The Chant of Savant

Friday 19 August 2011

Ngeleja na Malima acha utoto


Kwa wale wenye kufuatia mifumko ya kashfa za mara kwa mara nchini mwetu watakubaliana nasi: baadhi ya watendaji hawana hata chembe ya kujisuta wala nia njema na taifa letu. Wanafanya utoto na kutaka watendewe kama watu wazima wakati ni wa hovyo!

Ukiachia kashfa nyingine nyingi ambapo wahusika hawakuwajibishwa wala kujiwajibisha, kashfa ya hivi karibuni ya kukusanya pesa kwa ajili ya kuhonga wabunge wapitishe bajeti ya hovyo ya wizara Nishati inathibitisha hili. Kwanza, inashangaza kuona hata wabunge walioonyeshwa kama wapokea rushwa wamekaa kimya kuhusiana na kashfa hii! Ilishangaza zaidi pale wabunge walipopitisha bajeti ya wizara ya Nishati wala bila kumtaka waziri William Ngeleja na naibu wake Adam Malima kutoa maelezo ni kwanini walikuwa wakikusanya pesa kwa kisingizio cha kuwahonga wabunge. Je kwa kukaa kimya wabunge wamethibitisha ukweli kuwa pesa iliyokusanywa ililenga kuwahonga na hivyo kuridhia kuwa wao ni wapokea rushwa?

Kabla ya kashfa hii kulikuwa na kashfa ya mauaji ya Arusha ambapo jeshi la polisi liliua wananchi wasio na hatia kwenye mvutano baina ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na Chama Cha Mapinduzi. Ni pale CHADEMA ilitaka kuwahamasisha watanzania nchi nzima waiwajibishe serikali kwa kutoshughulikia ufisadi.

Yalipotokea mauaji ya Arusha wengi walitegemea waziri wa mambo ya Ndani Shamsi Vuai Nahodha na naibu wake na mkuu wa jeshi la polisi wangewajibika kuwajibisha au kwajibishwa. Hawakufanya hivyo. Kadhalika, hawakupoteza muda hata kuomba msamaha zaidi ya kujifanya hayawahusu na kuendelea kung’ang’ania ofisi za umma. Hili lilithibitisha watendaji hawa wasivyothamini utu wala haki za binadamu. Ajabu hata polisi waliofyatua risasi Arusha au wanajeshi waliozembea hawakuchukuliwa hatua! Tunajenga taifa la namna gani lisilo na chembe ya kumbukumbu wala huruma? Ajabu wanaotenda madudu na jinai bado wanaitwa waheshimiwa badala ya wezi, wala rushwa na wauaji wakubwa wasiopaswa kuishi achilia mbali kuwa kwenye ofisi za umma wakiendelea kutapanya mali na pesa vya umma.

Wengi wanaojua jinsi madaraka yanavyotumiwa vibaya nchini mwetu hawakushangaa kilichotekea hasa ikizingatiwa kuwa wahusika huwa hawawathamini watawaliwa zaidi ya kuwachukulia kama punda wa kuwabeba watawala na mizigo yao yaani beasts of burden kwa lugha ya kuazima. Je hali hii itaendelea hadi lini? Je wahusika hawajawateka watawaliwa kiasi cha kuwageuza watumwa na hayawani wanaoweza kuua hata kuibia bila kuwajibika? Je umma uende kwa nani?

Si hilo tu, kabla ya kufufuliwa kwa kashfa tajwa hapo juu kulikuwa na kashfa mbili za ulipukaji wa mabomu yaliyoua watu wasio na hatia maeneo ya Mbagala na Gongo la Mboto. Wahusika wakuu yaani waziri wa Ulinzi, Hussein Mwinyi, naibu wake na mkuu wa majeshi hawakujihangaisha hata kuomba msamaha. Je tunajenga taifa la namna gani iwapo maisha ya binadamu yanaweza kuondolewa kizembe na wahusika wasichukuliwe hatua?

Matukio hayo mawili hapo juu ya mauaji ambalo ni kosa la juu sana katika jamii ya binadamu yalianza kuibua hisia kuwa kuna watu wenye ubia na serikali kiasi cha kutoguswa. Wengi tulidhani huu ungekuwa mwisho lakini wapi! Kumbe wasioguswa au untouchable wako wengi!

Turejee kwenye kashfa ya ukusanyaji pesa ili kuhonga wabunge kupitisha bajeti. Je mawaziri husika wanangoja nini hata baada ya ushahidi mwingine kutolewa kuwa walipewa mgao wa pesa hiyo? Ajabu wahusika, walivyo vichwa ngumu na wenye dharau kwa umma, hawakuhangaika hata kujitetea wala kukanusha kuwa walipewa mgao kupitia kwa wasaidizi wao waliotajwa hata majina! Hivi kuendelea kung’ang’ania ofisi ambazo wameishazichafua licha ya kuwa aina fulani ya ufisadi, wahusika hawajui kuwa wanamwongezea mzigo wa lawama rais aliyewateua? Hivi hawaoni kuwa kutojiwajibisha ni kuzidi kumburuza rais kwenye uchafu wao? Je watu wa namna hii wana heshima yoyote kwa rais ilhali wanaendelea kuhatarisha hadhi yake? Je watu wasio na uwezo mdogo tu wa kuona kosa walilotenda wafaa kuendelea kukaa kwenye ofisi za umma? Wahusika wanaongoja nini kuwawajibisha kama wao hawataki kujiwajibisha? Kwanini tunajenga na kuendelea kulea mazoea haya machafu? Je kama wabunge walioingizwa kwenye uchafu huu wameamua kukaa kimya kwa sababu wajuazo, umma nao unakaa kimya kwa sababu zipi iwapo ofisi na pesa inayochezewa ni vyao?

Yaani watanzania tumejiruhusu kugeuzwa mataahira na vihongwe wa wezi wachache wasio na chembe ya aibu wala utu? Kwa faida na sababu gani? Sitaki kuambiwa kuwa wahusika hawana kosa bali katibu wa wizara ambaye naye amelindwa kwa kisingizio cha kupewa likizo. Unampa likizo mtuhumiwa badala ya kumfikisha mbele ya vyombo vya haki ili iweje? Hakuna mbunge anayehoji ufisadi huu wa kimfumo wa kulindana! Je ina maana kosa la kujipatia pesa kwa nia mbovu ya kuhonga ni la David Jairo pekee yake iwapo yeye alikuwa ofisini kupokea maelezo ya waziri na naibu wake? Kama kosa ni lake, inakuwaje waziri na naibu wake wasimwajibishe kabla ya bomu kulipuka kama hawakuwa wakijua? Kama hawakuwa na habari huu nao si uzembe unaotosha kuwaondoa ofisini? Wako pale na wanalipwa kusimamia nini kama mambo yanaweza kuwapita wakiwa hawana habari? Hata hivyo hapa ukweli ni kwamba Jairo, Ngeleja na Malima lao ni moja.

Tukubali kuwa Jairo amepewa likizo ya lazima ili kuchunguzwa. Na hawa wakubwa zake nao wanangoja nini lau kupata hiyo likizo? Kwanini hatutaki kujifunza hata kutoka kwa majirani zetu pale Kenya. Waziri wa Elimu ya Juu wa zamani William Ruto aliposhutumiwa kujiingiza kwenye kashfa na mwenzake wa mambo ya Nje Moses Wetangula, waliwekwa kando ili kuchunguzwa. Ajabu hawa wakenya wanaoona mbali ndiyo eti tunaungana nao tukitegemea kusonga mbele wakati wao wakisonga mbele sisi tunarudi nyuma!

Hivi mawaziri wa Kenya wakikutana na wetu wataelewana iwapo wakenya wanaangalia maslahi ya umma wakati wetu wanaangalia matumbo yao? Bila kujenga utamaduni wa kujiwajibisha, kuwajibika hata kuwajibishwa Tanzania itaendelea kuwa kichwa cha mwendawazimu kwa kila mafisadi, majambazi, mibaka na wezi kuja kujichotea watakavyo kama shamba la bibi.

Je waziri Ngeleja na naibu wake Malima wanangoja nini iwapo wameishachafuka kiasi cha kutosafishika? Kwanini wanamtwisha rais mzigo wao wa dhambi? Wananchi tutafute jawabu na ufumbuzi kama mamlaka husika zimechemsha kwa sababu na nia wazijuazo.
Chanzo: Dira ya Mtanzania Agosti 16, 2011.

1 comment:

Jaribu said...

Yot4e inaanza kutoka juu kwa Rais kushuka chini kwa wateule. Maana wao wana-practice trickle down, nay gushing down ncompetence. Rais mwenyewe kila siku kwenye ziara, mazishi na mambo mengine mepesi yasiyohitaji kutoka jasho, it makes you wonder who is left minding the store.