The Chant of Savant

Thursday 3 September 2009

'Well done' Kingunge dhidi ya kanisa


KWA mtu anayejua historia ya mzee Kingunge Ngombale-Mwiru na jinsi anavyosusurika kujisafisha na kujijengea kinga chamani, hashangai kusikia anayosema kuhusu waraka wa Kanisa Katoliki kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2010.

Kimsingi, waraka wa kanisa umetuama kwenye uadilifu na kuchagua viongozi waadilifu kitu ambacho binafsi nadhani kuwa ni kero na ndoto kwa watu wa kada ya Kingunge.

Hawawezi kumpenda mtu anayeuzindua umma, kujikomboa na kuutokomeza ufisadi ambao pengine kwa walio madarakani ni mradi unaowaingizia pesa nyingi.

Nashawishika kuamini kuwa ufisadi ni sera ya kundi la kada ya kina Kingunge aliyeamua kuikamua serikali kupitia Ubungo Bus Terminal!

Badala ya kumlaani na kumshutumu Kingunge, namshukuru kwa kumtoa paka kwenye kofia. Maana chama cha Kingunge (CCM) kimekuwa kikikanusha na kujinakidi kama chama kilichodhamiria kuleta maendeleo ingawa matendo yake ni kinyume.

Hebu fikiria; kama wazee tuliodhani wana busara na udhu, mfano Kingunge, wanaweza kusimama na kuwakaripia watu wema wasihimize wema, hao wengine wakoje?

Matendo na maneno ya Kingunge yakiongezewa na ya CCM ni ushahidi wa uozo usiovumilika. Ni harufu mbaya ya chama kilichochoka kiasi cha kulea na kutukuza ufisadi na mawazo mgando. Ni ushahidi kuwa kinachoitwa maendeleo ni ndoto.

Tulipoambiwa maisha bora kwa wote, tulisahau kuwa wote waliomaanishwa katika hilo ni wale walio karibu na Kaisari. Waliobaki lieni tu. Hamna chenu hapa. Kwangu hii ndiyo maana sahihi ya tafsiri ya karipio na kejeli za Kingunge na wenzake.

Kingunge haoni baya lolote katika sera nyakuzi na nyemelezi za chama chake. Ataona baya gani iwapo anakula mkate ulioloa siagi akiwaambia Watanzania wale mawe?

Kwa kina Samuel Sitta, John Malecela na wengine waliogutuka na kukengeuka kuwa umma unaweza kushtuka na kufanya kweli, wakaona kuwa ufisadi ni mbaya.

Wao ingawa wamo ndani wakishiba na kusaza, bado machale yanawacheza kuwa umma huu si wa mawe ni umma wa wanadamu ambao siku zote ni vigumu kuwatabiri.

Hivyo basi, kwa nia nzuri au mbaya, wameamua kusimama upande wa haki hasa kipindi hiki tunapokaribia uchaguzi ili kuhakikisha hawakosi baraka za wananchi.

Hawa wanaogopa kwa kufahamu ama kuona cheche za mabadiliko zilizo wazi kwenye jamii ya Kitanzania. Hawa si vichwa ngumu kama kina Kingunge na chama chao.

Wanaendelea kuwahadaa Watanzania, kama vipofu, kuwa CCM imefanya maajabu! Kama kuna maajabu iliyofanya si mengine, ni kuendelea kuwa madarakani bila kutimuliwa na umma licha ya kashfa mbalimbali zinazoihusisha yenyewe na vigogo wake.

Kingunge ni kada ya wana CCM wanaowachukulia Watanzania kama wale wa kwenye ‘Pepo ya Mabwege’. Hawa kwao, ni halali kwa kupe kukwea kwenye mgongo wa ng’ombe na kumnyonya.

Hawategemei ng’ombe hata anyonywe na kukonda vipi aasi. Kwa kuwa ni hayawani asiye na uwezo wa kupambanua mambo.

Hivyo, kwa kuonyesha jeuri na kejeli za CCM tuna kila sababu ya kumpongeza na kumpenda Kingunge kwa kutuzindua ili tufanye kweli.

Kingunge ananikumbusha hadithi ya mke wa mfalme aliyesikia watu wakiandamana mitaani kupinga utawala wa kijambazi wa mumewe mfalme kwa kusababisha ukosefu wa mikate.

Mama huyu juha na kipofu aliwajibu waleta habari: kama hakuna mikate si wale keki? Maskini juha huyu hakujua kuwa nje ya kasri lao, maisha yalikuwa ni jehanamu!

Leo CCM, watawala, wapambe wao kama kina Tambwe Hiza, Salva Rweyemamu na wengine wameshiba hadi kulewa kiasi cha kujiaminisha kuwa mambo yataendelea kuwa yalivyo.

Haiwezekani. Haiwezekani kabisa CCM iendelee kuwa madarakani tena kwa usalama huku ikiongozwa na watu ambao ama wao au marafiki zao wanatuhumiwa kwa ufisadi.

Kama kina Kingunge wangesoma alama za nyakati, wangeshinikiza watuhumiwa wa ufisadi wanaotajwa kila kukicha wafikishwe mahakamani na kusafishwa au kupatikana na hatia kutokana na tuhuma zinazowakabili.

Wasingeridhika na matumizi ya mchezo wa nyani kusafishana kwa mawe na vijiti wakati wahusika hawasafishiki.

Watu wenye visheni na misheni wangelaani badala ya kubariki. Wangeonya badala ya kutisha. Wangesuluhisha badala ya kupatiliza. Wangetahadhari badala ya kukejeli.

Ila kitu kimoja ni wazi. Watanzania hata wa mashambani wanaanza kujua kinachoendelea huko juu. Wanajua kuwa deste lao limejaza mikono ya walafi na wachafu wakila bila kunawa tena kwa mikono na miguu.

Kwa watu wanaojitakia mema, wangetumia ukaribu wao na Rais kumueleza ukweli kuwa utawala wake umeshindwa kila upande na kwa karibu kila kitu.

Wangemkumbusha ahadi alizotoa hasa kupambana na ufisadi. Ajabu wameamua kwa makusudi kumuingiza kwenye kila upuuzi. Je, wanafanya hivyo kwa sababu wanajua alikuwamo tangu mwanzo au kwa vile haoni kama wao?

Rais naye ameridhika. Kama mwenyekiti wa chama nadhani amebariki haramu na kulaani halali. Namna hii hatufiki popote. Hatuna tofauti na pweza ajipaliaye mkaa asijue utamuunguza na kumgeuza mafuta.

Hii ni alama na ushahidi wa chama na wakubwa wake kufilisika kisiasa kisera na kimkakati. Kwa nini kupinga watoa hoja badala ya hoja yenyewe?

Ninaamini CCM ipo taaban hasa tunapoelekea mwaka 2010. Haijitambui mbele ya ufisadi kwa kuwa watuhumiwa wakuu wa ufisadi wamo ndani yake, ndio wanaoisaidia kwa namna moja ama nyingine.

La muhimu kufanya si kupambana na ukweli bali kutafuta ukweli ili kuwa huru. CCM ina lipi la kufaa kurejeshwa madarakani? Naamini kwamba kuirudisha CCM kwenye utawala ni kubariki dhambi isiyostahiki msamaha!
Chanzo: Tanzania Daima Agosti 2, 2009.

No comments: