahawa na njaa za kashata. Kwa upofu wao hawakujua kuwa walikuwa wananiuzia kijiwe ili nami nikibinafsishe kwa bei mbaya kama ninavyopanga kufanya hivi karibuni akipatikana Mwarabu wa kuninunua.

Mwenye ng’ombe mpumbavu aliamwamini mchungaji mpumbavu alipomuuza ng’ombe wake akaanza kujipekua mifukoni kuona kama yumo. Hawa nao wasipoamka watalia kama mwenye ng’ombe.

Tuache utani, majuha wanaweza kukengeuka nikajikuta pabaya hasa hili la kuni-impeach. Je, nifanyeje ili yasinifike ya kunifika?

Lakini kwa vile wameanza kusalitiana na kuvujisha siri nitakula nao sahani moja. Kwanza nitaanza kuwapa ofa wale vidomo domo wote wanaotaka kunifanyia kitu hii mbaya. Nitawaganya kwa kuunda tume mpya ya kuchunguza mgawanyiko katika kijiwe.

Pia washirika wangu akina Mbwa Mwitu lazima watoe mchango wa kupiga kampeni za kunipamba na kunionyesha kama kiongozi mzalendo na shupavu hata kama mimi ni kibaka.

Hapa lazima na yule rafiki yangu mwandishi wa habari anayependa kunywa kahawa za dezo kwenye kijiwe chetu nimuongezee kashata nyingi ili azidi kujenga hoja ya kubomoa hoja za wabaya wangu.

Isitoshe, juzi mama Ndiza alitoa msaada wa maandazi kwa wake wa wanakijiwe waliofurahia msaada huu. Hivyo, hawa watanisaidia kuwalainisha waume zao wanaotaka kunitoa kwenye ulaji huu wa dezo.

Kwanza itabidi nijipe likizo ya mauzauza haya. Itabidi nielekee Nairobi na Kampala kujinoma na wanavijiwe wa huko, wakati wakereketwa wangu wakisahau. Nikirudi naanzisha zengwe jingine ili wasahau kabisa.

Kuhakikisha nawafunga kamba vilivyo, nitahakikisha naunda tume feki ya kuwachunguza akina Mbwa Mwitu. Na nitawateua washirika wetu na Mbwa Mwitu kuwa wajumbe wa tume hii mauzauza ili kuwapiga changa la usoni wana kijiwe wanaoshikia bango maulaji yangu.

Hawa wanywa kahawa hawanijui vizuri. Huoni nilivyowatwisha changa la machoni walipotaka eti nimsulubu mwenyekiti wa kijiwe wa zamani kwa kosa la kuiba mikaa ya kupikia kahawa inayotoka kule Kiwira, Mbeya.

Sasa nitawafunga kamba kwa kuwataka vidokozi wachache tuliowauzia vikombe vya kashata kwa bei ya kutupa wavirejeshe ili angalau nipumue.

Tukutane wiki ijayo kwenye mikakati na harakati za kuzidi kuwaibia wana kijiwe.

Salamu maalumu kwa Eddie Kuwasha. Hongera kwa kunusurika kashfa ya Richmonduli. Nasikia mzee mwenzangu ameamua kuwatoa sadaka akina Bangusili M7ha na Kadamage ili kukuokoa wewe baba lao katika ulaji huu.

Ya WEPA ya kwenu nasikia mchezo ni ule ule. Wanashughulikiwa dagaa nyungumi mnaendelea kupeta. Heri yenu kwa vile nyangumi mwenzenu ndiye yuko kwenye usukani.

Chanzo: Tanzania Daima Septemba 3, 2008.

No comments: