The Chant of Savant

Friday 17 April 2009

Ufunuo wa Mpayukaji kwa Wadanganyika


Huu ni ufunuo kama ulivyoshushwa kwa Nabii Mpayukaji mtume kwa Wadanganyika. Umepigwa mhuri wa mihuri na kuvuviwa uvuvio wa uvuvio kwa amri ya mfalme wa wafalme.

Tazama naona anga ya asubuhi iliyochukia mithili ya faru aliyeuliwa mtoto. Naona malaika wa nuru akinushukia na kuniambia. “Nena usiogope Nabii wa Mungu Mpayukaji mwana wa mzee Msemahovyo mjukuu wa mzee Wambie.

Tazama mbingu ile yenye hasira inafunguka. Naona maiti aliyenuka akiwa amevalishwa mavazi ya hariri yenye kumeremeta akizungukwa na maiti wengine waliooza na kubakia mifupa huku wakiwa uchi wa mnyama!. Naona maiti wakimsujudia yule maiti aliyevaa kitani. Anaonekana alikuwa akichekacheka. Kwani uso wake unaonekana hauna kunyanzi na meno yake yote yamekenuliwa.

Kinyume na maiti msujudiwa, maiti wengine wamekondeana na sura zao zinaonyesha kunyanzi ingawa baadhi yao wanaonekana walikufa wakiwa wamenona.

Namuuliza Malaika. “ Hii maana yake nini? Anajibu bila kujivunga. “Huu ni mfano wa taifa lililoongozwa na mfalme fisadi akaliteketeza. Mfalme huyu aliitwa Kiweke aliongoza taifa la Tanzia miaka mingi baada ya gharika la Nuhu.”

Malaika alipiga mbawa zake na kutoa cheche na kuendelea. “Nabii Mpayukaji. Nenda kawambie watu wako wajue wakiendelea kufanya ufisadi yatawakuta yaliyowakuta Tanzia.”

Mbingu inazidi kufunguka. Tazama naona yule maiti msujudiwa akitoa wadudu kinywani. Nahisi harufu kiasi cha kutaka kutapika pale alipofunua mdomo wake kuongea na maiti wamsujudiao.

Anasema. “Wapendwa Watanzia nyinyi mko hai ingawa mwaitwa maiti. Nami si maiti ingawa nazushiwa umaiti. Ningekuwa maiti nisingevaa hariri na kukaa kwenye kiti cha enzi.” Anageukia kiti chake cha enzi kilichokwishagugunwa na mchwa. Kimezungukwa na dumuzi na mifupa itokanayo na watanzia awalao. Kiti ingawa kinaonekana kuwa cha enzi na kizuri, ni kichafu hakuna mfano. Kwani kila akikikalia hujaza uoza na harufu imtokayo.

Namuuliza Malaika.”Nini maana ya haya?” anasema. “Harufu ni alama ya uongo na uoza ni alama ya ufisadi. Mifupa na dumuzi vilivyozunguka kiti ni wale mafisadi waliokuwa wakimpamba Kiweke wa Tanzia. Maneno uliyosikia ni kujilisha pepo kwa Kiweke akijidanganya na kuwadanganya Watanzia.”

Alisugua mbawa na kutoa cheche nyingi zaidi ya zile za mwanzo na akaonyesha kusononeka na kuendelea. “Harufu mbaya imtokayo Kiweke kinywani ni uongo na ahadi alizokuwa akizitoa kwa Watanzia. Kawambia Wadanganyika washike maneno haya. Ni kwa ajili ya ukombozi wao.”

Aliendelea. “Ile mifupa uionayo imejaa kwenye kiti cha enzi, ni Watanzia wote waliodhulumiwa haki na kuibiwa mali na raslimali zao.”

Mbingu ilifunguka tena. Tazama niliona mavazi ya hariri yakikwanyuliwa na kitoto kichanga na kumuacha Kiweke akiwa uchi wa mnyama akitokwa usaha kila sehemu. Ulimtoka kwenye midomo, masikio, macho, puani na matundu yake ya nyuma. Kumbe yale mavazi yalificha aibu isiyowahi kuonekana duniani! Kumbe Kiweke alikuwa hana sehemu za siri. Hakuwa mwanamke wala mwanamume bali dude tu! Harufu ya usaha huu ilitosha kuua tembo mia kwa tone kutokana na ukali wa harufu hii. Nilizidi kusukwa sukwa. Nilipokaribia kutapika, tazama Malaika yule wa nuru alipitisha mkono wake kwenye pua zangu nikanusa riha nzuri.

Alisema. “Yakupasa uyaona na kuyashika haya ili ukwaonye Wadanganyika.

Nilimuuliza maana ya haya. Alisema. “ Umeona yule mtoto aliyemvua nguo mfalme? Huyu ni yule ajaye atakayetawala na kuitiisha nchi ya Tanzia ambaye watabiri walishindwa kumtabiri.

Huu usaha ulioona ni ishara ya ulushi na ugonjwa utokanao na ufisadi ambao aliutengeneza Kiweke ili ummalize. Ni ujanja ujanja na ujahiri vilivyomuwezesha Kiweke kuwadhulumu Watanzia bila kuchelea mbele.”

Mbingu ilifunguka tena ili nione ya kuona na kushika ya kushika nikiyaweka rohoni kwani yametiwa mhuri. Mara mfalme Kiweke aliyekuwa akitokwa usaha wa damu alianza kuvimba nusu ya kupasuka. Mara dhoruba kali alianza kuvuma huku radi na tufani vikiitikisa mbingu kiasi cha kunitia woga nusu ya kukimbia. Pembeni naona kundi la njiwa, tausi, kuku na baadhi ya kunguru walioshika mishale na ngao wakielekea alipo Kiweke na watumwa wake. Naona na siafu na myuki wakija wamepanua vinywa vyao na kutoa meno yenye makali kama msumeno kuelekea kiti cha enzi.

Nauliza na hii maana yake nini? Malaika anapiga mbawa zake na kutoa cheche tena kwa wingi zaidi ya mwanzo. Anatabasamu na kusema. “ Radi tufani na vimbunga ulivyoona ni nguvu ni ishara ya mabadiliko. Na hawa njiwa, kuku, tausi na baadhi ya kunguru ulioona ni Watanzia waliosifika kwa upole wao ingawa kulikuwa na kuku ( yaani wale walionyonywa kiasi cha kula wasichozalisha na kuzalisha wasichokula kama kuku) tausi na njiwa (watu wema wasio fisadi), kunguru (watanzia wachoyo waliokuwa wakiuza kura zao na kuabudia mafisadi) wakielekea kiti cha enzi kumkabili na kumuangusha Mfalme Kiweke na kumsambaratisha yeye na utawala wake dhalimu muhimili wa uovu

pamoja na watumwa na wezi wenzake. Siafu ni wale majeshi yote waliokuwa walinzi na muhimili wa utawala dhalimu wa Kiweke. Wameamua kuungana na umma baada ya kungundua kuwa kumbe nao walikuwa wakitumiwa na kunyonywa sawa na watanzia.”

Mbingu ilifunguka tena. Niliona wale watumwa waliokuwa wakimsujudia Kiweke wakigeuka nyoka, nge, fisi mbweha na mbwa mwitu huku wakianza wakiraruana. Walianza huku Mfalme akiwa pembeni akiangalia asiamini. Kwani naye aligeuzwa mbwa tena mdogo asiyeweza kumtisha hata mwana mbuzi!

Niliuliza maana ya haya ni nini? Malaika alinyoonya mkono wake na kutoa kitambaa na kuanza kupunga akisema. “Wale wanyama ulioona wamelaaniwa na wanapenda nyama. Nyoka unajua hula wadudu lakini ana sumu. Waliobaki wote wana meno na makucha makali kwa ajili ya kula wanyama wengine. Lakini hapa unaona nyoka akimng’ata nyoka na wale wanyama wakiraruana kila mtu na mnyama aina yake. Hawa ni wapambe wa Kiweke. Wameanza kugeukana baada ya upepo wa mabadiliko kuvuma kuelekea kupeperusha utawala fisadi wa Kiweke.”

Tutaendelea tukijaliwa.

Walatini husema radix molurum est cupiditas yaani tamaa ni mzizi wa maovu yote. Tazama Kiweke alijifanya mjanja asijue kila lenye mwanzo shurti liwe na mwisho!
Chanzo: Tanzania Daima April,15, 2009.

No comments: