The Chant of Savant

Monday 16 August 2010

Wanaotaka mdaharo na Kikwete hawamtakii mema


Ingawa wengi wamekilaumu Chama Cha Mapinduzi (CCM) kutoridhia mgombea wake Jakaya Kikwete kushiriki mdaharo wa wagombea urais kama ilivyotakiwa na mgombea wa CHADEMA Dk. Wilbrod Slaa, kuna haja ya kuangalia historia na ukweli.

Nani mara hii amesahau kuwa Kikwete huyu huyu aliyetuonyesha uhalisia wake kwenye ngwe inayoisha alikacha mdaharo mwaka 2005 akiwekeza kwenye ushabiki kibubusa wa watanzania wakati ule baada ya kuuchoka ukale na ubabe wa Mkapa? Sababu? Aseme nini iwapo kila kitu ki wazi? Mtangulizi wake Benjamin Mkapa mwana tasnia ya uandishi wa habari na mahusiano ya kimataifa alipenda sana midaharo na kuimudu. Hapa lazima ukumbuke vitu viwili-taaluma na uwezo binafsi wa mhusika.

Kumbuka. Wakati Mkapa akiingia madarakani tulikuwa hatuna cha kumuuliza kutokana na sababu kuu mbili. Kwanza alikuwa akiashiria mpito toka chama kimoja kwenda vyama vingi. Hapa euphoria niseme kihoro, vilikuwa vimetawala.

Pili Mkapa licha ya kuwa msemaji na msomi aliyebobea, alikuwa ameungwa mkono na gwiji na kipenzi cha watanzania , hayati Mwl. Julius Kambarage Nyerere ukiachia mbali kuwa hakuwa akijulikana vilivyo. Lakini pamoja na mapungufu yote haya Mkapa hakuukacha mdaharo kutokana na kujiamini na usomi wake ambao unakubalika licha ya mapungufu aliyoonyesha kwenye utawala wake.

Pia Mkapa hata Mwalimu, alijua umuhimu wa midaharo hasa katika kujenga taswira ya mhusika na kutoa kile anachotarajiwa kufanya. Mkapa pamoja na mapungufu yake, hakuwa mtupu wala mweupe.

Je ni kwanini CCM na Kikwete hawataki kushiriki mdaharo? Hivi mnategemea Kikwete kweli afue dafu mbele ya wasomi kama Dk. Slaa na profesa Ibrahim Lipumba ukiachia mbali Dk. PAul Kyara? Kwanza, ana nini jipya la kuwambia watanzania iwapo wanamjua nje ndani-urahimu na masihara yaandamanayo na kucheka cheka hata wakati wa mambo yanayohitaji kununa? Kimsingi saizi ya Kikwete ni watu kama Augustine Mrema na wengine aina yake lakini si Slaa wala Lipumba.

Hivi mlitaka Kikwete achukue kitanzi na kuweka shingo lake? Kwani hamjui kuwa kashfa ya hivi karibuni iliyoripotiwa-si na wapinzani, bali shirika la umoja wa mataifa ya shilingi trilioni 1.7 ni pigo la mwisho kwa Kikwete kama wapiga kura na watanzania wangekuwa wanajali uongozi bora na uwajibikaji?

Tujalie Kikwete ashiriki mdaharo huru halafu aulizwe sababu za kutotaja mali zake kama sheria anayopaswa kusimamia inavyotaka. Mnategemea atajibu nini zaidi ya kujikaanga.

Hapa hujagusia kashfa inayosemekana kuundwa ili kumpatia mtaji wa kuingilia madarakani ya EPA. Hapa bado hujagusa watu wake kama vile mkewe ambaye anadaiwa kuunda NGO ya kuchumia utajiri baada ya Kikwete kuapishwa. Hapa hujagusa tuhuma kuwa mwanawe anautumia Umoja wa Vijana wa CCM- UVCCM kujinufaisha pamoja na utawala wa baba yake. Bado hujaongelea maswahiba zake wa karibu kuhusika na kashfa mbali mbali zilizoligharimu taifa mabilioni ya shilingi kiasi cha kuzidi kuwafanya watanzania maskini zaidi na zaidi.

Hujagusia shutuma za usanii yaani kuahidi hiki na kutotekeleza. Yako wapi maisha bora kwa watanzania wote ukiachia mbali walio karibu na kiti cha ulaji?

Bado hujagusia rushwa na migongano ya mitandao ndani ya chama. Hii ni mbali na kipaji na elimu ya mhusika japo tuliwahi kuaminishwa na wasaka ulaji kuwa ni chaguo la Mungu wakati si kweli.

Wanaotaka Kikwete ashiriki mdaharo uwe mdogo hata mkubwa hawamtakii mema. Wanamkejeli na kumshakizia auingie moto. Maana ataulizwa maswali ambayo yatamuacha bila nguo.

Hivi mnategemea nini toka kwa mtu anayeamini kuwa msongamano wa magari barabarani ni ishara za maisha bora wakati ni ushahidi wa ombwe la uongozi na mipango madhubuti?

Je mnategemea aseme nini mtu ambaye amekuwa akiongopa kila uchao? Rejea kuwahi kusema kuwa ana orodha ya kila wahalifu.

Kikwete na washauri wake wanajua kuwa kuna maswali na masuala mengi mazito ambayo hawezi kuyatolea majibu yenye mashiko. Hivyo kumuepusha na aibu na pigo wanashikilia kuwa mgombea hawezi kupimwa kwa mdaharo. Na hakika. Wanajua ni kwa kiasi gani wanaongopa na kujiongopea. Maana hata hao wanaodhamini chaguzi zao yaani nchi tajiri huwapima wagombea wao kwa njia hii muafaka na ya kisayansi. Kwa maana nyingine rahisi ni kwamba Kikwete hana cha kuwafanyia na kuwambia wapiga kura zaidi ya mazoea na ukale hasa ikizingatiwa kuwa CCM imekuwa ikikabiliwa na ombwe la uongozi jambo ambalo hawajawahi kukanusha kumaanisha kuwa ni kweli. Na hakika. Kukacha mdaharo ni sehemu mojawapo ya ombwe.

Kimsingi, wapiga kura na watanzania waogope na kujitenga na mgombea anayeongopa kueleza mawazo na mipango yake. Kikwete kwa hili hasingiziwi kuwa hakutimiza ahadi zake. Nitajie ahadi lau moja aliyotekeleza katika makumi aliyoahidi. Hakuna zaidi ya siasa na sanaa kama kawaida. Kikwete amethibitisha kuendeshwa na matukio yanayolenga kuahirisha lakini si kutatua tatizo. Jana aliahidi hiki asitekeleze. Na usishangae kumsikia leo akiahidi kile ambacho kadhali hana mpango wa kutekeleza. Ameshindwa kufanya maamuzi magumu kama alivyowahi kupewa ushauri wa bure na wazee wa chama chake aliowaita wafitini waongo na wenye wivu.

Kama Kikwete ameshindwa kutekeleza ahadi zake na kutobadilika kwa miaka mitano iliyopita, mnategemea ni miujiza gani itafanyika aweza kuiona nuru-to deliver?

Hakuna haja ya kuandika mate ilhali wino upo. Utendaji dhaifu wa Kikwete kwenye awamu iliyopita ni ushahidi tosha kwa hukumu yake-kutochaguliwa kama wapiga kura watakuwa makini na kujua kuitumia silaha yao yaani kura.

Hivyo tufupishe kwa kusisitiza kuwa kumtaka Kikwete ashiriki mdaharo ni kumpa kitanzi ajimalize ingawa ameishakwisha kama tutatumia busara na kuangalia rekodi zake binafsi, waliomzunguka na utawala wake kwa ujumla.

Nashauri mdaharo ufanyike hata kama Kikwete hatashiriki kutokana na mapungufu niliyotaja hapo juu ili umma ujionee wenyewe mbivu na mbichi pumba na nafaka.
Chanzo: Dira ya Mtanzania Agosti 16, 2010.

No comments: