The Chant of Savant

Thursday 9 September 2010

Sera yangu ni ufisadi kwanza

NATOA tahadhari. Jakaya Kikwete na Dk. Wilbrod Slaa jiandaeni mgombea makini nakuja. Sina shaka. Msimu huu tutagawana kura mtake msitake. Wakati sera ya Kikwete na CCM yake ni Kilimo Kwanza, mie natoka na kitu Ufisadi Kwanza. Yeye anaendesha CCM nami nimeanzisha FACCM yaani Fight against a Cabal of Criminal Mafia.

Hii ni baada ya kugundua kuwa wakulima na wafanyakazi wanapozalisha, mazao yao yanaliwa na mafisadi. Hivyo kuliondoa tatizo hili nakuja na Ufisadi Kwanza.

Mkinichagua jueni. Nitawakamata mafisadi wote wawe na madaraka au wastaafu mie nafyeka tu na makazi yao ni lupango niaminini. Mie sina mshiko wa kuhonga kwani ni kinyume cha sheria na dhambi.

Pia sitaahidi kupandisha mishahara wakati huu wa kampeni. Kwani kufanya hivyo, hata kama tutajifanya kujirusha kimanga, ni rushwa ya wazi. Unaahidije kupandisha mishahara wakati huna mamlaka hadi uchaguliwe? Kwa wale waliomaliza muda wao, kwanini hawakufanya hivyo wakati wakiwa madarakani? Si ni hawa hawa waliowaambia wafanywakazi kuwa hawataki kula yao? Leo watu wazima wanakuja na upuuzi wa kitoto wa eeh unajua sikueleweka vizuri, unajua dokta Silaha ndiye anapinga kupandishwa mishahara wafanyakazi. Jamani, tufanye vitu kiakili na kisheria na si kitaahira kisanii na kipuuzi. Hili mkinichagua litabaki historia.

Nimeanzisha Chama cha Mafisadi si kwa maana ya kumilkiwa na mafisadi kama kile cha mafisadi bali kupamaba nao. Chama changu ni sawa na 'jeshi la wananchi' ambalo huwabonda hao hao wanapoliboa na kuendelea kuitwa la wananchi. Usiniulize maana ya hii ni nini. Sitaki matatizo mie ati.

Nasema mwaka huu uchaguzi utakuwa mtamu kutokana na kuingia kwa kidume mie kwa sababu zifuatazo.

Mosi, nimepima afya yangu na kuambiwa ni fit kichizi kiasi cha kuweza kuhimili mikiki mikiki ya kampeni na utawala bila kuanguka. Ili kujua nilivyo fit, nimepima kwenye hospitali za kawaida na kuweka wazi matokeo yangu na si kwa vigagula kama Yaya Hossein anayewadaa watu. Huyu jamaa mshenzi sana. Anaweza kukutabiria kuwa utaishi maisha mazuri wakati akimaanisha kinyume. Anaweza kukutabiria kuwa watakaokupinga watadedi kumbe akimaanisha wewe. Mie nimeamua kugombea bila kujali wala kuogopa vitisho vya shehe ubwabwa wa Migomigo aliyemuwangia jamaa hadi akadondoka dondoka kila mara.

Ifahamike. Hata mtakaponichagua kuwa rais, afya yangu haitakuwa suala binafsi la kifamilia na usalama wa taifa bali mali ya umma. Lazima mjua status ya afya na kiongozi wenu ili msiishie kuwa Nigeria na marehemu Oumaru Yar' Adua ambaye wapambe na waramba viatu wake walificha status yake hadi kumtesa akifa kwa mateso na kuwaumbua.

Hata ikitokea nikaukwaa au kuugua na kuanguka, sitaficha wala kudanganya umma. Nitawambia fika ninachoumwa hata kama ni ukimwi. Kwani mimi ni jiwe zaidi ya kuwa binadamu wa kawaida tena dhaifu? Hakuna ufisadi unaonuka kama kudanganya au kuficha afya ya kiongozi wa nchi.

Kitu kingine ambacho lazima nifanye ni kutangaza mali zangu. Nafanya hivyo ili kumpiku Kikwete ambaye amegoma kufanya hivyo. Hivyo kwa kutangaza mali zangu na afya yangu, nitakuwa nimemnyima uwezo wa kuchaguliwa na kura zake nitapewa mimi.

Mkakati mwingine ninaopanga kufanya na kunadi, ni kuuelezea umma ninavyomuenzi mzee Mchonga bin Musa bin Burito wa Mwitongo. Kama ambavyo hakuwatumia watoto au mke wake kwenye kampeni na uongozi wake, nami nitatangaza wazi kuwa mke na watoto wangu hawataruhusiwa kufanya shughuli yoyote ya kisiasa vinginevyo si kwa mgongo wangu. Kwa vile Kikwete anawatumia wanae, wapiga kura watamnyima kura na kunipa mimi.

Kitu kingine ambacho napanga kupigia debe ni kuwambia wapiga kura kuwa mke wangu mama Kidume, hataanzisha NGO baada ya mimi kuchaguliwa kuwa rais wa jamhuri. Sitamruhusu ili kuepuka migongano ya kimaslahi na kujiingiza kwenye biashara za ubuyu.

Nitawambia wapiga kura wazi kuwa wake za wakubwa wanapojiingiza kwenye NGO, licha ya kufuja madaraka ya waume zao, wanauibia umma. Hamjamuona mwizi mmoja anayezunguka huku na kule akimpigia kampeni mumewe kwa mwamvuli ya NGO iliyodhaniwa ni ya watoto wa kike kumbe hola? Kwa leo sitamtaja. Ila nikizidiwa nitamuanika ili mmjue na kumuepuka yeye na mumewe hata chama chake.

Kitu kingine, nikishachaguliwa mwaka huu, mwaka 2015 nitaunda tume huru ya uchaguzi na kukutana na vyama vya upinzani kuchagua mlezi wa vyama vya siasa. Sitafanya usanii kama wa wale wala kutumia asasi hizi kujineemesha kisiasa. Kwa vile sera zangu ni nzuri, sina cha kuchelea wala kuvunga.

Kitu kingine, nitaunda mamlaka huru ya kupambana na kuzuia rushwa siyo kuizua na kuipamba kama ilivyo. Nikiwa rais sitataka ofisi ya kupambana na kuzuia rushwa iwe chini ya ofisi yangu. Pia nitawawezesha polisi na vyombo vingine vya siri kuwachunguza tume ya kupambana na rushwa ili nao wasile rushwa kama ilivyo. Naamini hili litaondoa utata uliopo ambapo wala rushwa huwakamata wala rushwa wenzao. Lazima kuchunguzana na hakuna cha kuaminiana kienyeji.

Jambo jingine muhimu wapiga kura kujuzwa ni ukweli kuwa katibu mkuu wa chama changu si mpayukaji wala vuvuzela kihiyo. Ni msomi mkata tamaa. Nadhani wengi mnamfahamu. Nilimteua baada ya kuona katibu wa chama wa zamani mgosi Machungi wa Makambale,
kwanza kuwa kihiyo na pili vuvuzela aliyekuwa akitumiwa na akina Ewassa, Kanji na Mbwamwitu kuibia kijiwe. Hivyo naingia kwenye uchaguzi na kitu kipya tena kifaa kilichokwenda chuo siyo lile vuvuzela zilipendwa bingwa wa ufisadi mgosi.

Pia nawafahamisha wapiga kura kuwa mie sitachangiwa wala kudhaminiwa na magabacholi ili hapo baadaye niwalipe fadhila. Tegemeo langu ni wananchi wenye uchungu na kaya yao inayoendelea kunajisiwa na gendaeka wale muwajuwao ambao lazima mwaka huu niwakomeshe kwa ushindi wa kiatomiki siyo ule wa wizi wa kitsunami. Hivyo nawashauri wapiga kura wasikilize sera na kuzizingatia badala ya sura na longolongo. Maana kura yako licha ya kuwa kula ya mwingine ni taslim wal tasalum yaani ikienda hunyakwa na hairejei. Hivyo epuka kuwapa kura yako sharmutah na habithi wajao na uongo wa mchana.

Hakuna kitu kilinikera kama wezi fulani kuambiwa ukweli kuwa waliiba njuluku ya kaya halafu eti wanalalamika wametukanwa na lugha iliyotumika si ya kistaarabu. Hivi kweli hawa wanaujua ustaarabu? Kwani siri? Mlikwiba na mnaendelea kupanga kukwiba kula ili mshinde isitokee nikaukwaa nikawashindilia lupango bila huruma. Akina Ewassa na Roasttamu na Endelea Chenge, Nimmy Mkonongo na wengine mpo? Nyinyi na baba yenu ni mijizi tu hata kama kuna wajinga wanawaita waheshimiwa wakati hamna heshima. You are but thugs by all accounts. Samahani. Huwa nikipandisha mwenembago huwa naongea kimombo hata kilatini wakati mwingine Kijerumani.

Wakati mwingine huongea kwa lugha lakini siyo kama wale wezi wanaotangaza kwenye luninga kuwa wanafanya miujiza wakati miujiza yenyewe ni kuwaibia maskini na kujitajirisha.

Ngoja niwahi kwa msajili mshikaji kumwekea pingamizi Njaa Kaya kwa kutotangaza mali na afya yake.

Chanzo: Tanzania Daima Septemba 8, 2010.

No comments: