The Chant of Savant

Wednesday 13 April 2011

Nimelazimika kugombea urais 2015

Baada ya kuona watanzia wanavyopuuzia mambo ya maana na kupwakia yasiyo kuwa na maana, nimejikuta nikilazimika kugombea urais mwaka 2015. Nina uhakika nitashinda.

Leo naandika nikiwa serious. Sitafumba wala kuzungusha bali kulonga na kuzoza vilivyo. Nitagombea urais. Pia nikichaguliwa sitakuwa rais rahisi au kichwa cha mwendawazimu cha mafisadi na mawakala wao. Nitakuwa chuma cha pua kama Mchonga. Sitakuwa rais rahisi wa kutoa ruksa au kuchekachekea mabalaa na mambo ya hovyo. Nitakuwa muadilifu kama Madiba. Wala sitakuwa limbukeni na kayaya wa kutukana walevi kuwa wana uvivu wa kufikiri kama njomba Ben Makapi aliyewatukana akaingizwa mjini na mama la kikishumundu akaishia kuishi kwa kujificha kama bundi. Mie sitatawaliwa na mke wangu wala kaka zake. Kiwila ziiii! Net Group Problems ziii! Uongo na ufichi ziii! Message delivered.

Kwanza ngoja niwamegee sababu zilifanya niamua kugombea:

Mosi, ni ile habari chafu kuwa eti na Eddie Luwasha anajiandaa kugombea kiasi cha kuchukua njuluku toka kwa Roast Tamu eti kujisafisha. Hivi kuna mwendawazimu anaweza kuninyima kura akampa mwizi na jibaka kama Luwasha? Kwa taarifa yenu, mkinichagua namfunga maisha na kutaifa mimali yote aliyojirundikia baada ya kukwapua kwenye asasi zenu.

Pili, nitahakikisha nakuwa rais ili nirejesha nyumba zenu na kuwafunga akina Kagoda na wale wote walioghushi vyeti vya kitaaluma. Siwezi kuwa rais bwege anayeweza kuchekelea wizi wa nyumba za umma unaohangaika na kupanga ilhali nyumba zake zinakaliwa na mibaka. Siwezi kuwa rais juha ambaye yuko tayari kuona nyumba za umma zinapangishwa kwa maponjoro na magabacholi huku umma ukiendelea kusota. Never! It shall nary happen under my watch.

Tatu, siku ya kwanza nikiingia ikulu nitamwita babu wa Loriyondo na kumpiga marufuku aache usanii. Maana naona amegeuka serikali kiasi cha kuacha mambo yote ya muhimu na kupwakia usanii wake. Kama ni kuoteshwa mie ndiyo nilionana na Sir God. Hata hawa matapeli wadogo wadogo waliotamalaki wakitangaza kuoteshwa tiba wakidhani hili ni taifa la ndondocha na wagonjwa nitawapiga marufuku na ikiwezekana kuwafunga. Hata vigogo watakaokwenda kupata vikombe nitawatupa lupango maana ni wapuuzi. Serikali yangu haitakuwa na dini wala duni.

Ndani ya siku mia baada ya kuapishwa, nitaunda jopo la wataalamu kuchunguza madhara hali ya ukimwi ili kujua ni kwanini watu wanapwakia kila upuuzi uitwao tiba. Maana inaonyesha tatizo ni kubwa kuliko lilivyo. Pia nitahakikisha kuwa yeyote atakayetaka kuteuliwa nami anapima na kuweka wazi matokeo ya afya yake. Yes. Huwezi kuwa public figure ukaendelea kuficha status yako.

Ndani ya siku mia nitahakikisha Kagoda, Dowans na majambazi wengine wananyea debe. Lazima turejeshe taifa kwenye mijadala yenye siha badala ya kujadili ushirikina na utapeli tena wa kijuha kama madawa ya kuoteshwa.

Kitu kingine kilichonisukuma kugombea ni kuhakikisha walevi wanapata katiba safi. Hii inatokana na kuanza kuona dalili zote za uchakachuaji wa katiba mpya. Katiba nitakayosimamia ni ile inayotamka wazi kuwa rais lazima atangaze mali zake na mkewe na kuapa kupambana na ufisadi kwa vitendo na si ngonjera. Pia nitapendekeza adhabu ya kifo kwa mafisadi na sitakuwa rahisi mwenye ushikaji na mafisadi maana ni upuuzi. Pia mke wa rais asiwe kupe mgongoni mwake kama ilivyo.

Sitakuwa rais rahisi mwenye kujiruhusu yeye na taifa kufanyiwa majaribio ya kitibabu kiloliondoLoliondo. Never, never on my dead body. My foot! This shall not happen in my presidency.

Nitakuwa rais bora si bora rais. Nitatangaza sera zangu ambazo nimeanza kuzitangaza kwa kuorodhesha sababu za kugombea. Kauli mbiu yangu ni utawala kwa vitendo na si maneno. Sina kazi wala ari za uongo na usanii. Mimi ni rais anayechukia kuunda tume za kijambazi au kuendekeza ndugu na maswahiba zangu kula eti kwa vile nimekuwa rais. Ukifikiria kula mgongoni mwangu kama kupe, uwe mke, mtoto au rafiki yangu, jua umeliwa tena sana tu.

Sababu nyingine iliyonisukuma kugombea ni ile hali ya kuona wapinzani wanafanya mambo kwa majaribio. Wako wapi CHAKUDEMA? Yako wapi maandamano Kaya nzima zaidi ya yale ya kwenda Loriyondo? Au nanyi mmelishwa au kunywesha vikombe na chama cha manonihino kama rafiki zangu Prof na Madevu waliogeuka nyumba ndogo hivi hivi tinaona? Tiambiane jamani.

CHAKUDEMA nawaita itikeni. Mko wapi? Au nanyi mnaanza kuelekea ile sumu ya ufisadi na ubinafsi iliyowanasa ngunguli na ngangari wakaishia kung’ang’aniana kwenye ulaji wa aibu? Je nanyi mna mpango wa kuwekwa nyumba kimada au kufunga ndoa hii chafu na ya aibu?

Nawasihini mchunge sana gwiji naja. Tena nakuja baada ya kufanya utafiti kuwa nitashinda. Siji kimkwara kama akina Lyatongolwa waliokuja wakatikisa wakaishia kuwekwa rumenya na sasa wanaramba matapishi yao. Mie nakuja na uhakika kwa aslimia elfu. Nitashindwaje iwapo walevi wanajua wazi kuwa kuna ombwe na anayeweza kuliondoa ni mimi?

Si uchonganishi. Juzi nilisikia taarifa za ufisadi wa kutisha na hakuna aliyeamka na kutoa lau karipio zaidi ya kuchekeana! Yaani karne ya 22 ya kompyuta na dot com bado mnalipana mishahara hewa hata kwa marehemu! Mie ni mtu makini. Nilishatamka mara nyingi kuwa nachukia kiza na kupenda mwanga. Hivyo chini ya utawala wangu sahauni mgao na kulanguliwa umeme. Chini ya utawala wangu sahau mibanano na upuuzi mwingine mnaoshuhudia kwa sasa.

Najua mtatizo ya wanakaya ni ufisadi, usanii na kutokufikiri sawa sawa. Walevi wanaijua falsafa yangu. Ni simpo. Fikiri kwa kichwa badala ya tumbo na kiuno. Hivyo, nina simpo solusheni kwa matatizo ya walevi. Nitafanya mambo kinyume na sasa. It is that simple so to speak.

Hebu nitoe demo kidogo. Kwa sasa mafisadi wanafugwa. Nikiingia madarakani nafanya kinyume-natwanga shaba. Kwa sasa watu wanaghushi vyeti. Nikiingia madarakani nao nalambisha shaba. Wale wazito wanatumia mashangingi huku wakiwapa wagonjwa bajaj wasahau. Nikiwa rais itakuwa kinyume. Kwanini mgonjwa asipewe shangingi lau akafarijika na bajaj wakapewa waliotaka uongozi kwa hiari yao tofauti na mgonjwa ambaye hana hiari na ugonjwa?

Yule jamaa ananidai. Acha nijikate kisilesi kabla hajanienga.

Chanzo: Tanzania Daima April 13, 2011.

5 comments:

malkiory said...
This comment has been removed by the author.
malkiory said...

MHANGO: Ni uamuzi wa busara na kishujaa. Taifa letu linahitaji watu jasiri kama wewe, tuko pamoja katika harakati hizi za ukombozi!

Yasinta Ngonyani said...

Hakika si utani kakangu na tupo nawe bega kwa bega. na ukisha kuwa Raisi basi mimi naomba kuwa ..... wewe utanipa hicho utakachoona nafa kuwa...

Ndugu Nkwazi N Mhango said...

LOL! Naona naanza kunyakua kiti hata kabla ya kuingia kwenye kinyang'anyiro! Allah Akbar!
OMG! Mie mkishanichagua msome tena ahadi zangu ili tusijelaumiana. Maana nalenga kuwakomboa walevi wa Bongolalaland toka mikononi mwa mafisadi na Njaa Kaya.
Nawashukuruni na muanze kunipigia kampani ya kampeni ili nami niule.

MloMmoja said...

Ukituita tutaika,japo tuna mashaka coz joka la kibisa kabla halijajivua gamba lilifanikiwa kutung'ata mara kadhaa kwa ahadi nono za nchi ya maziwa na asali....