The Chant of Savant

Thursday 11 August 2011

NIMEGUNDUA DAWA YA KUUA INZI

Pumba za Mlevi Mdanganyika

Baada ya kuona inzi wamezidi kuongezeka wakichafua kila kitu, nimejipa kazi ya kupambana nao. Nimeamua kufanya hivi ili kunusuru maulaji ya walevi. Kwa wale ambao hawajawahi kufikia Uwanja wa Fisi tunapojichana mapupu, utumbo au amfitifi kwa lugha nyingine na maulaji mengine, kuna inzi kweli kweli. Hivyo basi nimeamua kuchonga rungu ili niwasambaratishe inzi.

Nimeamua kuchonga rungu kuepuka kutumia doshi kununua nyundo. Hivyo lazima nibane matumizi hata kama wadanganyika hasa wanywa gongo hawafanyi hivyo kama serikali yao. Naonya. Msianze sema eti nafanya uchochezi. Hasha. Nani hajui kuwa nchi hii inaliwa na kila fala kwa namna na wakati atakao? Anayebishia hili ajiulize mantiki ya kampuni la Usafiri Bongo and Around (UBA) limeuzwa kwa kabilioni kamoja wakati thamani yake ni mibilioni 12? Hii akili au matope? Huu ujanja au ujambazi mbuzi na ufala? Hivi hawa wanaouza mali ya umma kama njegere wana tofauti gani na inzi? Najua maswali yangu magumu kwa mtu mwenye akili ya kawaida kutokana nami kufikiri kigongo gongo na kibangi bangi. Sikupenda kuwa mnywa gongo wala mvuta bangi. Wanaouza mimali ya umma kwa manufaa binafsi ndiyo wamenifanya niwe mvuta bangi na mnywa gongo. Maana hii hunisaidia kuepuka kujinyonga ukiachia kunipa stimu ya kupanga kuwatokea siku moja na kuwabomoa sura zao kwa chupa za gongo.

Turudi kwenye inzi hawa wachafu kama wale niliotaja hapa juu. Si wanafanya ufska wao kiasi cha kujisahau na kudondokea kwenye kanywaji kangu wanadhani nitawaacha. Hawa hawana tofauti na akija Devil Jero Jeuri waliofanya ufuska wao na kuangukia mjengoni. Ingawa wao wamelindana na kupumzishana. Mie hawa inzi wangu nawapiga rungu bila kujali ni wadogo au hayawani. Kwanini niwavumilie inzi wakati wanakunya kila mahali kuanzia chooni hadi kwenye sahani?

Inzi ni wadudu wachafu na hatari sana. Wanaambukiza watu kipindupindu. Kwa wale inzi watu wanaambukiza watu ugonjwa wa kipindupindu mifukoni hata akilini. Nani atakuwa na akili timamu wakati muda wote anafukuzia gongo na ndururu lau aishi? Ni wangapi wamegeuka vibaka na vyangudoa bila kusahau matapeli kutokana na hali hii?
Mie nawachukia inzi wawe hayawani au vinginevyo. Wanakunya hata ikulu hawana adabu hawa tena wanaitana na kupatia uchafu. Hawajui hii ni ofisi tukufu ya rais ambayo Mchonga aliita patakatifu pa patakatifu ingawa inzi wamepafanya pawe pachafu pa pachafu!

Waarabu humuita inzi au afananaye naye Dhubab dhakar yaani mchafuzi wa kila kitu kwa lugha ya kimakonde. Huruka na kutua juu ya yule na kufanya ufuska wake hapo hapo humdandia mwinginie hivyo hivyo hadi anakufa. Wakati akifanya ufuska wake hasahau kunya hovyo hovyo. Huyu ni dhubab dhakar, marhun mkubwa.

Kweli wakati wa Mchonga hapakuwa na inzi ikulu hata kama walikuwapo walikuwa kidogo. Wengine wanasema eti ni kwa sababu nchi ilikuwa imefilisika kiasi cha kukosa ulaji wa kukaribisha mainzi. Yawezekana ni kweli. Ila alipoingia Ali ndiyo usiseme. Inzi walianza kualikana na kujazana kila sehemu. Wanaopamba utawala wanasema eti inzi waliongezeka kipindi cha Ali kutokana na ruksa ambapo ulaji mwingi ulitengenezwa kiasi cha kukaribisha hata kunguru wa india na inzi. Mara alipoondoka wakazidi kuzaliana na hatimaye kujazana zaidi na zaidi. Lazima tufanye mpango wa kupasafisha mahali hapa. Najua rais hapendi uchafu. Naamini ataniunga mkono kusafisha ikulu. Nitamwandikia barua ya kumtaarifu kuwa nakwenda kule kuwapigilia mainzi mbali kwa rungu langu. Mie sihitaji ufagio uchwara na wa uongo wa chuma.

Ukienda Baa unakuta mainzi. Kwenye dala dala nako inzi. Ukienda Airport yamejazana mainzi. Kwenye mbuga za wanyama ndiyo usiseme. Jamani! Kila mahali inzi! Jamani inzi mbona wanatusumbua hasa sisi walevi. Ukinunua mapupu utamuona katua achukue kitu kidogo. Ukikatisha barabarani yuko mgongoni mwako akitaka kitu kidogo. Ukienda maofisini kila unachofanya inzi yupo mgongoni hata mbele yako akitaka kitu kikubwa! Mwe! Jamani nyie inzi mmetumwa na nani yarabi? Mainzi yanapanda hata mashangingi! Haya yatakuwa yanafaidi kodi yetu. Lazima tuyasafishe kuanzia Igunga, Monduli, Bariadi, Chalinze hadi Mara na kwingineko.

Hakuna wanyama na wadudu nawachukia kama kunguru na inzi. Maana, kila unapokwenda kuna inzi. Ukinunua bia yako huyo! Kaisha tua na kuanza kufanya ufuska wake. Tena naona lile inzi lina kitambi utadhani jiheshimiwa! Linavyorukaruka hapa na pale utadhani linafanya kampeni ya kugombea ulaji wa bure ambapo hata makalio hulipwa posho. You houseflies, get out of the house. We are tired of you really. What a heck you are causing!

Kwa vile inzi hawaelewi lugha rahisi, nimeamua kuchonga rungu la kilo kumi ili nitakapowaona natwanga bila kujali kama nitavunja vyombo au nini. Hii ni kweli na si hadithi za Abunwasi wala Alinacha. Mie nitafanya kweli bila kujali nani atachukia wala nini.

Kwanini mainzi yanenepeana wakati walevi tunakondeana wakati yanakula jasho letu? Naona hata kunguru nao wananenepeana utadhani hii nchi ni yao! Kwanini tunafuga wanyonyaji hawa tena wachafu? Yaani tumegeuka jamii ya kunyonywa! Jana baada ya kutoka kupiga gongo nikajitupa kwenye kitanda changu cha kamba. Mbu walivyonishambulia sina hamu. Hii ikiongezewa na kiza na joto ndiyo usiseme. Hata kile kiyoyozi yangu chapa Mzaramo sijui kiliibiwa na nani? Maana sisi wanywa gongo kiyoyozi chetu si kingine bali feni ya mkono.

Mainzi yanavyozaliana siku hizi sina mfano. Kila siku utaona hili likiibuka pale na jingine kule. Kwanini yasipange uzazi? Lo! Sasa naanza kuchanganya! Kwanini mainzi yapange uzazi wakati uchafu upo jaro na yanakula bure? Kwa vile sijapata gongo tangu asubuhi, wacha nitimke kwa mama Betty nikaongeze mafuta tayari kukabiliana na inzi. Inzi mpo? Kaa chonjo bwana rungu naja. Sitaangalia rangi wala ukubwa. Inzi ni inzi kila nitakapomuona natwanga. Laiti wanywa gongo wote wangekuwa na moyo mkubwa kama wangu!

Chanzo: Dira ya Mtanzania Agosti 11, 2011.

No comments: