The Chant of Savant

Thursday 5 February 2009

Chuo Kikuu kinapogeuzwa Choo Kikuu!



JUZI kuna jamaa aliniudhi sana . Eti anasema chuo kikuu sasa kimegeuzwa choo kikuu, na nzi wenye heshima na utukufu wanatua hapo!

Kwanza sikumuelewa alimaanisha nini? Je, hao nzi wanapata wapi heshima iwapo nzi ni nzi tu hata awe mnono?

Kwanini wenye chuo waliruhusu nzi kuingia kwenye chuo chao?

Je, hawa nzi na adha zao ndiyo wamesababisha wanafunzi hata walimu kugoma?

Maana binadamu hawawapendi nzi, wanaleta magonjwa, hasa Ukosefu wa Uadilifu Moyoni (UUM) ambao hutokana na ugonjwa uitwao ufisi na ufisadi.

Ugonjwa huu hufanya mtu aharishe sana ubongo kiasi cha kufanya mambo ambayo hata hayawani hawezi kufanya.

Kutokana na kuahirisha ubongo sana, muathirika wa ugonjwa wa UUM huwa mchoyo, mlafi na mbinafsi.

Hujiangalia mwenyewe bila kujali wengine. Kibaya zaidi ugonjwa huu unaua kumbukumbu kiasi kwamba mja huwa kama nyani. Haoni kundule.

Wakati najiuliza maswali baada ya kunusurika kupewa kibano na Fanya Fyoko Ubondwe (FFU), niligundua ni kwanini wanafunzi walikuwa wanagoma kusoma! Kumbe wamechoka na uchafu na uchafuzi wa nzi!

Hawataki kukumbwa na ugonjwa hatari wa UUM ambao wataalamu wanasema humfanya mtu kuwa kichaa na asiye na aibu.

Msomi na kiongozi gani atake ugonjwa unaomgeuza zezeta na juha kama wale walioruhusu hali kuwa mbaya hadi nzi kujaa chuoni kiasi cha kuwachukiza wanafunzi?

Kinachoshangaza ni kwanini wanafunzi hawaungwi mkono kupambana na kadhia hii? Kuna kajamaa kanaitwa Udasa ndiko pekee kalikowaunga mkono huku wazazi wao wakiishia kulalamika utadhani ni jibu!

Inaonekana ugonjwa huu umeharibu watu wengi. Ajabu ukiwaambia wanaumwa wanakuchukia ukiachia mbali kukanusha! Wapo wanaoshangaa kwa nini rais hachukui hatua za kusafisha chuo kikaondokana na nzi. Hawajui rais ana mambo mengi, wapambe na wakati mwingine masikio yake hayawezi kusikia kila kitu pale chuoni.

Wengine wanasema rais si rahisi kujiingiza. Kwani hana hata kitegemezi kimoja pale. Kitegemezi chake na wakubwa wengine husomea nje ya nchi kuepuka kukumbwa na ugonjwa wa UUM, ukiachia mbali adha ya nzi.

Ila ajabu kuna watu wamekumbwa na UUM sijui ni kwa sababu walisomea pale? Mbona wakati ule wa mzee Musa chuo hakikuwa na wachafuzi (nzi)!

Wapo wanaosema kuwa mtoto wa rais hawezi kusomea kwenye chuo kilichojaa nzi.

Kwa hadhi na nasaba yake hii ni kufuru. Yeye lazima asome na kutibiwa nje kama wazazi wake watukufu. Hata watoto wa mawaziri hawafai kusoma kwenye chuo kichafu kama choo namna hii ingawa wazazi wao walisoma pale tena bila kudhalilishwa na udahilishaji!

Kweli nchi hii imevamiwa na nzi na kunguru. Juzi nilikuwa pale kwa mama ntilie. Ni nzi wa jiji. Ukienda hospitali nako uchafu ni ule ule.

Nasikia hata pale Benki Kuu ndio waliofanya mpaka kukawepo na wizi wa EPA!

Mara nikiwa najiuliza nini la kufanya, alitokea Kapende akiongea peke yake. “Tazama sasa wanachukia mwanga na kupenda giza . Fisi hupenda kiza sawa na wao. Ufisadi umegeuza watu kuwa fisi, licha ya heshima walizonazo. Angalia wanavyochezea shilingi shimoni. Yaani mnakubali kugeuza chuo kuwa choo kiasi cha kushibisha nzi.

“Hee” nilijisemea. “Kapende nawe umeona nzi pale chuoni kama mimi?

Alijibu huku akitikisa kichwa. “Bwana eeh, nusura nipigwe mitama nilipokatiza pale. Sikujua kuna mgomo wa kupinga chuo kugeuzwa choo kikuu na nzi wanene!”

Tukiwa tunashangaa shangaa mara anatokea Kidevu aliyekuwa akitusikia tukishangaa upuuzi huu wa kutounga mkono mgomo.

Alisema. “Mara hii mmesahau nyakati za Mwalimu? Watu walisoma chuoni pale na kilikuwa safi bila mainzi kama sasa baada ya mafisi-ahadi kuvamia kila kitu na kila mahali.”

Aliendelea. “Tangu Nyerere aondoke nchi imeingiliwa. Mafisi na mafisadi yametamalaki. Sasa wameingia na nzi sijui tutakuwa wageni wa nani Yarabi?”

Aliendelea. “Hivi unadhani bila na wadudu fisidi na nzi kuingilia chuo kikuu kiasi cha kugeuka choo kikuu wanafunzi wangegoma?”

Nami nilimjibu. “We kweli muongo sina mfano. Mbona chanzo cha mgomo ni mikopo?”

“Naam!” Alijibu na kuendelea. “Hapo hapo. Hujui hiyo mikopo ni michafu na imejaa nzi ndani? Kuna mtaalamu ameiainisha aina ya nzi hawa. Kitaalaamu wanaitwa Mucandalas Maghembus nyongeae. Inasemekana walitoroka kwenye maabara moja iitwayo Kikwecus longolongolos kwenye nchi ya Tanzia.”

“Sijakuelewa bado,” alijibu. “Hujanielewa au umelewa kama wale nzi mafu pale chooni? Tangu lini watu wakasoma kwa mikopo? Mbona wao walipokuwa wakisoma hapakuwa na mikopo wala midebe bali maji ya bomba la Mchonga?”

“Unamaanisha bila kuwa na kopo la kwendea chooni pale shuleni husomi?”

Alijibu. “Swadakta.’ Kwa uchafu ule pale bila kopo nambie utaingiaje chooni? Bila kopo si utajipaka kinyesi kwa kiu ya kutafuta elimu?”

Kumbe jamaa alikuwa anaongea kama Yesu. Kumbe hoja yake ni kwamba wanaowatwisha wenzao mizigo wao hawakutwishwa mizigo walipokuwa wakiisaka nuru!

Sasa nimeelewa maana ya ufisi, mafisi na ufisadi. Kiza kitupu kama ni hivi. Na nzi naanza kuwaona. Wapo wengi kweli kweli. Naona lile nene kama nune. Naona na jingine kama kupe. Kweli kuna nzi kwenye choo kikuu ambacho jamaa amekibatiza kuwa chuo kikuu.

Kweli nzi hupenda uchafu. Na bila ujinga hakuna uchafu. Je, hawa washabikiao kiza na ujinga si nzi tena mafu? Jamaa kweli ana akili za ajabu! Amejua kuwapa jina wadudu hawa.

Juzi nilikutana na mtoto wa mzee Machungi akiwa analia. Alipigwa virungu na maefuefuyu hana hamu. Kosa lake eti ni kutaka chuo kisafishwe na inzi wote wauawe ili waweze kusoma vizuri. Unajua ilikuwaje?

Nzi mkubwa aliwaarika wenzake. Kwa vile chuoni kuna vyoo vingi, basi nzi wale waliona sasa wamepata pa kuponea. Waliingia kila kona hadi kwenye Cafeteria na mifuko yote pale chuoni kiasi cha kukigeuza chuo choo kikuu.

Maskini nzi hawakujali kuwa chuo ni mali ya wananchi. Wao walikigeuza chao huku wakiwatimua watoto wa wananchi!
Chanzo: Tanzania Daima Februari 4, 2009.

No comments: