The Chant of Savant

Friday 2 July 2010

Tunataka uwajibikaji si wingi wa mikoa ya kulipana fadhila

Baada ya serikali ya rais Jakaya Kikwete kujiingiza kwenye kashfa tele ambazo zimeligharimu taifa wengi walidhani angalau angestuka.

Hata baada ya serikali ya Kikwete kuwa zigo tokana na kutapanya mali na pesa ya umma wengi walidhani angestuka.
Hata pale wafadhili walipoamua kuiminya serikali ya Kikwete kifedha ili ipambane na ufisadi vilivyo badala ya kuushabikia na kuukingia kifua wengi walidhani angestuka.

Nani amesahau kuwa ripoti ya mkaguzi wa mahesabu ya serikali kila mwaka hufichua matumizi mabaya kwenye karibu wizara na serikali zote za wilaya?

Nani haoni kuwa hali hizi zinasababisha maisha magumu kwa umma ulioahidiwa kupelekwa peponi Kanani ukaishia kwenye mazonge?

Kutokana na upogo na upofu huu wachambuzi wengi walimlingansiha Kikwete na bwana Ziro ambaye siwezi kumtaja kwa vile anafahamika na alivyovurunda, kama alivyokuja kukiri mwenyewe.

Hii inanikumbusha kisa cha ndege mmoja mpumbavu ambaye baada ya kumeza punje moja ya hindi alighafirika na kumeza nyingine. Ndege huyu mpumbavu aliishia kukwamwa na punje na kupasukilia mbali huku mbegu zile zikimgeuza mbolea.

Wengi wanashangaa. Wameshangaa mantiki ya Kikwete kuanzisha mikoa mipya mitatu wakati ile ya zamani inamshinda kutokana na mzigo wa kiutawala. Kwanini sasa kuelekea uchaguzi na si alipoingia madarakani? Jibu liko wazi kuwa hiki ni kishawishi wananchi wanaoangukia kwenye mikoa mipya. Hii ni hoja hata sera kwa waramba viatu wa Kikwete kuwahadaa wananchi kuwa “mnaona Kikwete kaanzisha mikoa wilaya na tarafa mpya ili kuleta huduma karibu.” Kwanini hakuianzisha wakati anaanza tukaona ambavyo angeihudumia? Wajinga wengi watasema tumpe kura Kikwete ili akamilishe mema aliyoanzisha. Rais hakuchaguliwa kutenda mema bali kutekeleza ahadi sera na katiba vilivyomuingiza madarakani finish.

Kwa Tanzania kuwa na kata, tarafa, wilaya hata mikoa haisaidii chochote kama watawala wanaposema kuwa wanafanya hivyo kuleta karibu huduma. Kuna huduma gani zaidi ya umaskini wa kutengenezwa na wajinga wachache wenye mamlaka?

Katika kuelekea uchaguzi, leo tuna mikoa mipya mitatu yaani Njeruma, Geita na Simiyu. Wengi wanahoji mantiki ya ufinyangwaji wake ukiachia hata majina yake. Tuna wilaya mpya kadhalika. Hizi ni Mulele Gairo, Nyasa, Chemba, Ikungi, Mkalama, Mbogwe, Nyang’wale, Buhingwe, Kakonko na Ushetu!
Hata majina yenyewe yanatia shaka achilia mbali kinyaa. Kwanini Njeruma si Mkwawa hata Mnyigumba? Kwanini Geita na si Ziwa au Simiyu na si Bariadi hata Nguliati kwa wanaojua historia ya mkoa huu?

Hapa tunaongelea ulaji kwa Kikwete (kura) na ajira (kulipa fadhila) kwa marafiki wa Kikwete ukiachia mbali majisifu yasiyo na maana. Hujaongelea shilingi zaidi ya bilioni 150 zinazodaiwa kwenye sekta ya elimu mwaka 2008. Si Kikwete wala mawaziri wake wanataka hili lijulikane wala kujadiliwa. Pesa inaibiwa wewe unapanua serikali badala ya kuipunguza ili usimamie vizuri. Uchumi gani huu?

Usishangae kusikia baadhi ya makanjanja na walamba viatu wengine wakipewa ukuu wa wilaya hata mkoa na ubaki kuishia kupigwa na butwaa. Maana kwenye balozi zetu nje nafasi zimejaa ukiachia mbali kwenye bodi za mashirika na ulaji mwingine wa kulipana fadhila.
Leo tuna wakuu wa wilaya hata wabunge waliokuwa wauza maandazi na hakuna anayeuliza walivyofika hapo ukiachia mbali vihiyo wengine kwenye taaluma nyingine hata sheria.

Wengi hasa wachumi wanaoona madudu ya serikali ya Kikwete walidhani: kuondokana na matumizi makubwa yasiyoshabihiana na mapato, Kikwete angepunguza serikali yake badala ya kuipanua. Kwa vile mifumo na siasa zetu ni kwa ajili ya kundi dogo la watawala kujihudumia, Kikwete, washauri na maswahiba zake hawakujihangaisha kuuliza nani atagharimia mzigo huu. Watahangaishwa na nini wakati punda kihongwe (mlipa kodi maskini) yupo na halalamiki?

Je ni vigezo gani vimetumika kufinyanga hii mikoa na wilaya zaidi ya ushikaji kisiasa? Sijui kama hata huo mkoa mpya wa Njaruma ni mkubwa kuliko wilaya ya Kahama. Kesho tutaamiwa. Bagamoyo hata Chalinze ni mikoa! Kweli namna hii tutasonga mbele au nyuma? I have no idea.

Benjamin Mkapa ambaye waliokata tamaa wanaanza kumkumbuka alishambuliwa alipogawa mkoa wa rafiki na mtendaji wake mkuu Fredrick Sumaye kuwa mkoa kwa sababu alizojua. Leo “chaguo la Mungu sijui sheta…” naomba nisimalizie, ameamua kuonyesha maneno uchumi na umma yasivyo kwenye kichwa chake sijui tutafanya nini? Je sisi si mateka wa kiumbe tuliyemtengeneza kama jini na kumtoa kwenye chupa akaanza kuturudi?

Je hapa wa kulaumiwa nani kati ya makuli wabeba mzigo na bwana mkubwa mbebeshaji watu mizigo yake? Mmeonya si mara moja wala mbili kuwa mna muung mtu kwenye ofisi yenu kuu lakini mwamgwaya kiasi cha kuwatoa kafara kwa faida zake na marafiki zake mkiona na msifanye kitu? Katika kitabu changu cha Saa ya Ukombozi nilidurusu hali kama hii kwenye nchi ya Mizengwe ambapo umma uliamka na kuondoa kadhia bila kuchelea patilizi na maangamizi. Je nyie mko tayari? Kazi kwenu. Mnata mitume waje na waseme mara ngapi mkengeuke na kuchukua hatua achia mbali kuamini?

Ukionja nyama ya mtu huishia kwenye urahibu. Kikwete alipanua serikali yake na hakupata misukosuko. Sasa anazidi kupanua zaidi wakati dhiki zikipanuka zaidi. Je tufanyeje? Jibu mnalo waathirika wakuu.
Chanzo: Tanzania Daima Juni 30, 2010.

No comments: