The Chant of Savant

Thursday 3 March 2011

Bado mmilki wa Dowans ni Rostam Aziz na mabosi wake



Kujikanganya kwa brigedia Suleiman Al Adawi anayedaiwa kuwa mmilki wa kampuni tata ya Dowans ni ushahidi mwingine kuwa huyu jamaa si mmilki halisi wa Dowans bali msanii wa kawaida tu.

Al Adawi ambaye kumbe amegundulika kuwa ni Mzanzibari mwenye utata juu ya alivyopata nyumba zake za Zanzibar, hashawishi kuwa mmilki wa Dowans.

Kuna sababu lukuki za kuamini kwa Dowans ni mali ya Rostam.

Rejea Al Adawi kuwahi kuikana na kutamani apewe Dowans bure kama ilivyotokea hivi karibuni alipokuja kusafisha ufisadi kwa kisingizio cha ubilionea usiojulikana alivyoupata.

Je ni sababu gani zilizofanya kuikana kampuni “yake.” Ni mtu gani asiye kichaa anaweza kukana kampuni yake tena inayodai mabilioni ya shilingi? Je utajiri wa Al Adawi ni kiasi gani hadi kuwa na jeuri ya kukana mali na biashara yenye zaidi ya dola 300,000,000? Maana ukiangalia thamani ya mitambo ya Dowans na pesa wanayodai kama fidia ni pesa nyingi tu ambayo hata Bill Gates hana uwezo wa kuikana hasa inapokuwa ni mali yake hasa na si usanii kama huu tunaofanyiwa mchana na wapuuzi wachache.

Jiulize swali jingine. Serikali na Tanesco wamekana kumwalika. Je amealikwa na nani kuja kufanya usanii wake? Je kama serikali haikumualika kwanini isimkamate hata kwa makosa ya kujipatia nyumba za umma kinyume cha sheria na taratibu? Maana inasemekana Al Adawi ana nyumba mbili Zanzibar alizonunua kimagendo kwa kusaidiwa na kiongozi mmoja mstaafu wa Zanzibar.

Turejee kwa Dowans. Je tuamini lipi kati ya kuikana na kudai ni yake? Hili swali linamkabili hata aliyemleta tuseme bosi wake anayejifanya kuwa mfanyakazi wake yaani Rostam.

Rostam amewahi kukana kuijua, kuimilki wala kuwa na uhusiano na Dowans tena mbele ya bunge. Kimsingi,Rostam alilidanganya bunge jambo ambalo ni kosa la jinai. Je kwanini bunge halimchukulii hatua? Je bunge la namna hili halijawekwa rumenya na mafisadi?

Je madai kuwa spika wa sasa Anna Makinda alichaguliwa na mafisadi ili kuepuka kuchaguliwa kiboko yao spika wa zamani Samuel Sitta hayapati uzito na mashiko hapa? Nitashangaa kama bunge na spika watakaa kimya bila kushughulikia kashfa hii mpya ya Rostam kulidanganya bunge. Na bila spika kulishughulikia hili wengi wataendelea kuamini yale yaliyovuma wakati alipoteuliwa kugombea uspika kuwa alikuwa chaguo la mafisadi. Rejea baadhi ya vyombo vya habari viliporipoti kuwa ni Rostam aliyekwenda kumshawishi Makinda agombee na wote wawili wasikanushe. Je wakati wa Makinda kulipa fadhila ndiyo umefika kwa kukalia kashfa hii?

Kwanini Makinda aweze kumtimua mbunge wa Arusha (CHADEMA) kwa kudai kuwa waziri mkuu Mizengo Pinda alilidanya bunge lakini akae kimya bunge lake linapodanganywa?

Tuache mchezo na maisha yetu na vizazi vyetu. Tuzidi kuwabana wahusika ili tujue ukweli. Je ukweli ni upi kati ya huu wanaotwambia sasa na ule waliotwambia siku za nyuma wakiikana Dowans. Rostam aliwahi kusema kuwa haijui Dowans achilia mbali kuimilki kupitia Powers of Attorney. Je uongo na ukweli ni upi?

Kwanini Rostam na brigedia wake waliikana Dowans halafu baadaye wakaja kuikubali na kuitumikia? Kwanini hawasemi kuwa nao wanatumika na mkubwa asiyependa kujulikana kuliibia taifa? Hata hivyo, wao wana uchungu gani iwapo wana kwao kwingine pa kukimbilia mambo yakichacha? Hata wanaomtumia nao hawana akili nzuri ikizingatiwa kuwa wengi kama wao wameadhirika baada ya mambo yao kufichuka. Nani alijua kuwa uoza, kwa mfano wa Benjamin Mkapa wa Kiwira ungegundulika baada ya kuachia madaraka?

Sababu nyingine ni kwanini brigedia aliogopa kupigwa picha? Je alijua kuwa akipigwa picha wanaoumfahamu watamuumbua kama inavyoendelea kubainika kuwa kumbe alisoma Zanzibar? Hakik, kama alivyodai kuwa hapendi sifa, kama ni kweli, basi huyu jamaa ni mfanyabiashara wa kwanza kutopenda sifa. Hata hivyo huku ni kujidanganya. Kama hakutaka kujulikana basi asingetaka hata jina lake lijulikane.

Sababu nyingine ni kubainika kuwa kumbe aliyekwenda Marekani kuileta Dowans ni mfanyakazi wa Rostam aitwayeHenry Surtees. Pia ukiangalia mgongano wa maslahi na matumizi mabaya ya cheo, Rostam hawezi kukwepa kuwa na hatia ya kutumia vibaya madaraka yake kichama chini ya kile mahakama ya kimataifa ilichoiita ushawishi mkubwa.

Sababu nyingine ni ile hali ya Rostam eti kupewa power of attorney hata kabla ya kampuni yenyewe kuanzishwa. Kisheria hii ni batili kama wanasheria wetu wataacha kutumia njaa kutetea kesi. No contract or agreement can be entered over nonexistant entity. Haiwezekani mtu au watu kuingia mkataba juu ya kitu ambacho hakipo. Kitu kama hakipo hakipo hivyo hakiwezi kumilkiwa hadi kiwepo.

Sababu nyingine ni kugundulika kuwa Dowans haina biashara nchini Costa Rica inakodaiwa kuzaliwa ukiachia mbali sheria za nchi hii kuruhusu usajili wa makampuni ya kitapeli.

Bila wahusika kujibu hoja na maswali yaliyoulizwa hapo juu pamoja na mengine, bado tutaendelea kuamini kuwa Dowans ni mali ya wakubwa wanaowatumia kina Rostam kuficha uoza wao. Vinginevyo hadi hapa, bado Dowans ni mali ya Rostam na siyo hawa wasanii anaotuletea wakashindwa hata kuitetea kampuni wanayodai ni yao.
Chanzo: Dira ya Mtanzania Februari 2011.

1 comment:

Anonymous said...

Rostam na Kikwete ni majambazi na watapeleka nchi yetu pabaya tusipowashughulikia haraka sana.