The Chant of Savant

Wednesday 24 December 2008

Walevi wamekula majani hadi kutia akili

JUZI nilikwenda Mahakama ya Kisutu kuona waishiwa wanavyohenya na kuhaha. Sikujua kuwa nao ni waoga. Wanaogopa hata kamera! Kwetu uswekeni ni dili. Ukimuona mpiga picha tena wa magazeti makubwa au runinga unakenua ili akupate vizuri, kesho yake ujinome kwenye kioo na meza za wauza magazeti. Ajabu mibaba mizima tena inayotushawishi tuiite waheshimiwa wakati ni waishiwa eti inaogopa kamera!

Uswazi hatuogopi kamera, EPA, IPTL, Richmond wala CIS. Sisi mashujaa. Tumegharimia mazimwi, kunguni na minyoo miaka nenda rudi. Sisi wajanja japo mafala wanaojiona wajanja yanatuona mafala.

Yupo fala afananaye na mdudu aitwaye Gonimbrasia belina au kiwavi. Alitwambia; hata tungekula majani tule, Mfalme ajinome angani kama mwewe. Mwe! Kaya hii ina mambo tena makubwa tu. Madogo yana wenyewe!

Hatukujivunga. Kama mbuzi, tena wachizi, tulifakamia majani hadi kutia akili kiasi cha kujikuta tukijinoma na waishiwa hata kama kujinoma kwenyewe ni Keko.

Hatuogopi Keko. Nini Keko? Tulishazoea kifungo kwa mama mzaramizi, ambapo licha ya kuombwa bia, mboga na zawadi, unatukanwa mtindo mmoja!

Keko unalala huku ukilindwa bila kulipia. Ukiamka kwenda kwa pilato unapewa basi na walinzi kwa sana huku kamera zikikungojea na wachora umbea.. Mungu akupe nini?

Watulishao majani, wajue wanatufanya tutie akili kweli kweli. Kwa akili hii tunataka Ewassa wa Richmonduli, Kagodam, Kadamage, Vijisenti Endelea Chenga mzee wa Jersey , Roast Tamu L’Aziz nao wamfuate Grey Mgonjwa lupango wakasherehekee Noel huko.

Bado hatuiishi hapa. Kwa akili za mbuzi na kula majani. Tunamtaka Tunituni na Bi Annae Tamaa, Annae Mugando Ballaa, Yosefu Manji, hata Joe Makamba wakanyee mitondoo.

Ohoo! Nilimsahau bingwa wa kughushi Sammy Ubwabwa Chitaahira wa Buchosha. Lazima tumsurubu. Hawezi kutugeuza mafala na sirikali, akafoji nyaraka na kulipwa njuluku zetu kwa kutubamizi mkenge.

Pia tunawataka walioshirikiana na majambizi wa AIPTIELO kutulangua nishati wakidhani tuna akili kama za mbuzi, waipate fresh.

Niwape stori. J’pili tatu ziliyopita, nilijinoma St. Josefu kushuhudia vitegemezi wa majambizi vinavyooana. Nilipewa kadi na rafiki yangu Shilingi Mbili wa Kuramba. Ehee! Nafika, bonge la butwaa! Nilimuangaza nisimdeku kumbe alikuwa Keko akitanua! Nilidhani chenga zake za Kisutu na kupewa usafiri wake vilikuwa vimemsaidia asinyee debe.

Ila mambo hayakuwa mabaya. Mshikajie na mume mwenzi Tunituni angekuwapo. Alishtuka. Aliogopa kamera na wambea wa vyombo vya habari wasimuulize siri ya mafanikio yake kutopelekwa lupango. Nasikia waheshimiwa wanataka avuliwe kinga ili tumpe disipilini.

Unajua wabongo siku hizi wana akili kama za mbuzi? Mbuzi huwezi kumficha hata kama kuna hatari utamsikia meee meee. Mtie kwenye gunia atalia mee mee. Mfanyie MaEPA na mahepe, au Mrichmonduli, bado atazoza tu. Heri kuishi kwa kula majani kuliko kulewa madaraka na kuishia kuadhirika mchana kweupe.

Ningekuwa yule fala ningewambia walevi wale mawe ili yawang’oe meno ili wakitaka kutamka maneno yasieleweke kuliko kuwalisha majani wakawa na ndimi mchongoko kama mbuzi. Hamkusikia hata Yesu hakupenda mbuzi? Aliitwa mwana kondoo na alikuja kuwatafuta kondoo waliopotea na siyo mbuzi.

Hivyo hata Mkuu asihangaike na mbuzi wawalishao majani wanadamu, tena kondoo wa Mchonga. Wawaache mbuzi watamalizana na Pilato na maaskari wa kirumi.

Achana na kina Yuda Iskarioti uokoe kondoo wa Bwana. Imeandikwa, atakayenisaliti ni yule akaaye meza moja nami. Kuwa nao meza moja siyo dili mkuu. Muhimu ni kuwaokoa kondoo wa Bwana utalipwa mbinguni na duniani. Wafunge Dellilla, Samson, na mke wa Loti. walioamua kujigeuza chumvi iliyovia. Wapiganie wana wa Mungu wasijegeuzwa mbuzi na mbuzi tena kiasi cha kuishia kulishwa majani.

Ee mkuu msifika na mpendeka, nakusihi warejeshee mbuzi uhayawani wao na kuwarejesha wana wa baba utu wao. Utawezaje hili? Peleka kila mbuzi lupango hata awe mkubwa na mzuri kiasi gani. Peleka mbuzi wote si bangusilo au mbuzi wa shughuli.

Juzi kuna mbuzi alijisifu: anakufahamu vizuri; u swahiba yake. Tangu lini ukawa uswahiba na mbuzi usiwe mbuzi? Mbuzi chake kisu na kamba mguuni. Haya ni mantiki ya kuwapeleka lupango siyo wawekwe bali wakatiwe ngwe na kufungwa kamba kwa sababu ni yao. Wembe uwe ule uliomnyoa Richmonduli akatimka na Chenga Chenga na Kadamage. Uwe ule ule uliowakomesha akina Ramba Ramba na Mgonjwa waliodhani ulaji ni urithi wao. Ule ule uliowanyoa akina Jitu na Migabacholi na vicheche.

Muhimu ujue. Kama mbuzi watatingishwa ili kutufanya tusahau, kwa akili ile ile ya mbuzi hatutaacha kudai na kudai, hata kuacha kula majani tukaanza kula nyama yao. Kama hii itakuwa tisha toto na changa la machoni amini mkuu, kondoo wategeuka chui simba na mbwa mwitu na kuwararueni.

Mkuu inabidi uelewe. Hata hufikia mahali kondoo akamuua ng’ombe hasa yanapomzidi. Hata kihongwe bingwa wa kubeba mizigo anapofikia kusema basi madhara yake huwa makubwa. Huibwaga mizigo na kumchapa mateke bwana wake. Mimba yaweza kudharauliwa kuwa ni kichanga kisicho na mabavu wala akili, lakini ikifika wakati wake wa kutoka, hutoka hata kama ni kwa kumuua mama au kumlazimisha kufanyiwa operesheni, lazima izaliwe.

Hali hii mkuu ni mimba. Heri tumalizane nayo kwa operesheni ya kuwarejesha mbuzi kwao lupango kuliko kuiacha ituue kwa kuwatetea mbuzi watu.

Ngoja jamani nisiwachoshe. Kwa vile ni juzi nimerejea kula chakula baada ya kulishwa majani na mbuzi-watu, natimkia kwa mama Ng’ani lau nikajipongeze kwa ubwabwa baada ya kuona mbuzi wanaingizwa mwao.

Mwisho kabisa, nawe mkuu usiwaigize wale mbuzi kutuamrisha tule majini. Maana majani mengine hasa yale makubwa huchetua akili na kufanya watu wawe machizi. Muhimu kama tutarudia kula majani basi halalisha vurugu hata utusweke lupango. Hatutavumilia kuona mbuzi wakindelea kula vinono kama watu.

Swali la leo. Je wanaojidhamini kwa mabilioni, siyo yale yatokanayo na matumizi mabaya ya madaraka? Ama kweli huku ni kumkaanga samaki kwa mafuta yake kiasi cha yote kuonekana kama usanii! Kwa nini tuwe na uchungu na bilioni 12 za matumizi mabaya tujisahaulishe bilioni 133 za EPA? Au ni changa la machoni. Tuambizane.

Chanzo: Tanzania Daima Desemba 24, 2008.

No comments: