The Chant of Savant

Wednesday 4 March 2009

Liyumba, ufisadi, utawala wa kijambazi na ulioshindwa



HUWA siachi kujiuliza, hivi watu wa aina ya Mwalimu Julius Nyerere wakifufuka leo itakuwaje?

Bila shaka, kwa kihoro na chuki, watajinyonga ili wasiwe sehemu ya utawala mbovu na wa kifisadi tulio nao.

Hivi hawa wanaotufanyia ufisadi na usanii huwa wanajisikiaje wanapokaa peke yao na kutafakari wanayoyafanya kama kweli wamebaki na chembe ya utu na uadilifu wa kufanya hivyo?

Kwa watu wanaofuatilia kufuru na sanaa zinazoendelea Tanzania, si haba, wanatucheka na kutuona kama mataahira.

Watendwa na watendwaji wote katika kapu moja.

Huwa siachi kujiuliza, hivi inawezekanaje nchi yenye kila nyenzo ishindwe kushughulikia wahalifu kama wa EPA na wengineo? Inashangaza licha ya kusikitisha na kuchukiza!

Kwa sasa, baada ya kuona filamu nyingi, kuna filamu moja imetawala, nayo ni ile ya Amatus Liyumba, iliyotungwa na wasanii wetu wakuu waliotuambia kuwa alikuwa ametoroka.

Swali hapa ni kweli alikuwa ametoroka au alitoroshwa; au kuna kikundi cha watu kilikuwa kinapima ujazo wa maji katika sakata hili?

Sasa tuna filamu ya minara miwili, tunapaswa kuwa makini ili isituleweshe tukawasawahau kina Kagoda. Liyumba ashughulikiwe sambamba na Kagoda. Bila hili kufanyika yote ni bure.

Kujibu swali hili nitatoa maelezo.

Mosi, hivi kama Liyumba angetoroka au kutoroshwa, wangetwambia nini? Kwanza, serikali ingethibitisha ilivyoshindwa kutimiza wajibu wake.

Pili hakimu aliyeamua kudhalilisha mahakama kwa kutoa dhamana tatanishi kwa mtu ambaye kisheria hakupaswa kuwa huru hata kwa sekunde moja kama sheria zingetumika bila kupindwa asingekwepa lawama.

Lakini pamoja na Liyumba kupatikana, je, tumejifunza nini hasa kuhusiana na utoaji wa dhamana?

Kosa la kwanza lingeanzia kwa aliyetengeneza hati ya mashitaka.

Mtu anahujumu uchumi unamfungulia mashitaka ya matumizi mabaya ya fedha ya umma na upotevu! Je, wanasheria hawajaliona hili?

Sasa baada ya kutafuta jibu la tatizo letu tunadandia matawi. Ndiyo. Tunadandia matawi kwa kuangalia mhusika wa filamu badala ya mtunzi na mwendeshaji wa filamu yenyewe!

Leo tunaambiwa watu wanamalizana kwa sumu. Je, hadi wanafanya hivi, sheria zetu na serikali yetu ambayo ndiyo msimamizi wa sheria hizi iko wapi?

Watu wanahujumu na kuuibia umma halafu wanapewa nafasi ya kuua! Bado, tunajigamba kuna utawala wa sheria na bora! Hakika haya ni matusi ya nguoni kwa Watanzania.

Ajabu ya maajabu ni pale unaposhuhudia wananchi wakishangaa yanayojiri kana kwamba hayawahusu! Kwanini tusiiulize serikali; kazi yake ni nini kama imeshindwa na kikundi kidogo cha wahalifu?

Kwa jeuri ya mpumbavu bado tunajisifu tutaleta maisha bora kwa Watanzania. Nasi kwa ujuha na upogo wetu tunajifanya hadhira wakati ndio wasanii wenyewe.

Ama kweli maneno ya Hassy Kitine yamekuja wakati muafaka.

Ingawa analaumiwa na maneno yake kupindishwa ukiachia mbali kupunguzwa uzito, Kitine kalenga kwa wakati muafaka.

Tukirejea sinema ya Liyumba, ni ushahidi kuwa hata utawala wa kienyeji haupo.

Kama kuna utawala basi si mwingine ni wa kijambazi na kifisadi.

Nikosoe ukitaka. Kama si wa kijambazi, majambazi kama Liyumba wangepata wapi jeuri ya kutuweka roho juu, sijui kutoroshwa bila kuogopa hasira za umma?

Huu ni ushahidi kuwa tu taifa la hovyo lisilopaswa kuwa kwenye uso wa ardhi. Mungu pishia mbali.

Ingekuwa hivyo, watu kama Liyumba wasingejidhamini kwa mali za wizi ambao wanashitakiwa kwao.

Kama kuna kosa kubwa ambalo litatugharimu tulilotenda, si jingine bali kuwa waoga na wanafiki.

Tunaogopa kuwambia wezi kuwa ni wezi na badala yake tunawaita waheshimiwa. Tunashindwa hata kuwaita waheshimiwa wezi!

Lengo la makala hii si kutukana wala kuzua. Tueleze. Kwanini serikali yenye majeshi, polisi, magereza, mahakama na kila kitu imezidiwa kete na kiumbe kama Liyumba anayesifika kwa ufuska na israfu?

Huu ni ushahidi kuwa tunaendeshwa kipumbavu na kipunda.

Wezi wetu tunawajua ila tunawaogopa utadhani wana uwezo wa kutuhilikisha. Tunaogopa vivuli vyetu. Wahalifu ni wahalifu. Angalia hata kuhimili dola kulivyoshindikana, badala yake vyombo vya dola vinatumika kulibomoa taifa badala ya kulilinda.

Rejea kwa hakimu kutoa dhamana kinyume cha sheria huku akijua. Je, alilishwa nini mwanasheria huyu? Je, alijiamini nini kufanya makosa kwenye mali ya umma kama si kuwa na waheshimiwa wezi nyuma yake?

Hii inanikumbusha ujambazi uliotembezwa wakati wa kesi ya Augustine Mrema akidai mwenyekiti wa CCM taifa kuhongwa sh milioni 500.

Unakumbuka ilikuwaje? Aliteuliwa hakimu mmoja ‘kihiyo’ hivi akavuruga kesi hiyo na mwisho wa yote mtuhumiwa alizidi kupeta.

Jana walimtorosha mtuhumiwa mkuu Daud Ballali, waliyeishia kummaliza ili kumaliza ushahidi.

Kesho wanaweza kumtorosha Liyumba. Mtondo hatujui watamtorosha nani.

Kitu kimoja kiko wazi. Laana ya jinai yao itawaandama waanze kumalizana kama ilivyoripotiwa kuwa wameanza kupeana sumu.

Mungu tusaidie wamalizane badala ya kutumaliza sisi. Laana hii itawakumba kuanzia mfagiaji hadi mungu mwenyewe, baba wa wizi na ujambazi huu.

Sakata la sinema ya kutoroka au kutoroshwa kwa Liyumba inathibitisha tusivyo salama. Ni ushahidi kuwa Jeshi letu la Polisi na idara zote za upelelezi, ulinzi na usalama vimewekwa kwenye mikoba ya mafisadi. Hivi leo tukivamiwa na nchi makini, mbona tutamalizwa kama kuku!

Kinachokera ni wasanii kuendelea kujiaminisha kuwa sinema yao itamalizika wao wakiwa salama. Frederick Chiluba, rais wa zamani wa zambia alifanya maajabu yanayofanana na haya.

Kwa wafuatiliaji wa vituko vya viongozi wa Afrika watakuwa wanakumbuka jinsi kifo cha mtoto wa mzee Kenneth Kaunda, Meja Wezi, kilivyozua utata huku serikali iliyokuwa chini ya Chiluba ikinyooshewa kidole kuhusika na tukio hilo.

Ni Chiluba huyo huyo enzi zake, alijaribu kufanya maajabu kwa marehemu Levy Mwanawasa (makamu wake aliyetokea kuwa rais baadaye na kumshughulikia Chiluba).

Kama wezi wetu, alidhani atawamaliza wote, asijue mwisho wa mchezo atamalizwa yeye.

Sasa muulize yuko wapi? Naye anaugulia akihesabu siku huku roho ikimuuma. Masikini hataishi kutumbua chumo lake la wizi, sawa na vibaka wetu.

Daniel arap Moi, rais wa zamani wa Kenya, yeye serikali yake walishutumiwa sana kwa kifo cha Robert Ouko na Ezekiel Oyugi, aliyedaiwa kutumika kumuua Ouko na wengine wengi.

Ingawa Moi angali akiishi maisha ya raha mstarehe, kwa mabingwa wa kusoma alama za nyakati watakubaliana na mimi, siku zinakuja ambapo hatakuwa salama kutokana na tuhuma mbalimbali zinazoelekezwa kwake, anazodaiwa kuzifanya wakati akiwa madarakani.

Mwaka kesho tuna uchaguzi mkuu. Kwanini tusichukue somo kutoka Kenya baada ya kuonja waliyoonja wakenya? Je, tunaogopa tutachagua kenge wale wale watakaokuwa wemejiweka kwenye kundi la mamba? Kwanini tusiwe makini?

Tuhitimishe hivi. Kuna haja ya kubadilika na kuitaka serikali itueleze wajibu wake ni nini kama wapuuzi na wezi wachache wanaweza ‘kutoroshwa’ mchana? Tuiulize. Ina nini cha mno cha kutufanyia ili tuichague mwakani iwapo kuwapo kwake ni bora kuliko kutokuwapo?

Sinema ya Liyumba, ingawa imetuonyesha kama taifa la wapuuzi na wahalifu, si wote. Lazima itufanye tutafakari badala ya kushangaa na kulalama.

Sinema ya Liyumba ituamshe, tukatae kuruhusu wezi kujidhamini kwa mali za wizi kama inavyoendelea kufanyika.

Kila la heri.
Chanzo: Tanzania Daima Feb. 4, 2009.

No comments: