The Chant of Savant

Wednesday 16 February 2011

Somo kwa wake wa marais Afrika












LEILA Ben Ali au binti Trebelsi, mke wa Rais wa Tunisia aliyeangushwa na umma alijulikana kama ‘Imelda Marcos wa ulimwengu wa Kiarabu’ kutokana na israfu na wizi wa pesa ya umma.

Mhudumu huyu wa saluni wa zamani alifanikiwa kumuingiza majaribuni Ben Ali kiasi cha kutimuliwa kama mbwa kutoka madarakani hivi karibuni.

Leila mama tamaa hakuwa peke yake katika mchezo huu mchafu. Inasemekana tangu mumewe kuingia madarakani alikuwa mtu safi. Ben Ali alianza kuharibikiwa alipomuoa mama huyu mpenda raha.

Ndoa ya Leila na rais ilimwezesha Leila kutengeneza ukoo wa mabilionea yaani, kaka zake wapatao 10. Walimiliki kila biashara iliyoingiza pesa kuanzia internet café, uuzaji wa magari, hisa katika mabenki na shirika la ndege la Tunisia na kupata upendeleo katika mikopo hadi kaka yake kuanzisha benki iitwayo Zeitouna, ambayo ilichomwa moto na waandamanaji.

Uliza walikopata mtaji. Ni sehemu moja. Dada yao alikuwa anamiliki chumba cha kulala na rais. Mtaji wa ajabu sana kama tutaangalia hili kwa makini.

Je, ni wangapi Afrika wanatumia mapenzi yao kwa marais kujinufaisha wao na familia zao? Leila hakuwa na haja ya kuanzisha NGO ili kupata pesa ya kificho zaidi ya kuiingiza ukoo wake kwenye ujambazi dhidi ya umma.

Kuna uvumi genge hili la ndugu Watunisia walilozoea kuita mafia lilikuwa likijihusisha na utoroshaji wa pesa na biashara haramu ya mihadarati.

Kilichofanyika Tunisia ni picha ya kinachoendelea kwenye nchi nyingi za Kiafrika.

Huu ndiyo utukufu na ukuu katika nchi za Kiafrika ambapo mpaka kati ya rais, watoto zake, mkewe na waramba viatu wake haupo.

Rejea jinsi walioko nyuma ya kashfa ya Richmond-Dowans-Kagoda wanavyolihenyesha taifa.

Nchini Zimbabwe, Grace Gucchi Mugabe, mke wa imla Robert Mugabe, anaweza kufanya kufuru yoyote kifedha na asiulizwe kisa analala kitanda kimoja na rais. Ni mama mwenye ushawishi si kawaida. Hata uhusiano wake wa kimapenzi na Gavana wa Benki Kuu ya Zimbabwe (RBZ), Gideon Gono ulipofichuliwa, Mugabe hakuchukua hatua yoyote.

Nchini Ethiopia mke wa Waziri Mkuu, Meles Zenawi, aitwaye Azeb Mesfin huitwa Queen of Mega, kutokana na kushiriki ufisadi mkubwa (Mega Corruption).

Nchi ya jirani ya Kenya, mke wa rais, Lucy Kibaki, ana madaraka kiasi cha kuvamia vyombo vya habari na kuwazaba vibao waandishi kwa kuandika uoza wa familia yake.

Pale Uganda ndiyo usiseme. Mke wa imla wa nchi hiyo, Janet Museveni ni mbunge, First Lady na waziri, ukiachia mbali kuwajaza wanawe na ndugu zake kwenye ofisi ya rais na sehemu nyingine za ulaji. Hapa kwetu, sitaki kusema, utajua mwenyewe.

Wengi wanaona kama huu ni ufisadi wa aina yake. Wangetaka wake za marais wa Kiafrika waache kutumia madaraka ya waume zao kujineemesha wao na ndugu zao na mashoga zao.

Siku hizi wamebuni hata mtindo wa kuwa na vikao sambamba na waume wao kwenye mikutano ya Umoja wa Afrika kama mlivyoona hivi karibuni. Mbona hatuoni wake au waume wa viongozi wa Jumuia ya Ulaya wakifanya hivyo kama huu si ufisadi na ukupe wa kutupwa?

Turejee kwa Leila. Alimgeuza rais wa nchi bwege na kifaa cha kuchumia utajiri haramu na haraka kwake na ndugu, mashoga na waramba viatu wake. Si rais wala mkewe, hakuna aliyeona mbali. Je, wako wangapi kama hawa barani Afrika?

marehemu Baba wa Taifa, Mwl. Julius Nyerere alituhusia kuwaogopa watawala wanaotawaliwa na wake zao. Hakuruhusu mkewe na watoto wake watumie ofisi ya umma aliyokuwa ameaminiwa na umma kujineemesha wala kujidai.

Alijua mipaka ya madaraka yake kiasi cha kuacha historia inayong’ara ambayo imewashinda wengi waliofuatia.

Siku hizi si ajabu kuona mtoto wa rais akiwa kijirais kidogo chamani mwake au mke wake akiwa kijirais nyuma ya pazia, kwa sababu tu analala kitanda kimoja na rais.

Nyerere hakuwa mchovu wala wa hovyo hivi. Aliona mbali kiasi cha kujitenga na ufisadi huu unaooanza kuhalalishwa ambapo Ikulu nyingi zinaendeshwa kama magenge ya ujambazi dhidi ya umma. Kilichotokea Tunisia ni ushahidi wa kutimia kwa utabiri na wosia wa Mwalimu.

Hakika kilichojiri Tunisia ni changamoto kuwachunguza watawala wetu na familia zao. Ni suto kwa wale wote wasiosoma alama za nyakati kama Ben Ali na Leila wake ambao wanaishi kama vibaka uhamishoni huku wakisakwa nyumbani kwao waadhibiwe.
Chanzo: Tanzania Daima Februari 16, 2011.

No comments: