The Chant of Savant

Friday 2 July 2010

Long live my kingdom


Mwezi Juni unaingia kwenye vitabu vya kumbukumbu ya himaya ya walevi kuwa ndio wakati uliposimikwa utawala wangu mfalme mkuu wa walevi almaarufu mfalme Mpayukaji Jackal Kimwemwe I ambao wabaya wangu huuita ufisi yaani Ufisadi Siasa-fisidi na Usanii ingawa siyo.

Kuhakikisha ufalme wangu unadumu milele, nimewateua waramba viatu wangu na wanafamilia kuusimamia na kuusimika katika mioyo ya walevi ambao wananipenda kuliko wanavyojipenda.

Wengi wasiojua siri ya maulaji wamenilaumu kuwa nawachelewesha kwenye himaya na neema niliyowaahidi walevi zama zile! Waarabu wana msemo: “ Kul takhira fi’ khira yaani wakati mwingine bora kuchelewa kuliko kuwahi. Hata waswahili wamesema: Pole pole ndiyo mwendo na haraka haraka haina baraka ingawa ngoja ngoja nayo huumiza matumbo. Tuchague lipi? Mtajijeijei na kiherehere chenu. Mkilizwa mnalalamika wakati ni kiherehere chenu na kutaka takrima na kitochi. Sasa mnataka mimi niwafanyeje yarabi?

Mliambiwa mali mnayo lakini mnaikalia. Akili mnazo lakini hamzitumii badala yake mnatumia matumbo na njaa!

Kuhakikisha ujiko na usalama wa ulaji wangu haviguswi, nimemteua kifungua mimba wangu aitwaye Rizikiwani kufungua usanii kwa kuhakikisha naungwa mkono na wanyama, wadudu, mimea, mbingu, bahari, magari na walevi.

Najua walevi wapenda sifa watachangamkia tenda ya kuniunga mkono kwenye vijiwe vyote wakijisifu kuwa wamenidhamini wakati mdhamini wangu mkuu ni pesa na wenye nazo tu.

Ingawa juzi baiskeli ziligoma kunibeba, lazima kila kitu kitii ufalme huu uliotoka kwa Mungu.

Juzi tu alijitokeza bazazi mmoja kutaka ufalme uangushwe na kila mtu aruhusiwe kugombea kuwa kiongozi wa walevi.

Nilimuita mteule wangu mkuu wa makuhani na kumwambia nisisikie upuuzi huu. Japo mimi si mzee wa makuhani wala msomi wa torati, nilimuagiza ahakikishe shauri hili linakufa haraka. Alifanya kweli na kuutangazia umma kuwa ufalme utadumu milele. Sababu? Kwanza, angegomaje wakati nilimteua kwa kumpendelea kutokana naye kutokuwa na udhu wa kuwa mkuu wa mkuhani kama yule mkuu wa usajili wa timu za kupingana Joni Tenda.

Naitangazia dunia kuwa kila kitu kimetiishwa chini yangu. Si wakuu wa makuhani, waandishi, mafarisayo hata kina Zakayo, masadukayo wala watoza ushuru. Masadukayo wameishaonyesha vitu vyao kwa kunichangia maelfu na ndururu kwa ajili ya kusimika ufalme huku waandishi wakiimba sifa zangu na wazee wa makuhani wakipitisha amri zangu bila kujali mie si msomi wa torati.

Hamkusoma katika Marko 12:43,44 juu ya yule mwanamke maskini aliyotoa senti mbili na kuhesabiwa haki? Mie sihesabii maskini haki bali wenye nazo ambao lazima wanichangie kuimarisha ufalme wangu. Wabaya wangu wanasema nitaishi na kuisha kama Nabkadnezza! Niishi na kuisha mara ngapi zaidi ya wao ninaowabebesha mizigo kama vihongwe?


Pili, wanaotaka kubatilisha ufalme na kuleta jamhuri hawana sura nzuri- yaani they are not beautiful enough to become king even president like me -the most beautiful one and the choice of God.

Tatu, hawana fweza za kuwanywesha walevi kwa kuwapa kitochi na kuonyesha ukarimu wao kupitia takrima.

Nne, wao si chaguo la walevi wala hawapendwi na watu kama mimi kiasi cha watu kunichangia wakati nakwanyua kila uchao mimi bi Nkubwa na wenzangu. Kama alivyowahi kusema chizi mmoja baada ya kulewa maulaji kuwa walevi wanaweza kula majani lakini lazima mkuu apate pipa atanue na shortie wake.

Juzi nilicheka niliposikia kuwa wakati watu wanamchangia jamaa yeye anapaka ikuu nkorogo ukiachi ambali kuahidi milaputopu wakati ukweli ni kwamba kwenye ilmu zilishaibiwa bilioni 150! Upo hapo mshrika? Hii usimwambie mtu kuepuka idadi ya wanaojinyonga kuongezeka kutokana na hili. Nichangieni mie mfalme asiye na makuu.

Tano, hawana ahadi nzuri za kuwazingua na kuwachengua walevi. Hawana lugha tamu ya kuwaahidi Kanani pepo na vinono vingine hata vikigeuka kuwa shubiri kwao.

Sita, hawajasomea sanaa wala hawajui kutumbuiza kwa mipasho yenye kupumbaza kama mimi.

One thing must be noted. Naongea kizungu mjue nimebukua hata kama ni kamba. Baada ya mama mmoja toka huko milima ya Pale kuja na mpya kuwa ukintongoza mwannke usintukane, nimejifunza toka kwake. Ukitaka kuibia wale lazima uwatongoze kwa kuwaahidi kila vinono hata kama unajua huna sera na mwisho wa yote wataishia kusaga meno. Mie nimeahidi spiidi zaidi, Mori zaidi na power zaidi ya kuhomola.

Niliwaahidi walevi majembe ili walime kahawa na kuwa mabilionea nikachemsha. Kwa vile wanapenda kutongozwa na kupumbazwa, kipindi hiki nawaahidi kompyuta kila mlevi na GPS ili nikiwa natanua ajue niko mitaa gani kule majuu ili waje tutanue pamoja, je hii inawezekana? Tia akilini.


Sitanii. Kwa vile nina mpango wa kumrithisha mwanangu ufalme wangu, kipindi hiki nitatanua sana kwani ni lala salama ya ufalme wangu. Wale wanaonikamia kuwa watanitoa nohino nikishamaliza ngwe yangu ya mwisho wamenoa. Hawajui kuwa nitahakikisha mrithi wangu anakuwa mtu wangu kama si mwanangu kiasi cha kunilinda kama nilivyowalinda akina MbwaMwitu na Kanji Roast tamu na wengine kama Tunituni na ukoo wake?

Anayebisha aangalie nilivyomtupa nje ami Mpemba kwa kumwamuru agombee ukuu wa kijiwe kule ng’ambo ili kwa msimamo wake wasijempendekeza arithi kiti changu baada ya kung‘atuka. Unadhani usanii wangu wa leo tu? Shauri yako.

Zama zile nikikwea kiti cha ufalme huu niliwakamata walevi kwa ahadi ambazo ziliishia kuwa sanaa. Sasa nimebadili mbinu. Nataka nitawale kwa ndoto. Nina ndoto kubwa hata kama wapinzani wangu wanaziita za mchana. Nataka walevi wote waendeshe VX na kupanda ndege kama mimi na bi nkubwa na watoto wetu ukiachia mbali waramba viatu wangu.
Nataka vitegemezi vya walevi viishi kama watoto wangu kwa kila kitu. Lazima visome kwenye shule za bei mbaya zinazotumia si kompyuta tu bali lapu topu.

Kwa ufupi ngwe hii ni ya kwenda Kanani kwa vitendo sitanii.

Nhh! Mbona yule ni kama ndata! Acha nijikate wasije na viherehere vyao wakanikata mitama.
Hata hivyo, ngoja nipayuke kabla hawajanitia mikononi. Long live my corruption sorry kingdom.
Chanzo: Tanzania Daima Juni 30, 2010.

No comments: