The Chant of Savant

Wednesday 2 March 2011

Januari Makamba usishangae kuingia bungeni



MBUNGE wa Bumbuli (CCM), Januari Makamba, ambaye ni mtoto wa katibu mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Yusuf Makamba, alikaririwa akisema anashangaa alivyofika bungeni.

Kutokana na umuhimu wa suala zima la jinsi watu wanavyoingia bungeni na unyeti wa ubunge, nimeonelea niliongelea hili.

Makamba alikaririwa Februari 16, akisema, “Rais wa Marekani aliyepata kuwa mbunge huko kwao na kule kwa wenzetu ubunge ni miaka miwili alipata kusema katika utumishi wake wa ubunge alitumia mwaka mmoja kujishangaa amefikaje bungeni na mwaka wa pili kuwashangaa wenzake wamefikaje hapo.”

Aliendelea kusisitiza ujumbe wake japo hili linazua maswali mengi kwa wachambuzi. Alikaririwa akisema, “Ndivyo ilivyo kwangu katika mkutano wa kwanza nilishangaa mimi nimefikaje humu ndani… lakini kwenye mkutano huu nikawa nawashangaa wenzangu wamefikaje pia hasa pale walipoamua kususia hotuba ya Rais.”

Kwanza, ni makosa kwa Makamba kulinganisha mtindo na mfumo uliomwingiza bungeni na rais wa Marekani. Wakati rais wa Marekani aliingia kwa juhudi zake na kushinda kupitia ushindani wa kweli na safi, Makamba aliingia bungeni kutokana na ukoo wake yaani kuwa mtoto wa Makamba ukiachia mbali kupitia uteuzi na uchaguzi mchafu na usio wa haki na huru. Rejea madai yaliyotolewa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) bila kuwahi kukanushwa na CCM kuwa uchaguzi ulichakachuliwa na kura kuibiwa.

Rejea madai ya mbunge wa zamani wa Bumbuli, William Shelukindo, ya Januari kutumia madaraka ya baba yake na kucheza rafu hata kabla ya kipenga cha mwisho kupulizwa jambo ambalo linasadikiwa kuwa lilimsababishia kushindwa Shelukindo licha ya kumnyima haki.

Bila ushawishi na jina la baba yake, nani angempigia kura mtu ambaye alikuwa hata hajulikani huko anakokuita kwao? Bila jina la baba yake angewezaje hata kumilki nyumba na gari ukiachia mbali kupata kazi nono ikulu?

Turufu nyingine, licha ya siasa za kulindana iliyomwingiza Makamba bungeni, ni CCM kutumia pesa za umma kuwahonga wapiga kura huku kikihujumu vyama vya upinzani.

Sababu nyingine ni ujinga wapiga kura wetu ambao umekuwa mtaji mkuu wa CCM nchini. Rejea madai yaliyowahi kutolewa na chama chake kuwa watanzania hawasomi magazeti hivyo hata maovu yake yakianikwa hayataathiri kura zake.

Kama Januari ana ubavu ningeshauri ajibu makala hii. Wakati akifanya hivi arejee tambo za baba yake kuwa angekuwa waziri sawa na watoto wa vigogo wengine ambao hata wanadaiwa kughushi vyeti. Kama siyo bosi wake wa zamani kuona aibu kuonekana anatumiwa na Makamba au kuvuta muda, si ajabu angekuwa waziri. Na siku akiwa waziri tutasema kama tunavyosema kuwa ni shinikizo na ushawishi wa baba yake.

Hakuna ubishi kuwa Januari alisoma, kupata kazi hata ubunge si kwa sifa bali ukuu wa baba yake. Ukimuuliza alivyopata scholarship ya kwenda kusoma Marekani na kama amekwenda kwa kujidhamini alikopata pesa unaishia pale pale. Hizi ndizo sifa za watawala wetu wanaojihudumia huku wakitaka kurithisha madaraka kwa watoto wao.

Hata ajira yake ya ikulu ikichunguzwa kwa makini ni yale yale ya kujuana na kubebana kama ilivyowahi kuthibitika kule BoT.

Ni wangapi wenye shahada kama yake tena na kuzidi wangetamani waajiriwe ikulu lakini kwa vile hawana majina ya wana kundi la wenye nchi hawajui hata ajira za ikulu zinapatikana vipi?

Kwa ufupi ni kwamba Januari Makamba hana haja ya kushangaa alivyoingia bungeni. Kama anahitaji kushangaa basi angeshangaa mfumo na watu wetu kuendelea kuvumilia uoza huu.

Kwa ufupi ni kwamba kwenye ajira nyingi nono serikalini wamejaa akina Makamba. Sasa wamevamia bunge, sijia tutapona? Tunasikia kina January Makamba, Emanuel Nchimbi, Hussein Mwinyi, Vita Kawawa, Zainab Kawawa, na wengine kwenye maeneo mengine chamani na serikalini. Hili ndilo la kushangaa linavyoweza kuruhusiwa kushamiri wakati ni jinai.

Hata ukienda kwenye biashara zenye maana utasikia majina ya Fred Lowassa na wengine. Ukienda kwenye viwanja vilivyopimwa sehemu za maana ni wale wale. Bado hujaenda kwenye kazi nyeti kama tulivyowahi kufunuliwa kule BoT. Kimsingi hawa ni wale wale waliolelewa kwenye nyumba za wizi za umma ambazo wazazi wao baada ya kuzikalia wakilipiwa kodi na serikali, waliamua kuzitwaa kabisa.

Kama Januari ni bingwa wa kushangaa basi angejishangaa anavyoweza kupata mshipa wa kutetea Dowans kabla hata ya hao wapiga kura wa Bumbuli. Rejea kuipigia debe mitambo ya Dowans iwashwe ilhali akijua fika ina mgogoro.

Namshangaa Januari Makamba kujishangaa ubunge badala ya uoza uliomfikisha hapo alipo.
Chanzo: Tanzania Daima Februari 2, 2011.

3 comments:

Kalumekenge Lowassa Malechela said...

Na mimi kuanzia leo nabadilisha jina na kuanza kujiita Kalumekenge Lowassa Malechela. Nina PhD ya kughushi na nakupa mwezi mmoja tu na tayari nitakuwa nimepata kazi kubwa tu serikalini.

Sijui wanyonge wataamka lini jamani.

Kijana huyu naona amekomaa kweli mitambo ya Dowans iwashwe. Pengine yeye na babake ndiyo watailipa. Posho na mishahara wanayopata waki-combine zinatosha kuilipa Dowans bila shaka.

Ndugu Nkwazi N Mhango said...

Kalumekenge umeniacha hoi. Natamani niandike kijiwe kizima kuhusu hili. Mie nitaanza kujiita Plato Cicero Galileo Diogenes mjukuu wa Socrates bin Kikwete.

Anonymous said...

Wanaomfahamu January wanasema ni kihiyo kama baba yake na hakuwa na sifa za kujiunga na UDSM.
Hata hivyo uliyosema ni kweli, Bila madaraka ya baba yake na ubwege wa JK asingefika hapo alipo ndiyo maana anashangaa.
Kuna haja ya kuchunguza hata hizo digrii zake za kununua Marekani.
January hana tofauti na akina Nchimbi, Masaburi, Makongoro Mahanga, Mary Nagu, Lukuvi na wengine wanaojulikana kughushi. Kesho utasikia Makamba ana digrii ya kununua kama Lyatonga Mrema.