The Chant of Savant

Tuesday 19 January 2010

Mie mali sitangazi ng'o

JUZI nilitaka kupasuka. Nilitaka kupasuka baada ya kusoma magazetini kuwa kumbe waziri mkubwa wa Jamhuri ya Mgongano ya Kaya, Mizengwe Pita alitangaza mali zake hadharani.

Huyu jamaa hajui anatuponza wengine hata kama hatumo kwenye lisirikali lake? Laiti angejua baada ya kutia guu kijiweni swali la kwanza litakuwa ni lini nitatangaza mali zangu!

Bwana mkubwa uwe unaomba ushauri wetu hata kama hatumo kwenye lisirikali wala chama chako. Hayo ni ya wakubwa tuyaache. Tutayamaliza tujuavyo.

Sasa Pita kapindua hata wakubwa zake kama sisi akaamua kutangaza mali bila mizengwe. Kweli mzee mzima nitanusurika? Juzi kuna mshauri wangu alitaka niige mfano wa waziri mkubwa. Sikumuelewa.

Kwanza waziri mkubwa mwenyewe si wangu ni wa linchi. Mie ni kiongozi wa kijiwe bwana. Niliamua kujitetea kwa mshauri wangu huyu anayejitia ni mzalendo.

Baada ya kurejea nyumbani nilimfikishia salamu za kijiwe hasa kutaka nitangaze mali zangu. Kumbe naye alishazinyaka kwenye runinga yetu. Hivyo ulikuwa ni msiba kwetu hasa ikizingatiwa kuwa mwaka huu nina uchaguzi kijiweni na walevi wanajua madudu na sanaa zangu zote.

Swali la kwanza ilikuwa ni kumuuliza Bi mkubwa tufanyeje. Alijibu kuwa tufiche baadhi ya mali zetu kama vile mikufu yake, viatu vya bei mbaya na kadhalika. Niliona ni jambo zuri. Tatizo lilikuwa ni je waliokwisha kumuona na vipuri kama hivyo nisipotangaza si watauliza? Jibu? Alibaki kutoa mimamcho!

Wakati mimi nikihangaika na jinsi ya kuepuka kikombe hiki, najiuliza. Naye jamaa yangu nonihino wa juu kule atafanya nini iwapo walio chini wameamua kufanya kweli yarabi? Ajabu tunajua kuwa Shortie wake chini ya MAWAWA ameishatengeneza mabilioni kama si matrilioni. Sijui atakuja na kamba gani msanii huyu toba?

Jamaa inaonekana kuna uhasama kwenye usalama wa taifa. Inakuwaje jamaa aweke vitu vyote wazi wakati huu mbaya? Je utabiri wa shehe Ubwabwa unaanza kumgeukia jamaa au wale wazee wazima wenye hekima kama mlima wameanza kufanya vitu vyao. Pamoja na kwamba nami nimeoza, nangoja kuona jamaa atalitatua hili kwa kamba gani au sanaa tuseme.

Je naye atafanya kama alivyoshauri mke wangu-kuficha ukweli na kuwaongopea walevi wake au ataamua kuendelea kula pini kama mimi?

Tunituni alijifaragua akatangaza wakati wa kuukwaa. Lakini wakati wa kuutema sikusikia cha mali wala hali zaidi ya kutimka kama kibaka baada ya kuwa amechafuka mbele nyuma. Je jamaa yangu hapa atatembeza sanaa gani ili niige mfano ninusurike bila kuadhirika?

Naona ataagiza Shehe Ubwabwa atabiri kuwa akitangaza mali zake atakufa ghafla. Siku hizi kufa ghafla ni sera ati. Hivyo si bora kutangaza mali kabla ya uchaguzi wezi waliotamalaki kuteka mabasi wanaweza kwenda kumuibia jamaa hata kumdhuru na kaya ikawa kwenye mtafaruku.

Kwa vile wanakaya wengi ni waumini wazuri wa ushirikina na udaku, huenda wataingia mkenge kwa mara nyingine na jamaa aponyoke msalabani saa tatu kabla ya kusulubiwa. Kama atawapata katika hili nitaamini kuwa jamaa hawa kweli mataahira. Mie simo. Mie janja bwana. Naendelea kukamua wakati wao wakikamuana.

Jana nilipita kwenye baa moja jina siri kubwa kwa usalama wa taifa kama kuchonga peni dhidi ya ndata wanapoiba miexaminations. Nilisikia jamaa akisema ana usongo na jamaa. Anasema asipotaja jumla ya nyumba zake hasa zile ndogo, jamaa atajinyonga mbele ya listeitihausi.

Mwingine nilimsikia kwa masikio yangu mwenyewe akisema kama jamaa hatatangaza mali, yeye atazitangaza mali za jamaa azijuazo.

Jamaa ingawa ni mlevi alikuwa na pwenti. Unajua alisemaje? Alisema hakuna haja ya sisi wakubwa kudanganya kwa sababu mali zetu zinajulikana. Kwa kusema hivyo nilisikia kiroho kikininyatuka. Maana huyu jamaa alinitisha.

Kama wanajua mali zetu si anaweza kutuvua nguo kichaa huyu tena hadharani?

Kumbe walevi wanajua mengi sema wanajifanya mabwege tu. maana mwenzie alisema tena kwa uhakika kuwa anaijua miradi mikubwa mikubwa ya bi mkubwa kule kusini! Mwenzenu kusikia hivi nilisikia haja ndogo ikianza kunibeep.

Vyoo vyenyewe vya kulipia na siku hiyo sikuwa nimetembea na kashi zaidi ya ATM mashine iliyonusurika kuchanywa na waziri nonihino alipomuuliza mlinzi fulani: unajua mimi ni nani? Jamaa mmoja alisikika akijibu: “Fisadi wa kawaida kisiasa aliyependelewa.”

Basi bwana, nikiwa naanza kuloa kwa jasho, nilingoja jamaa amalize nijue kama anajua habari za kijiwe changu. Maana baa ile iko karibu na kijiwe chetu. Akiwa anajiandaa kusema si mlevi mwingine aliingilia kati. Alisema: “Sisi hatutaki kutangaza mali tu bali kueleza hiyo mali ilivyopatikana wakati sisi tunakufa bila hata tone la mali.” Du! Kumbe walevi wanajua siasa kuliko wanasiasa.

Mara nilimsikia mlevi mmoja akisema: “Nangoja kusikia waziri wa uwekezaji na uchukuaji na kadhalika akitangaza utajiri wake. Maana kila siku humuona mwanae akiendesha Hummer anapokuja mtaani kumchukua changudoa jirani. Hubadilisha magari kama nguo. Je, huyu ataweka mambo hadharani madudu kama haya?”

“We unasema huo mgari na kubadilisha magari kama tai. Mbona huongelei yule kitegemezi wa vidudu aliyehonga wapiga kura wa kamati ya nonihono kumchagua tena kwa kukata madafu 35,000 kila kichwa? Hawa jamaa wanatufanya sisi wapuuzi siyo? Wanarithisha ulaji kwa watoto wao je watoto wetu wale wapi? Baya zaidi wanasema kaya ni yetu sote wakati wamejibinafsishia wao na walamba viatu wao!”

Kicheko.

Mwingine alisema. “Natamani mzee wa Vijipesa au Daktari Iddiliishia kwa Rashid naye atangaze tujue kama atatangaza akaunti yake ya Londoni.” Mwenzie anamkosoa na kusema: “Sema Landani siyo Londoni bwana we.”

Nikiwa najiandaa kuondoka, mlevi mmoja alitoa mpya! Alisema. “Nijuavyo sera za sanaa na mibangaizo ya kaya hii, jamaa atatufunga kamba na kusema ameruhusu wa Kupinda atangaze vitu vyake ili yeye afanye hivyo baada ya uchaguzi. Baada ya hapo, imetoka lala salama. Mmeliwa wajameni. Jamaa ana roho ya chuma hatangazi kitu na akifanya hivyo sanaa tupu.” Mwenzie aliingilia ghafla.

Nkiwa najiandaa kusikia bomu jingine si mlevi mmoja mwenye lafudhi ya Kiha alikuja na mpya. Alisema. “Mugaboye, mie nashaangaaa.

Umesikia yale ya Zaainzibaaa. Eti yule Mugabo wa madevu anataaka uchaguzi uhairishwe atimize dili lake la kutumiana na Karumekenge wa Migebuka! Karabaye mugaboye! Hizi ni ngorane gusa ye.”

Hili limenikera hadi natamani nimlambe mtu bakora. Eti kule Zaainzibaa yule jamaa wa Madevu aliyejigeuza nyumba ndogo ya Karumekenge anasema tusifanye chaguzi? Is he sick or what? Akasome katiba aache uvivu wa kufikiri.

Kwa vile haja ndogo iliendelea kunibana, niliamua kukitoa nikiwaza jamaa yangu, kama mimi atafanyaje?

Tangazeni mali zenu muumbuke. Hata mkigoma, mtaumbuka tu kama Madevu na Karumekenge wanavyoumbuka na kuhaha kutuweka sawa wasiweze.

Mie simo ila nyinyi mmo tu tangaza au tangaziwa tujue nani afaa na nani amechemsha. Hapa kuna haja ya kupigana vibuti kama alivyosema Matewo wa Kareishi. Jamaa amezidiwa na hana sera wala sura.

Lo! Kumbe nami nahusika! Naona jamaa wa tume ya maadili wanakuja kuulizia utajiri na madili yangu. Acha niishie.
Chanzo: Tanzania Daima Januari 20,2010.

No comments: