The Chant of Savant

Wednesday 27 May 2009

Amri ya Pinda juu ya UBT Kingunge vipi?


BAADA ya kugundulika wizi na hujuma vya kutisha kwenye Kituo Kikuu cha Mabasi cha Ubungo vilivyokuwa vikitendwa na familia ya kada maarufu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Kingunge Ngombale-Mwiru, waziri mkuu alitoa amri kwa mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali kuchunguza na kuutangazia umma alichogundua.

Ajabu siku zinazidi kuyoyoma. Umma haupewi taarifa wala chochote kuhusiana na kadhia hii. Kwa ukumbusho, kashfa ya wizi wa mabilioni ya pesa toka UBT iliibuka mwezi Machi na waziri mkuu Mizengo Pinda alituaminisha angavalia njuga ufisadi huu.

Lakini kadiri siku zinavyozidi kwenda, tunaletewa sanaa nyingine kubwa ikiwa ya hivi majuzi baina ya Reginald Mengi na Rostam Aziz kiasi cha kufunika kashfa hii pamoja na nyingine kama vile Kagoda. Je waziri mkuu anaweza kuupa umma taarifa juu ya alikofikia katika kupambana na kushughulikia kadhia hii?

Wengi walingoja Kingunge ajitetee angalau wasikie hoja zake. Ajabu hadi sasa ni miezi miwili, Kingunge, kama Benjamin Mkapa, ambaye naye anahusishwa kwenye ufisadi mwingi tokana na tamaa za Bi. Mkubwa, hajajibu. Je ni kiburi kama cha Mkapa kwa vile anajua chama kitamlinda? Je hana cha kujitetea, hivyo kimya hiki ni ishara ya kukiri kuwa yaliyodaiwa ni kweli, hivyo ni kubali yaishe? Je anatumia mbinu ile ile ya mwenyekiti wake rais Jakaya Kikwete ya kukaa kimya na kujifanya hasikii wala hajui kitu ili hatimaye mambo yajifie?

Je na kimya cha waziri mkuu kinamaanisha nini? Je ameitwa na kukaripiwa naye akaamua kuufyata na kuishia mitini? Je waziri mkuu amevutwa shati na kuambiwa sera ya CCM ya kulinda hairuhusu watu wazima kuadhiriana?

Wakati maswali yote haya yakingoja majibu, haijulikani kama mtuhumiwa amesimamishwa kuendesha hujuma yake pale UBT!

Hii maana yake ni kwamba watawala wetu wanaendelea kutufanyia usanii ili muda uende waendelee kuchuma. Kuna haya ya kuzidi kulidurusu na kulinusa nusa sakata zima la Ubungo kuanzia kwa familia ya Kingunge, waziri mkuu, mkaguzi mkuu wa fedha za serikali na popote penye harufu ya jinamizi la Ubungo.

Kuna tabia chafu inaanza kujengeka na kuota mizizi. Watawala wetu wamethibitisha kuwa na vinywa vikubwa lakini wasio na masikio wala ubongo. Ni maangizo mangapi yalikwisha kutolewa nao yasitekelezwe? Je huwa wanafanya hivyo kuturidhisha wakijua fika hayatatakelezwa? Je hawa wasiotekeleza maagizo ya wakubwa wao wanapata wapi kiburi kama siyo karata tatu?

Ndiyo. Maana ukiangalia hata ujambazi wa Kagoda unavyozidi kufumbiwa macho na kupigwa tarehe ili uchaguzi ujao ufanyike halafu ngoma itoke, unaona dhahiri kuwa kama umma hautaamka na kukumbushia hata kuchukua hatua nyingine mujarabu, uwezekano wa mibaka kuendelea kutuibia na kubaka uchumi wetu ni mkubwa. Kwa hali ilivyo, wananchi wanachezewa sawa na kile kinyago cha Joyce Wowowo. Kila tukikaribia kumtia adabu fisadi yeyote, ima tunasahaulishwa kwa kuletewa sanaa nyingine au kutokumbushia. Leo rasmi nimeamua nimkumbushie waziri mkuu. Najua halazimiki kutoa maelezo kwa msukumo wa makala yangu. Lakini bado hii inaweza kurjesha kashfa ya Kingunge kwenye mjadala. Na saa nyingine wahusika wanaweza kuona haya wakaamua kuchukua hatua mujarabu kwa wakati na uzito unaostahili.

Imeishia wapi kashfa ya wanyamapori ambapo hata walinzi wa mbuga walilalamikia wakubwa wao wanaoshirikiana na majangili? Iko wapi taarifa ya waziri wa nishati na madini Williama Ngeleja kuhusiana na wamilki wa Kiwira? Sasa ni karibu mwaka, Ngeleja amekuwa akilidanganya Bunge angewaweka wazi bila kufanya hivyo. Je amenyamazishwa au katumwa na wahusika asifanye hivyo?

Wakati kufuru hii ikiendelea, CCM na serikali yake, bila aibu eti inawaaminisha watanzania waipe kura kwa vile imeleta maendeleo! Hivi haya ndiyo maendeleo ya watawala kuwa vidhabu wakisema mengi na kutotenda hata moja? Rejea ahadi alizotoa Kikwete akiingia madarakani. Ametekeleza ngapi? Hakuna hata nusu! Lakini bado anazidi kujiaminisha kuwa lazima apewe muhula wa pili akazidi kuvuruga! Je tutaendelea kugeuzwa mazezeta na kutumiwa kama vijiko tusiambulie kitu?

Tunatembezewa ujambazi mchana kweupe nasi tunanyamaa kana kwamba hii nchi si yetu! Hebu jikumbushe alivyotoroshwa gavana wa zamani wa benki kuu Daud Ballali hadi kukolimbwa kuficha ushahidi ambao ungeweza kuumbua mnaowaona watukufu na wasio na hatia. Nini kimefanyika zaidi ya kuchukuliwa kama tukio la kawaida? Tulipaswa kuwabana watawala waunde tume. Maana pesa iliyoibiwa si yao wala mama zao. Ni pesa ya watanzania wanaoendelea kuteseka sawa na pale Ubungo.

Mheshimiwa Pinda, je umefikia wapi na kuchunguza na kushughulikia kashfa ya Kingunge na familia yake pale Ubungo? Tumechoka kusubiri na maneno matupu bila vitendo. Shughulikia kashfa ya UBT kwa ipasavyo badili ya maneno matamu.

Nangojea jibu lako haraka na kwa udi na uvumba.
Chanzo:Tanzania Daima Mei 27, 2009.

No comments: