The Chant of Savant

Monday 4 October 2010

Hatuchukii CCM, Kikwete wala kampeni zao



Kuna maswali mengi kuliko majibu kuhusiana na staili ya mgombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Jakaya Kikwete ya kutumia wana familia yake kwa gharama za serikali. Pia kuna shutuma na lawama nyingi kuhusiana na mtindo wake mpya wa kuendesha kampeni zake kwa ujumla akiwatumia wakuu wa mikoa na wilaya kinyume cha sheria. Rejea waraka wa hivi karibuni uliofichuliwa na CHADEMA uliodaiwa kuwahimiza kuhakikisha CCM inashinda. Kutumia raslimali za umma kwa manufaa binafsi ni ufisadi. Ingawa hili linapotoshwa na wapambe zake, ukweli ni kwamba umma haufurahishwi na matumizi ya familia yake.

Kikwete si wa kwanza kutumia wana ukoo wake kufanya kampeni. Rais wa zamani wa Argentina Nestor Kirchner alimpigia kampeni hata kumwezesha kushinda kiti alichokiacha mkewe Cristina Elizaberth Fredinand de Kirchner. Lakini alifanya hivyo bila kificho kwa njia zinazokubalika kikatiba. Alimpigia kampeni mkewe kama mgombea (mwanasiasa) aliyeteuliwa na chama chake cha Partido Justicialista na si kama mkewe. Na isitoshe Cristina alijulikana kuwa mwanasiasa tangu akiwa mdogo na siyo kuanzia alipokuwa mke wa rais kama hawa wetu.

Rais wa zamani wa Marekani Bill Clinton, alimpigia kampeni mkewe Hilary lakini kama mwanasiasa na si mkewe. Kadhalika Hilary alianza siasa akiwa shuleni na siyo White House kama hawa wetu.

Barbara Bush aliwapigia kampeni mumewe na mwanae Gerge W Bush Sr and Jr si kama mke au mama bali mwanachama ambaye hakutumia raslimali za umma.

Juzi juzi tulimuona mke wa rais wa Marekani Barack Obama, Michelle akimpigia kampeni mumewe. Alifanya hivyo kabla ya mumewe kuwa rais na akigombea tena hawezi kutumia fedha ya umma kufanya hivyo na asiathiri matokeo yake.

Hapa ieleweke bayana. Kinachogomba kwenye kampeni za Kikwete si kampeni bali namna zinavyofanyika ukiachia mbali wafadhili wake. Kinachogomba ni kile waingereza huita nepotism yaani utawala wa kidugu.

Salma na Ridhiwani, Miraj Kikwete hata Rahma Kharoos binti Kasiga wana kila haki ya kumpigia kampeni mpendwa wao. Kinachogomba ni matumizi mabaya ya magari, fedha, ndege hata muda wa umma. Rejea kashfa ya hivi karibuni iliyofichuliwa na CHADEMA kuwa Salma alitumia ndege ya serikali. Kama nani hata kama ni kwa kukodishw ana CCM?

Salma na wanae wana kila sababu na haki ya kumpigia kampeni baba au mume lakini wafanye hivyo kwa njia sahihi. Salma kama mke ana haki ya kumpigia kampeni mumewe lakini si kama mwenyekiti wa WAMA.

Kinachogomba si wanafamilia ya Kikwete kumpigia kampeni bali kulindwa na vyombo vya dola, kupokelewa na wakuu wa mikoa na wilaya na makandokando mengine ambayo si stahili yao kikatiba. Huu ni ufisadi na ufujaji wa raslimali na fedha ya wanuka umaskini wa Tanzania. Huku ni kucheza rafu. Maana, kwa kugharimiwa na serikali, wanapoteza sifa mojawapo ya uchaguzi wa kidemokrasia na huru na haki. Tunataka uwanja sawa na fursa sawa hata kwenye vyombo vya habari.

Salma anatoa khanga na matamshi ya kukandia wapinzani kwa kutumia pesa yao kama wananchi walipa kodi wa nchi hii. Hii si haki. Huu ni mchezo mchafu hata kama unafanywa na wenye madaraka. Hii ni hatari kwa mstakabali wa taifa kama wapinzani na wapenzi wao wataamua kusema enough is enough. Hii inaweza kuzusha rabsha na mapambano baina ya wanaohujumu haki na wanaohujumiwa.

Kama Salma hawezi kuishi bila kufanya siasa au kuvunja katiba basi achague moja kati ya haya mawili. Agombee nafasi ya kisiasa hata kumshawishi mumewe amteue waziri kama alivyofanya imla wa Uganda, Yoweri Museveni aliyemteua mkewe kuwa waziri au mwanae kusimamia kikosi maalum. Pili aache kujificha kwenye NGO yenye jina zuri la Wanawake (wa Tanzania nzima bila shaka) na Maendeleo. Ajitokeze kama Salma mwanasiasa na si mwenyekiti wa NGO yenye kutia mashaka ukiachia mbali kuonekana kama matumizi mabaya ya madaraka hasa ikulu kusaka ngawira.

Imla wa Kenya, Daniel arap Moi, pamoja na uimla na ukihiyo wake, hakuwahi kuwaruhusu watoto wala mke wake kushiriki siasa ingawa aliwapa kibali cha kutumia jina lake kuibia mabenki na taasisi za Kenya. Kwa hili aliona aibu. Imla na wezi wa Congo Denis Sassou Ngwesso na yule wa Equatorial Guinea ndiyo hadi leo wana uchovu wa kuwatumia watoto wao wanaoibia serikali huku wao wakifumba macho. Hivyo sifa mojawapo za utawala wa ukoo kama tulivyoona kwenye baadhi ya mifano hapo juu ni uimla, wizi, matumizi mabaya ya mali ya umma vitu ambavyo nisingependa vimkumbe Kikwete.

Mfumo wa utawala wa kifamilia unapoanguka balaa huwa kubwa na familia husika huteketea. Maana huwa hazina uhalali zaidi ya kujificha nyuma ya madaraka ya mtu mmoja (rais). Tumeyaona kwa Saddam Hussein imla wa Iraki aliyeruhusu wanae kuwa marais wadogo wakifanya watakavyo. Wao na baba yao, utawala wao wa kizandiki ulipoangushwa wamekufa kama mbwa. Hatutaki hili kwa aliyewahi kuwa rais wetu.

Yule mwizi wa DRC zamani Zaire Joseph Desire Mobutu alipoangushwa familia yake ilisambaratika sambamba kutokana kuwa na marais wadogo wenye kutumia jina la rais kama sifa yao ya kuongozea nyuma ya pazia wakitenda kila aina ya jinai na aibu.

Imla wa Togo Gnassingbe Eyadema alipofariki madarakani aliacha balaa ambapo watoto wake wawili, rais Faure Eyadema na Kpatcha wanatishiana kutoana roho wakigombea urais wa baba yao.

Tumalize kwa kuzidi kushauri kuwa Kikwete, ili ajitendee na kututendea haki, aachane na siasa za ukoo urafiki na familia. Aachane na mambo haya kutokana na ukweli kuwa cheo ni dhamana. Hufikia mahali kikatoweka na mwenye kuwa nacho akabakia na aibu yake kama aliyatumia vibaya au heshima kama aliyatumia vizuri.
Chanzo:Dira ya Mtanzania Oktoba 4,2010.

6 comments:

Anonymous said...

Huyu changudoa wa kimakonde anakera basi tu. Siasa hajui wala elimu hana ila kiherehere na ulimbukeni. Koma we nke wa Kiwete

Anonymous said...

I salute you Mpayukaji.

MADELA WA MADILU

Miriam said...

I am so happy to learn about you. But I am also so sad that I can not understand your blog.

Anyway, I wish you all the best!

Ndugu Nkwazi N Mhango said...

Thanks so kindly Miriam for visiting my blog. Methinks. Shall you revisit my blog time and again, you surely will understand everything.
Welcome and be blessed.

Ndugu Nkwazi N Mhango said...

Thanks so kindly Miriam for visiting my blog. Methinks. Shall you revisit my blog time and again, you surely will understand everything.
Welcome and be blessed.

malkiory said...

Mhango you are doing such a wonderful job to educate and liberate fellow Tanzanians from all sort of mental slavery.