The Chant of Savant

Sunday 23 May 2010

Mwenzenu ulevi umeniponza

JUZI baada ya kuutwika nilijikuta nafanya kituko kilichoniacha bila nguo! Japo nilikuwa nimebwia ulabu, nikiri na kusema ukweli. Jambo nililofanya limewaacha wanakijiwe wakinikamia kwenye uchafuzi ujao.

Yaani tukio hili lilinikumbusha watawala kama farao Amenmesse, Nabkkadnezza mwana wa Nabopolassar, Julius Caesar Assas aliyejiita Mungu, Nymphidius Sabinus, Iulius valens Lucianus, Sadam Hussein aliyejiona bora hadi akaweka dhahabu chooni akaishia kukutwa kwenye shimo la tandu na wengine wengi waliotekwa na ulevi wa kinywaji kiitwacho madaraka wakaishia kuwa machukizo na hasara kwao na jamii zao.

Niliwakumbuka majuha hawa waliojiona wajanja wakaishia kuwa aibu na machukizo milele ili waliofuatia wajifunze ingawa si kwangu. Mie sijifunzi kutokana na ujanja si ujuha na upofu kama wale jamaa zangu.

Siku hiyo niliwakumbuka wasomi maarufu kama Plato, Socrates, Marcus Tullius Cicero, Leucipus na wengine wengi waliotoa maonyo ya kupuuzwa na walioyapuuzwa wakapatilizwa vibaya sana.

Nisichoshe na falsafa. Maana zinanikumbusha mbali nilipokuwa nikisomea PhD yangu ya upayukaji kule Harvad.

Tuyaache watu wasianze kusema eti ninajidai kwa kubukua wakati sina sera wala sura ingawa nina PhD. Ila elewa. PhD yangu si ya heshima wala ya kughushi kama wale jamaa zangu.

Hata hivyo inabidi nijilaumu kwa kichwa ngumu na upofu wangu. Kwani Msomi Mkatatamaa alishanionya kuwa nisome alama za nyakati nikadhani analia maya. Alinipa live kuwa nimelewa madaraka kiasi cha kuanza kujiona muungu mtu. Alisahau kuwa huwa sina muda wa kusoma vitabu.

Nitasomaje wakati yangu ni makamuzi kwenda mbele? Nisome kupata nini wakati nilishapata zamani? Walevi wawe wakubwa, wadogo hata wenye madaraka huwa hawana tabia ya kujisomea. Watakunywa saa ngapi?

Unajua ilikuwaje? Si wateja wa kahawa walilalamika kuwa nakunywa kahawa bure na kutanua sana kiasi cha kuwapandishia bei ilhali hali zao ni dhoofu ilhali. Waliongeza kuwa mie na mke wangu na washirika wangu tunafilisi kijiwe kutokana na kupeana kahawa na kashata bure huku tukiwatwisha wao mzigo.

Walilalamika kuwa nao wanataka haki sawa na wafanywakazi wa lisirikali linalopunja wazalishaji wake kiasi cha kutaka waongezewe mshiko huko nalo likiwatishia kuwafuta kazi.

Hivyo walikuja na hoja ya kutaka nipunguze makamuzi ili bei ya kahawa ishuke. Walisema nisipofanya hivyo ama wagome kunywa kahawa au kutonichagua kwenye msimu wa uongo ujao.

Baada ya kuona walevi wamedhamiria kufanya kweli, niliitisha kikao maalumu cha walevi wakongwe na kumwaga nyodo nisijue nakula chambo!

Niliwapaka ile mbaya kulaleki! Kutokana na wakongwe wale kupewa kahawa na kashata za bure walikuwa wakitikisa vichwa kuunga mkono kila tusi na kashfa nilivyorusha.

Wengi waliwashangaa wakongwe hawa kutokana na kuishi bila kunywa kahawa kutokana na kutoimudu. Maskini kumbe mtu mzima anaweza kuwa hovyo! Maskini hawakujua duniani hakuna vya dezo na kama vipo vinaponza! Bila wao unadhani aibu yangu angeificha nani? Maskini hawakujua mie ni Lugard wa kisasa ambaye bila gawanya utawale hana mashiko!

Sikuwakawiza. Nilitema cheche kuwa atakayeendelea na upuuzi huu wa kudai visivyodaiwa nitakwenda kaya jirani nilete walevi wengine nione kama nao watakunywa na kula jeuri yao.

Hata hivyo ukweli ni kwamba nilikuwa nawafunga kamba. Kama wangefanya kweli manonihino yangenitoka kusema ule ukweli.

Kutokana na ulevi wa ulabu na madaraka nilio nao, nilimwaga nyodo utadhani siku ya siku nitajichagua mwenyewe au kura ya shortie wangu ndiyo itaamua!

Sasa yameishanifika. Niko nahaha kuwaweka sawa walevi wasinitose nikaumbuka. Kuna wakati nafikiri kukubaliana na madai yao. Lakini hata hivyo nachelea kukonda na kufa kutokana na kukosa makamuzi.

Mie naweza. Je, huyu bi mkubwa aliyezoea matanuzi atakubali? Maana nshamzoesha makamuzi kwenda mbele.

Pia nachelea mtu mwingine kuja na kufichua maulaji na mambo yangu. Hapa lazima ieleweke.

Siku nikiacha ukuu lazima nimuweke kibaraka wangu atakayenikingia. Upo hapo mwanangu? Siku hizi kutesa kwa zamu. Leo upo. Kesho historia hata mazonge. Maana avumaye baharini papa.

Hakuna aliyenikera kama mchunguliaji kuja na orodha ya makamuzi yangu na kuiweka hadharani wakati ilipaswa kuwa Top Secret. Kilichonisaidia ni kuweli kuwa walevi huwa hawatunzi na hawana kumbukumbu. Vinginevyo ningeumia.

Nichukue fursa hii kuonya: msipoangalia njaa na matumbo yenu mtaliwa mnaona. Mtatumiwa kama mitondoo kule lupango. Unajua kazi ya mtondoo? Tuyaache.

Kwa vile najua walevi wa kahawa hawana ubavu dhidi ya walevi wa madaraka, nitafanya fanya majamboz niukwae tena watake wasitake. Kwa muda uliosalia najua watasahau.

Siku ile ikifika wanachukua wanaweka waa nami naambua ushindi wa kishindo kama mibomu ya Mbalaga.

Nani amewajibishwa au kujiwajibisha baada ya mibomu kudedisha wana kaya bila hatia?

Watu ndiyo wanazidi kukamua wakikamia kuukwaa na kukamua zaidi. Kwanini wao waweze mie nishindwe?

Walevi walishangaa nilipopata ujasiri wa kuwazodoa na kuwaita majina ya ajabu ajabu kutokana na kutaka kuingilia ulaji wangu. Kwanza, niliwapa live kuwa ni wanafiki na waongo wanaodai natumia sana.

Hivi kwa ukuu wangu walitaka nitumie kama chokora au matonya? Mie natumia kama Mobutu na mke wangu anakamua kama Imelda Marcos au Gucci Grace Mugab wa Zimba za mabwe. Hapa wa kulaumu si mimi bali woga na ujinga wao. Kwani waone mara ngapi kujua mie sina mpango nao ili waamue waamuavyo?

Lazima nikiri. Siku ile sikuwa na roho mtakatifu bali mtakakitu aliyesukumwa na roho ya mwendawazimu kunena makufuru niliyonena.

Niliwapasha kuwa mie sitegemei kura za walevi kuendelea na ufalme wangu wa makamuzi. Nilisema wazi sihitaji kula ya mtu ila wajue nitaendelea kula watake wasitake.

Hata hivyo kiroho kinanisuta. Je, ni kweli sihitaji kura zao? Kupayuka kwingine ni ugonjwa utokanao na kichwa kukosa mawasiliano na mdomo.

Ngoja nijikate nikaaandae mikakati ya kuwaingiza mkenge walevi.

Naona wale wanaotukuta wanakuja. Acha nikitoa wasijeninyotoa roho.
Chanzo: Tanzania Daima Mei 19, 2010.

No comments: