The Chant of Savant

Wednesday 14 January 2009

Mipango ya Mpayukaji kuombea Kijiwe

BAADA ya maji kuzidi unga na sanaa kushtukiwa, mkuu amekuja na mpya. Eti anataka kuwe na siku maalumu ya kuombea kaya! Mwe! Dawa ya matatizo ya kaya si kuomba bali kuwajibika na kuwa waadilifu. Hamjui: hakuna laana kayani ila tamaa, ubinafsi, ufisadi, upofu, upogo, ujuha, ukondoo, ukuku, upanya, ukijiko n.k?

Hata shehe Yoyo Ubwabwa na utabiri mfu kawageuka. Asema mtameguka asijue mlimeguka zamani bado kufa tu. Mwasema yeye si Mungu. Mbona upuuzi wake mliupwakia kila mwaka? Hamkujua alikuwa akiwahadaa ili awaibie kama muwaibiavyo walevi? Eti si Mungu. Amekuwa Mungu wenu kwa miaka.

Hivi kukamata mafisadi kama Kagodamn na Richmonduli kunahitaji kushirikisha Godi! Tumekula kunywa na kulewa na kujisahau kiasi cha kumtia madole Godi! Ama kweli nao ni uvivu wa kufikiri aliosema na kutenda Tunituni na Anna Tamaa wake!

Hii mijitu nani kairoga kuacha kuuenga ukweli na kuenga mawenge? Mnadhani mzee mzima nitaingia mkenge wakati ni bingwa wa kuingiza watu mikenge? Mmenoa sana.

Kuna mnoko amenitonya kuwa baada ya kuona Rost Tamu L’Aziz kafanikiwa kupeleka chumo la wizi kanisani kwa mchunguji mbweha huko Kindononi, mkuu naye ameona atumie janja hiyo ili ionekana ufisadi ni laana ilhali ni matokeo ya michoro yake! Hivi walevi watakubali matusi haya huku wakijua fika: ni matokeo ya takrima ilivyokusanywa na nambari wahedi?

Japo mkuu na washikaji zake wamejiridhisha wataiepa EPA, tuendako watajaribu kila mbinu hawatafanikiwa. Za mwizi arobaini. Amefungua kesi uchwara za kina Rambaramba, Mgonjwa na Dan Jona akidhani tutaingia mkenge, hola. Kama hamjui jueni. Kinachofanyika ni kusogeza muda ili msahau mzidi kuliwa na zaidi.

Kuonyesha alivyo kanyabwoya amejiunga na wezi wa majoho kutaka kutuingiza tena mkenge! Jamaa hovyo. Alijisemea Mchonga.

Ili mjue kuombea kaya ni dili au la, angalia mipango yangu ya kukiombea kijiwe. Mkiridhika, swadakta salini hata mkeshe uchi muone hasira-sorry-- neema za Mungu zitakavyowashukia.

Kama mkuu, baada ya kuishiwa mbinu zote za kuwaweka sawa walevi, nimegundua mbinu mpya. Niliipata kwa rafiki zangu Zeki Ka-tortoise ambaye alikuwa jambazi ‘akaokoka’ na kuwa mtu wa dini. Kwa washikaji wake tunaomjua, tunajua hili ni gwanda tu la kazi. Anatumia dini kuficha madhambi na makucha yake. Bado anaiba sadaka kama kawa ukiachia mbali kuwa bingwa wa totoz.

Pia wapo kina wezi na vyangudoa wengine kama Gettie Rwakatahe, Silver Gamanyuwa, Chris Mwakasenge, Fau Mnihisi na mbweha wengine wawaibiao na kuwala kondoo wa Bwana.

Nitaarika wachungaji na mashehe na mashehena bila kusahau, nyumba zetu ndogo. Tutahanikiza kwa kelele tukitumia vipaza sauti vikali kuwachanganya. Tutaongea kwa ndimi.

Tutafadhiliwa na Jitu Kanji, Enderea Chenga, Rost Tamu L’Aziz, Eddie Ewassa na majambazi wengine wengi. Mgeni wa heshima atakuwa Njaa Kaya Kikwekwe.

Tutaomba wana kijiwe waendelee kuwa ndondocha ili kuwe na amani ambayo, kimsingi, si chochote si lolote bali shibe yetu, wake zetu na nyumba ndogo zetu.

Tutaomba maulaji yetu yaongezeke huku wana kijiwe wakiendelea kuwa kondoo wa Bwana waliwao na watumishi wa Bwana. Kwani mtume Paulo alisema; mchungaji hula vya zizini. Tunawapa vya rohoni. Je ni vibaya nanyi mkatupa vya mwilini? Msije nielewa vibaya, vya mwilini ni dhahabu, nyama za wanyama mbugani, mazao na fweza bila shaka.

Tutaoamba shibe yetu iongezeke huku wanakijiwe wakitubomu kahawa. Lazima mashikamano wa ulaji na uliwa yaendelee na kudumu milele.

Kijiwe kina amani. Unaiba kahawa hata kashata hakuna wa kukuletea za kuleta.

Ngoja nianze kufanya mazoezi ya sala takatifu itakayosaliwa siku hiyo.

Ewe Mungu uliyenichagua kuwa kiongozi wa kijiwe ukakiaminisha kuwa mimi ni chaguo lako, naomba usiangalie nitendayo bali nipangayo.

Nipo hapa mbele yako kuombea kijiwe chetu kiwe na amani, mshikamano na uvumilivu. Waepushe wana kijiwe na tamaa za kupenda ukuu na makuu. Wape imani ya amani wajue kuwa ulinichagua mimi pekee na hawa watumishi wako. Usizitazame dhambi zao bali neema na amani ya kijiwe.

Mungu uliye juu ya vyote, naomba uepushe laana iliyokumba kijiwe ambapo wanaitana mafisadi badala ya wapendwa. Naomba uzidi kuwafunulia wana kijiwe hekima yetu ya ajabu. Wajue kuwa pepo ni kwa walio maskini. Wajalie wauchukie utajiri. Maana utajiri unapoteza.

Imeandikwa. Heri walio maskini watauona ufalme wako. Nami ingawa naonekana mkuu ni maskini. Sijui kitu wala sina kitu. Ni mtupu kama kichanga.

Mungu zidisha neema kama mwaka uliopita. Tuuze kahawa nyingi nje hadi kuweza kununua mashangingi. Kijiwe kilikuwa na amani tele. Kama si mdudu wa kuitana mafisadi, kilikwenda vizuri. Mungu wape moyo wa subira watu wangu. Watii mamlaka. Kwani mamlaka zote hutoka kwako. Mimi ni chaguo lako ingawa walinipigia kura zao.

Usiwazindue kwenye usingizi wakanilaza mimi. Endelea kubariki ujumbe wako toka CCM au Chuo Cha Manabii uendelee kuwatuliza wana. Nipe kauli tamu ya kuwaliwaza na kuwaweka sawa ili amani iendelee kuwepo. Pia wasiangalie mezani kwangu na bi mkubwa.

Nakuomba uongeze idadi ya wawekezaji kwenye kahawa yetu inayosifika duniani. Pia uwape subira wana kijiwe wasiwabughudhi hata wanapokunywa kahawa na kula kashata kidogo. Uwape subira wangoje wakati wao huko tuendako.

Naomba uwajalie maisha bora wana kijiwe ambayo ni kukipenda kwa mioyo yao yote bila kujali kinawapa nini. Tuongezee mbinu za kuleta amani mshikamano na utulivu katika ulaji huu. Pia wape moyo wa kutupenda, kutuheshimu na kutusikiliza sisi viongozi wao bila kututilia shaka wala kutaka kutuchunguza.

Tunaomba uwape roho mtakatifu si mtakakitu. Watuamini tuwaongoze popote kama mchinjaji amuongozavyo kondoo kwenye machinjio. Wajalie wasiogope kuitwa kondoo. Kwani hata mwanao kipenzi aliitwa mwana kondoo.

Wote na tuseme HAMNA.

Hapa najua rafiki yangu shehena atapiga audhubillahi mina sheitwan rajiim.

Busara ya leo. Nani aliwahi kuona kupe aliyekonda hata kama yupo maungoni mwa mbuzi aliyekonda? Je ni kazi ya kupe kujali kuwa mbuzi hakondi wakati yake ni kunyonya damu? Fikirini.

Ha! Kumbe sijala!

Chanzo: Tanzania Daima Januari 14, 2009.

No comments: