The Chant of Savant

Wednesday 18 August 2010

TAKUKURU imepata wapi makali haya?





JAPO wengi wanaoshabikia mkumbo wa mambo baada ya kuchoshwa na ufisadi kwa muda mrefu wameipongeza Tume ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (TAKUKURU) kwa kugusa wasioguswa na vigogo wa chama jogoo, mie simo kwenye kundi hili.

Japo wengi wamefurahi angalau kuona mawaziri, wakuu wa wilaya na wakuu wengine wastaafu kufikishwa mahakamani kwa madai ya kutoa rushwa kwenye kura za maoni za Chama Cha Mapinduzi (CCM) zilizopita na kusifika kwa kughubikwa na rushwa, bado hairidhishi wala kustahiki kwa TAKUKURU kupongezwa.

Kwa wanaojua uhasama na uroho wa madaraka uliopo baina ya mitandao ya ndani ya CCM, wataungana nami kuhoji- TAKURURU kama kweli ina meno kama inavyotaka tuamaini, ilikuwa wapi ziliporipotiwa rushwa kubwa kama vile Buzwagi, Ununuzi wa rada na ndege ya Rais kwa uchache?

Kwanini waliokamatwa kipindi hiki hatuwaoni wale magwiji wa kwenye kashfa tajwa hapo juu? Kwanini TAKUKURU hii hii haijawahi hata kuchunguza wapi zilipokwenda pesa za ujambazi wa EPA ambazo tunaambiwa ndizo zilimwingiza Rais Jakaya Kikwete madarakani kama ilivyowahi kudaiwa na CHADEMA na wana mageuzi wengine?

Kwa nini TAKUKURU hii haijawahi kuchunguza baadhi ya ajira na vyeo ndani ya serikali ya CCM? Je, inao ubavu wa kuweza kufanya hivi?

Kwa wanaojua jinsi TAKUKURU ilivyovuliwa nguo wakati wa kutaka kutumika kuua kashfa iliyomng'oa waziri mkuu wa zamani Edward Lowassa, wana wasi wasi na hawa waliodaiwa kukamatwa na TAKUKURU-jibwa la rais lisilo na meno hata mawili.

Tuzidi kujiuliza. TAKUKURU imepata wapi haya makali ya sasa kama siyo kuagizwa na bosi wake kuwapatiliza na kuwakomesha wabaya wake ambao kimsingi waliusumbua utawala wake?

Kwanini TAKUKURU kama kweli inataka kupambana na rushwa, haijachunguza kukusanywa kwa shilingi bilioni 50 kwa ajili ya kumwezesha rais Kikwete kushinda?

Hivi TAKUKURU wanadhani watu wote ni mataahira siyo? Ni miradi mingapi hasa ya ujenzi wa barabara na tenda ina kila harufu ya rushwa na wakubwa zake wanapeta?

Hebu tuipe eneo mojawapo linalonuka na kuishinda hata serikali kulishughulikia kutokana na kuwa na mtu wake. Hili si jingine ni Tanroads. Muulize kila mtanzania anayefuatilia mambo. Anajua fika jinsi mkurugenzi wa sasa wa mamlaka tajwa alivyo serikalini ndani ya serikali.

Hapa hujaenda kwenye mbuga za wanyama ambapo maeneo ya uwindaji yanatolewa kwa rushwa mchana. Bado hujaenda bandarini na mipakani ambapo karibu kila kitengo kinatolewa kwa wahusika kulingana na uzito na kipato cha kitengo kwa upendeleo na rushwa.

Hebu tuchunguzane nani yuko wapi na aliingiaje hasa maeneo yenye ulaji mkubwa. Mbona TAKUKURU haijachunguza ajira za watoto wa vigogo waliojazana BoT?

Bahati mbaya sana, hata mashirika yanayofanya utafiti hayataki kufanya utafiti huku zaidi ya kujikita kwenye siasa kwa vile ni rahisi kupewa chochote kitu na kuja na matokeo ya kumjenga fulani. Nendeni huko muone nchi ilivyooza huku TAKUKURU ikiwa usingizini.

Kuna hili la rushwa ya wengine pasipo na kugusa rushwa yake. Ukichunguza mishahara ya wafanyakazi wa TAKUKURU na aina ya maisha wanayoishi ni vitu viwili tofauti.

Kama alivyodai mkuu mmoja wa Polisi, TAKUKURU nao wanakula rushwa hata kama hakuna wa kuwakamata. Hii inanikumbusha kisa kimoja kilichonitokea Tabora mwaka 1993.

Nikiwa safarini kuelekea Kigali Rwanda nilikamatwa na afisa mkusanya kodi njiani. Kosa langu ni gari langu kupakia mwanamke aliyekuwa anakwenda msibani ambaye hakuwa amelipa kodi.

Kutokana na kugundua ujuha wa ofisa mkusanya kodi aliyetaka nimlipie abiria wangu kodi ndipo aruhusiwe kuendelea na safari yake kwenda matangani, nilimtaka mhusika anipe karatasi yake ya kodi.

Ajabu ya maajabu niligundua kuwa kumbe naye alikuwa hana hiyo karatasi kutokana na ukweli kuwa hakuna ambaye angemkamata kutolipa kodi kutokana naye kuwa ndiye mkamataji wa wakwepa kodi.

Kadhalika na TAKUKURU inapaswa kuundiwa chombo cha kuichunguza. Tusiiamini TAKUKURU ambayo haiaminiki wala haituamini. Tufikie mahali tujenge vitengo vyenye kufuata kanuni za kijasusi vyenye kuchunguzana ili kutenda haki na kuleta uwajibikaji.

Kwa nini jeshi letu la Polisi lisipewe jukumu la kuichunguza TAKUKURU ili muone uoza wake?

Kwa kuwa chini ya ofisi ya rais, licha ya TAKUKURU kuweza kutumiwa kisiasa kama inavyoonyesha kwenye kuingilia mchakato wa kisiasa wa chama, inaonekana kama mwana mtukufu sawa na bosi wake.

Je, TAKUKURU haiajiri wanadamu hasa watanzania ambao wamebobea kwa rushwa kutokana na mfumo wetu kuwa wa kirushwa?

Mbona TAKUKURU haikamati wezi wakubwa waliojazana kwenye mamlaka ya kodi wanaojulikana kwa ukwasi wa kutisha kuliko hata hao mawaziri?

Kazi ya umma haina cha kuaminiana iwe kwa mtu binafsi au taasisi. Yeyote anaweza kutenda kosa. Ndiyo maana nchi zilizoendelea huwa na mashirika mbali mbali yasiyojuana yanayochunguzana ili kuleta ufanisi uliokusudiwa.

Kwa TAKUKURU kuingilia kura za maoni za CCM ni ushahidi kuwa inatumiwa na CCM. Na hapa vyama vya upinzani vikae chonjo. Hii inaweza kuwa ni gia ya kutaka kuwahujumu wagombea wa upinzani ambao ni tishio kwa CCM.

Na hapa ndipo CCM itaua ndege wawili kwa jiwe moja kuwabana viherehere wa ndani na wapinzani hatari kwa mustakabali wake.

Kama rais wetu ni msafi na anayefuata utawala wa sheria, hana haja ya kuweka mamlaka muhimu kama haya chini ya ofisi yake. Anaiweka chini yake ili aifanye nini zaidi ya kuitumia kwa maslahi yake binafsi? Tuulize swali jingine kuu. Kuna wengi tunaolalamikia utendaji wa mashirika yasiyo ya kiserikali ya wake za marais yaani Anna Mkapa na Salma Kikwete ambayo yanaonyesha wazi yalivyo ya ulaji kupitia mgongo wa Ikulu. Mbona TAKUKURU haiendi huko kuchunguza?

Kuna madai mengi ya tabaka dogo la watu tena wageni kumiliki uchumi wa taifa. Ni hawa hawa wanaotajwa kwenye karibu kashfa zote kubwa zinazobomoa uchumi wetu.

Nani anawagusa kutokana na wao kuwa karibu na wakubwa wa serikali wakidhamini mbio zao kuingia madarakani? Wengine wamefikia hata kuwaweka watoto wao kwenye ubunge ili kulinda maslahi yao na TAKUKURU haifanyi kitu.

Ni wabunge wangapi tunao wametokana na utajiri ama wa wazazi wao au jamii zao wasio na hata chembe moja ya mshipa wa siasa?

Kama kuna Taasisi inayoweza kubebeshwa zigo la kulinda rushwa si nyingine bali TAKUKURU ikishirikiana na ofisi ya rais. Ni afadhali kirefu cha TAKUKURU kuwa Taasisi ya Kuzua na Kupamba na Rushwa kuliko ilivyo.

Tukitaka kupambana na rushwa hasa hii inayowahusu wakubwa wetu, tuisuke upya na kuiondoa TAKUKURU chini ya ofisi ya rais. Na tusikubali kuchafuliwa kama inavyofanyiwa sasa kwa kutumiwa kwenye siasa chafu za CCM.

Ningekuwa mkuu wa TAKUKURU, kwa kujua taasisi yangu inavyoonekana yao hovyo na kutumiwa hovyo, ningeachia ngazi na kutafuta kazi nyingine ya heshima.
Chanzo: Tanzania Daima Agosti 18, 2010.

2 comments:

Maisara Wastara said...

Nami nilijiuliza sana swali hilo...

Anonymous said...

Hii ndiyo aina ya uandishi tunayotaka. Hakuna haja ya kuogopa kuibua maswali na kuamsha ushawishi na udadisi. Hongera mkuu.
Kikwete si mzima hata wapambe wake wakituaminsha hivyo.