The Chant of Savant

Wednesday 29 June 2011

Kama Nape msaliti, Wassira ni nani?

INGAWA siasa ni mchezo uliojaa uchafu, hadaa na kujilisha pepo, lazima unahitaji kutumia akili. Pamoja na uchafu wake, bado siasa ni kitu ambacho hatuwezi kuishi bila kuwa nacho.

Je, tukubali kila siasa ziwe ni chafu au tuanzisha ustaarabu na utamaduni mpya wa kuweka usafi kwenye siasa?

Tunauliza na kuandika haya kutokana na Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuendelea kuongeza uchafu katika siasa za nchi yetu ambazo tayari ni chafu. Kwanza tunashangaa jeuri na upogo huu vitaifikisha wapi CCM.

Kuna taarifa kuwa CCM ina mpango wa kuanza kushughulikia wanoitwa “Mapacha Watatu” ili kulipiza kisasi na kuwaokoa mafisadi waliotajwa na CCM yenyewe baada ya kupitisha uamuzi kuwa “wajivue gamba” kwa kuwatosa.

Hapa wanaotajwa kuwa Mapacha Watatu ni aliyekuwa Waziri Mkuu Edward Lowassa aliyeporomoshwa na kashfa ya Richmond, Waziri na Mwanasheria Mkuu wa zamani, Andrew Chenge anayedaiwa kujiingizia mabilioni ya shilingi kwenye ununuzi wa rada na ndege ya rais na Mbunge wa Igunga, Rostam Aziz anayeshutumiwa kuwa nyuma ya kashfa ya Richmond na ukwapuzi wa mabilioni toka kwenye fuko la Madeni ya Nje (EPA).

Pamoja na watatu hawa kujulikana ndani na nje kwa ushiriki wao katika kashfa hizi ukiachia mbali kuwa washirika wakuu wa Rais Jakaya Kikwete. Wananchi walijitahidi kunyamaza ili waone CCM na serikali yake ingefanya nini kujiondoa kuhusishwa na watu hawa.

CCM kwa kuzidiwa na tuhuma, iliamua kuitisha vikao vyake vikuu na kutoa tamko la kuwapa siku 90 ambazo zinaisha tarehe 10 Julai. Wengi wanangoja kuona nini kitafanyika ingawa dalili zinaonyesha kuwa CCM haikufikia uamuzi huu kwa dhati zaidi ya kutafuta muda na kufanya usanii kama ada.

Katika kutafuta namna ya kufunika kombe ili mwanaharamu apite, mikakati imeishaanza ya kutaka wanaojulikana kama wasaliti chamani yaani, Spika wa zamani wa Bunge na waziri wa sasa Samuel Sitta aliyeridhia kuchunguzwa kwa Richmond na Mwenyekiti wa Kamati teule ya Bunge iliyochunguza Richmond, Dk. Harrison Mwakyembe, mbunge na waziri pamoja na Katibu wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, kwamba watoswe kwa madai ya kukisaliti chama.

Kimsingi hakuna usaliti wala kosa kichama na kisheria. Kwanza, chama chenyewe hata akikuundwa. Maana kuundwa chama kikafa bila kusajiliwa kisheria ni kwamba hakikuundwa. Hata kama wangeunda chama kikasajiliwa na kikafa wasingekuwa wametenda kosa ikizingatiwa kuwa katiba yetu iko wazi kuwa kila mtu ana haki ya kujiunga au kuunda chama chochote wakati wowote. Huu si uhuru wa CCM wala serikali bali katiba.

Kama kina Nape, Sitta na Mwakyembe watakuwa wasaliti tuwaite nani kina Stephen Wassira, Masumbuko Lamwai, Walid Kabourou, Thomas Ngawaiya, Augustine Mrema, Maalim Seif Shariff Hamad na wasaliti wengine wa wazi ambao waliowahi kukimbia chama na kurejea baada ya kusota kwa njaa kwenye upinzani au kukaa kule wakiitumikia CCM? Je, hawa wanaoitwa wasaliti na mafisadi nani wanamsumbua Mtanzania?

Tuombe Mungu wanachama wa CCM waendelee kutafutana uchawi huku wakikwepa sababu kubwa ya kuzorota na kuchukiwa kwa chama chao ambayo si nyingine bali ufisadi mitandao na ubabaishaji.

Kama wanaona waliotaka kuunda chama ni wasaliti, basi wawaone hivyo hivyo walioanzisha mitandao ndani ya chama kiasi cha kugeuka mauti yake. Waliotaka kuunda chama wana nafuu ukilinganisha na waliounda mitandao. Kwani madhara ya mitandao kwa chama na taifa yamekuwa makubwa kuliko hata hicho chama mimba ambacho hakikuzaliwa.

Kuna haja ya kuwashauri CCM waache unafiki na upofu. Bahati nzuri, tarehe 10 Julai imekaribia ambapo CCM itavuliwa nguo kutokana na mafisadi kutoachia nyadhifa zao kama ilivyowataka wafanye. Ama kweli huu utakuwa mtihani kwa CCM na Jakaya Kikwete na kufichuka kwa ubabaishaji wake.

Nani hajui kuwa mitandao iliyoundwa na Kikwete na Lowassa iliacha madhara makubwa nchini baada ya kuingiza siasa za kuchafuana na kubaguana? Kama kuna kitu kinaitafuna CCM si kingine bali matokeo na laana ya mitandao ya kuchafuana, kubaguana na kuliana njama ili kupata urais kirahisi kama ilivyotokea kwa Kikwete ambaye ameonyesha kuwa ajali za kihistoria zaidi ya kiongozi.

Nani mara hii kina Salim Ahmed Salim pamoja na uzalendo na rekodi zao zilizotukuka walibaguliwa na kuitwa Waarabu? CCM wanadhani dhambi hii itawaacha bila kuwatafuna?

Hata hivyo, CCM hawana ubavu wa kuwatimua kina Sitta kutokana na ukweli kuwa wakifanya hivyo wataumbuka zaidi. Nani mara hii kasahau jinsi walivyoficha mambo mazito yaliyomhusisha Kikwete kwenye kashfa ya Richmond? Kama Kikwete kajifanya kusahau hili akumbushwe.

Akumbushwe kuhusu waliomtangulia kama Richard Nixon wa Marekani aliyetokomea baada ya kujifanya kusahau alichopaswa kukumbuka. Hata hivyo, CCM wakitimuana na kusambaratika ndiyo neema kwa wananchi. Tuombe hili litokee ili tujikomboe.

Kitu kingine kinachofanya CCM isiwe na mpango wala ubavu wa kuwatimua akina Sitta ni ukweli kuwa licha ya kuwa wanasheria, wana funguo za mochwari ya CCM kama itajifanya kuwaita wasaliti na kutaka kuwatimua. CCM wenyewe ni wasaliti waliowasaliti wananchi kwa miongo mingi tu. Wanapata wapi mshipa wa kuwaita wenzao wasaliti wakati wao ndiyo wasaliti wakubwa?

Kama kina Sitta wataguswa, watakimbilia kwa wananchi kutaka kujua wao na mafisadi ni nani adui wa wananchi. Kama CCM hawataliona hili na kulikubali kwa kujikubali kuwa hawana ubavu wala udhu wa kuwashughulikia “wanafiki”, watakuwa wameonyesha unafiki usio kifani.

Kuna haja ya kuwahimiza CCM watimize walichoazimia wenyewe bila kulazimishwa kuvua gamba kwa kuwatimua mafisadi wanaojulikana. Je, kama CCM wataamua kuwa vipofu na vichwa ngumu kiasi hiki, wananchi nao watakubaliana na unafiki huu unaonuka kuliko kitu chochote?

Kwanini CCM wanapata muda wa kushughulikia watu wasio na hatia wakati wao ni wenye hatia?

Bado Watanzania kwa mamilioni wanashangaa inapopata muda CCM kuwashughulikia wapambanaji dhidi ya ufisadi huku ikikalia makumi ya kashfa kubwa tena zinazoendelea kuwafanya watanzania maskini kuliko wote katika ukanda huku pamoja na kuwa na “amani’ na raslimali nyingi tu!

Wengi wanajiuliza, inakuwaje viinchi vilivyokabiliwa misukosuko na vita tangu uhuru wake kama Burundi na Rwanda vinaizidi Tanzania? Wanashagaa CCM inapopata mshipa huu wakati serikali yake inakabiliwa na mauaji ya wananchi wasio na hatia huku ikitapanya pesa na mali za Watanzania!

Wengi wanashangaa kuona CCM inapata muda wa kuwaonea watu wema ili kuwalinda waovu! Hivi kina Sitta na Mstapha Mkulo aliyelidanganya taifa na Bunge kwa kuleta bajeti ya kihuni ni nani mbaya au wa kwanza mwenye kuhitaji kuadhibiwa? Je, CCM ina ubavu wa kumuadhibu yeyote?

CCM haina tofauti na mbuzi. Kwani imefungwa kwa kamba mbili, yaani mafisadi na “wasaliti.” Ikikata kamba yoyote kati ya hizi mbili bado itaendelea kuwa mbuzi tu.

Chanzo: Tanzania Daima Juni 29, 2011.

4 comments:

Jaribu said...
This comment has been removed by the author.
Ndugu Nkwazi N Mhango said...

Jaribu hukuwa na haja ya kuchomoa hiyo comment. Anyway you are free to offer what you deem fit.

Jaribu said...

Unajua wakati mwingine napitia hapa usiku wa manane wakati nina usingizi na sipo makini.. Hii comment niliikusudia na ndio niliyoweka hapo chini, lakini nikawepa hapa kwa bahati mbaya. Wengine tunaona aibu kidogo tukichemsha, badala ya kulaumu watu wengine, unlike your average CCM cadre.

Ndugu Nkwazi N Mhango said...

Sasa nimekuelewa. Hamna taabu.