The Chant of Savant

Tuesday 26 October 2010

Kikwazo cha Tanzania si CCM bali wananchi

Kama Chama Cha Mapinduzi (CCM), kupitia ushindi halali au wa kuiba kura au vyovyote kitarejea madarakani, watanzania watateseka zaidi ya wanavyoteseka sasa. Pia hii itawaonyesha kama watu wa ajabu na wasiojifunza hata kidogo. Na wasimlaumu mtu wala chama bali wao wenyewe.

Mwaka huu tumeshuhudia mitikisiko kuanzia ndani hadi nje ya CCM. Kulikuwapo na miparurano ya mitandao ya kugombea ulaji. Kulifuatia zoezi lililotawaliwa na rushwa la kuteua wagombea ukiachia mbali uongozi legelege na fisadi na wa kujuana. Tulishuhudia rushwa ilivyokivuruga, kukidhoofisha na kuzidi kukichafua chama huku kuenguana, kuchafuana, kuhujumiana na kutosana vikianza kuchukua nafasi ya sera.

Yote hayo juu yakichangiwa na kuishiwa sera, visheni na mikakati, kutoa ahadi hewa, ufisadi, uzembe, ubabaishaji (usanii), ukale na mawazo mgando ya baadhi ya watendaji wakuu wa CCM, ni dhahiri CCM ni hoi na hovyo. Hivyo, haina sababu ya kurejea madarakani kama watanzania watataka kusonga mbele na si nyuma. CCM irudishwe kufanya nini kilichoishinda kwa miongo yote hii?

Pamoja na udhalili na utepetevu tajwa hapo juu, watanzania wana kazi kubwa ya kujibu swali dogo lakini muhimu. Nani anaonyesha kuweza kukidhi mahitaji na matakwa yako kama mpiga kura, mwananchi hata mkazi kati ya CCM na CHADEMA? Nani ana sera zenye mashiko tofauti na usanii waliouzoea? Nani anafanana nao na kuongea lugha yao na si ya mafisadi?

Kuna kitu rahisi kinachowashinda watanzania-upembuaji kati ya pumba na mbegu. Kwa mfano, CHADEMA, wameahidi kutoa elimu na huduma nyingine za kijamii muhimu bure sawa na alivyofanya mwanzilishi wa Tanzania, Julius Nyerere. Japo hili linawezekana hasa wahusika wasipofisidi mali za umma, kuna watu, tena tunaodhani wana akili sawa sawa kumbe siyo, wanakejeli tamko hili kombozi na la kizalendo!

Ajabu wanaowacheka CHADEMA ni wale waliotoa ahadi magunia miaka mitano iliyopita wasitekeleze. Ni wale wale wanaoendelea kutoa ahadi za kuahidi kutekeleza sera zisizotekelezeka kama alivyowahi kuonya rais mstaafu Benjamin Mkapa! Na wanaendelea kutoa ahadi nyingine za uongo wa wazi kiasi cha hata kurudia zile walizotoa miaka mitano wasitekeleze! Hivi hapa kweli kunahitaji shahada za vyuo kujua muongo na mbabaishaji anayepawa kunyimwa kura ni nani?

Kwa vile watanzania wengi wamejitoa mhanga na kuishi maisha ya kujidanganya kwa kujipa matumaini kama waathirika wa ukimwi (maisha ya uongo na urushi), nao wanaogopa ukweli na kukumbatia urongo wa mchana.

Tumewaona watabiri na wahubiri njaa, wanajeshi uchwara wanaotumiwa kama nepi, waandaaji kura za maoni mapakacha, mashehe shehena na wengine wengi wakijitahidi kujipendekeza kwa walaji waliopo ili nao wapewa mabaki kiasi cha kuzidi kuwatishia na kuwahadaa watanzania. Hawa tuliodhania wanafikiri sawa sawa wameusaliti umma uwe wa wananchi au waumini na kulala kitanda kimoja na ufisadi.

Wametanguliza matumbo badala ya vichwa kiasi cha kuwa shirika moja na wanaonajisi na kuliibia taifa letu.

Watanzania wanapaswa kutambua jambo moja rahisi. Kila tapeli na jizi linalokuja linajificha nyuma ya kulinda amani ya Tanzania. Huwezi kulinda 'amani ya Tanzania' kwa kuwakingia kifua mafisadi na matapeli wengine kama wale walioghushi vyeti vya taaluma, wawekezaji wezi na mauzauza mengine. Huwezi kulinda amani ya Tanzania kwa vitisho au kukiuka haki.

Amani ni haki na si maguvu, lugha tamu za uongo, vitisho iwe vya majeshi au majini na mengine kama haya. Amani ya kweli hainyeshi toka majukwaani wala haifundishwi na wanasiasa uchwara wenye mawazo mgando na ya kijima. Amani ya Tanzania haiwezi kulindwa kwa kuzuia watu kuhoji utawala wa kujuana, uswahiba, kulipana fadhili, familia na upuuzi mwingine namna hii. Amani ya Tanzania-kama ipo kweli- inawezeshwa na watanzania ama kutokana na ujuha au uvumilivu wao. Hapa sijui ni kipi ni kipi zaidi kuhitaji utafiti na darasa zaidi.

Si kwamba watanzania hawa ni majuha au mataahira kama wanavyodhaniwa na wanaowadanganya kutaka kuwatumia kama watakengeuka. Wasipofanya hivyo watathibitisha walivyo majuha. Kinachogomba hapa ni watanzania kushindwa kuwa wakweli kwa nafsi zao. Wameridhika na ubangaizaji na udokozi na bora liende kiasi cha kuona ndiyo maisha na kutishiwa nyau na wezi kwa kutishia kupotea kwa amani.

Kwangu heri nikose hiyo 'amani' mawenge ya kugeuzwa punda au ng'ombe ili nifaidiwe na makupe. Kwangu hakuna amani baina ya kupe na ng'ombe au kuku na mwewe. Amani ya namna hii ni mauza uza tu na uongo wa mchana unaodhalilisha mwenye kuukubali na kuutumikia.

Kinachoshangaza ni ujuha wa watanzania. Inakuwa vigumu kuamini kuwa wangehofia kuwa CHADEMA inaweza kuwadanganya ikilinganishwa na CCM ambayo iliwadanganya kwa kuwaahidi mengi isitekeleze lolote huku mgombea wake akiendelea kutoa ahadi nyingine za uongo. Nani wa kuweza kuamini kati ya Wilbrod Slaa na Kikwete ambaye miaka mitano yake madarakani imekuwa balaa na hasara tupu? Slaa akidanganya hatakuwa na ujanja wala kunusurika kama Kikwete ambaye anadanganya kwa makusudi akijua hii ni awamu yake ya mwisho. Na isitoshe kama CHADEMA kitachaguliwa hakitakuwa na ubavu wa kufanya madudu kama Kikwete kwa vile kitakuwa na chama chenye nguvu kwenye upinzani yaani CCM.

Inashangaza kuoan watu wazima wanaendelea kumuamini Kikwete na sera zake zisizotekelezeka kama alivyozielezea mtangulizi wake Benjamin Mkapa ambaye akilinganishwa na Kikwete ni sawa na mlima na kichuguu!

Kinachogomba zaidi ni watu hawa hawa kulalamika wanapoendelea kutapeliwa kwa upogo wao. Leo kwa mfano nani asiyejua kuwa fedha inayoishia kwenye misamaha ya kodi, rushwa, ufisadi, kutorosha nyara, madini na pesa za kigeni ukiachia mbali kuibiwa wizarani kila mwaka inaweza kutoa huduma za jamii bure?

Nani hajui kuwa kama Tanzania itapata viongozi si watawala wenye mipango na common sense wasiofuja pesa wala kupenda ukuu na kutumiwa inaweza kujiendesha bila kuhitaji misaada ya kipuuzi itokanayo na kujidhalilisha kwa kuombaomba? Nani anathamini elimu kati ya CHADEMA na CCM iliyoendelea kuwakingia kifua vigogo wake waliotuhumiwa kughushi?

Tatizo la Tanzania si ukosefu wa mtaji wala raslimali wala CCM zaidi ya watanzania wenyewe kuwa na malengo uchwara. CCM haina ujanja kuliko KANU. Wakenya walipoamua kuipiga teke KANU 'profesa' wa siasa Daniel arap Moi aliishia kutimka. Tumepoteza mianya mingapi tokana na viongozi wetu kuwa ndumila kuwili? Nani alijua kuwa CCM ingenusurika kutimliwa na kashfa ya Richmond ukiachia mbali wanafiki waliotuaminisha kuwa wanapinga ufisadi kutojiengua kama ilivyotokea Kenya?
Chanzo: Dira ya Mtanzania Oktoba 25, 2010.

No comments: