The Chant of Savant

Tuesday 20 September 2011

Siku mlevi aliponusurika kifo cha bajaj ya ambulansi

Sijui niite zali la mentali au mentali ya zali? Nashindwa kuiita hii ndude bajaj ya ambulansi au ambulansi ya bajaj.

Siku hiyo gongo yote niliyokuwa nayo kichwani ilinitokea puani nikaona nilimuona Ziraili yule mjumbe wa kifo na makucha yake akitaka kuninyakua. Pamoja na kujeruhika kijogoo nilimkaripia Ziraili nikisema aende kwa mafisadi wanaofisha watu bila sababu.

Tuligongwa na kujikuta ICU nikiwa na michupa ya maji hewa na damu bila kujitambua. Badala ya kutundikwa michupa ya gongo si walinitundika ya damu utadhani mimi mumiani! Kweli shida mwanaharamu! Nani alidhani nguli wa gongo kama mimi ningekaa hospitali wiki mbili bila hata kuonja gongo? Aminini nilikaa kule na kuondoka na kunguni. Waweza kuamini tulikuwa tukilala watatu kitanda kimoja? Aminini ilikuwa hivyo.

Turejee kwenye masahibu yangu. Siku ya ajali ya kugongwa na gari la mwishiwa fulani aliyekuwa akiwahi kutanua na dogo dogo zake nilikuwa nimeutwika mma kama sina akili nzuri. Nilipata ile gongo ambayo huwa tunaipima kwa kibiriti. Nakumbuka. Rafiki yangu Shemboza alininunulia mapupu tukapata bangi kidogo ndiyo ngoma ikatoka kwenda home. Kufika maeneo ya Friends Corner na shangingi la shangingi wa kisiasa likanivaa mwanakwetu. Kilichofuatia ni kuletewa ambulansi ya bajaj. Wakati huo sikuwa nimepoteza fahamu. Nilimuangalia dereva mwenyewe aliyekuwa akiendesha hiyo ambulansi na kugundua kuwa hakuwa dereva kitu. Dereva mwenye aliooneka alipata leseni kwa kutoa rushwa kama alivyosema mkuu.

Tuache utani. Huwezi ukaamini kuwa hiki kituko kilitokea karne ya 21 ya sayansi na teknolojia kwenye nchi inayojidai kuwa mbele kimaendeleo miongoni mwa nchi zilizosahaulika katika maendeleo. Huwezi kuamini kuwa hadi ninapoandika yameishawakuta wengi makubwa kuliko haya. Hebu wafikiri jamaa zetu wa Zenj walionyongwa na mafisi wenye meli na maafisa wa bandari walioruhusu mkangafu ule kubeba watu zaidi 6,000. Baada ya kugundua yaliyotokea kwangu na baadaye niligundua kuwa kumbe teknolojia tunayoambiwa inamaanisha kitu kingine kabisa. Sikujua kuwa kumbe ni teke linalokujia toka kwa watawala ambao mie kwa gongo zangu huwaita watu wala watu. Wao wanapanda mashangingi kwenda kutanua na madege kwenda kuchunguzwa afya hasa mafua.

Tuendelee na masahibu yangu ambayo kimsingi ni ya walevi na makapuku wote. Nashukuru Mungu sikunyotoka roho. Baada ya kukaa hospitalini kwa wiki tatu na kuwekewa POP nilirejea nyumbani nikiwa nimepigika. Kwanza wajua maana ya piopio? Hii ni Plaster Of Paris kwa wale waliosoma uganga. Mie niliusomea udaktari lakini nikaamua kukatiza masomo baada ya walimu wangu kunionea wivu kwa nilivyokuwa nawazidi akili.

Mambo ya Piopio tuachane nayo. Baada ya kufika nyumbani ugonjwa wangu uliongezeka baada ya kugundua kuwa kumbe pesa ya kulipia matibabu yangu ilikopwa na mke wangu kwa mpemba muuza genge. Hebu fikiria. Umaskini huu! Yaani mke wangu Cha Utamu anakwenda kukopa pesa kwa muuza genge! Walikubalianaje na nini hadi muuza genge akawa mfadhili wetu. Hili hadi sasa linaniumiza roho hasa nikifikikumbuka mpemba huyo huyo alivyokuwa akitania kuwa siku moja atakuwa mkwe wa binti yangu Mwapombe. Kumbe aliyekuwa akilengwa si Mwapombe bali Cha Utamu aliyegeuzwa Cha Wote na umaskini! Wasomaji nishaurini. Ungekuwa wewe ungefanyaje?

Nakumbuka kipindi fulani baba mwenye nyumba alitaka kututolea vyombo nje. Mke wangu alijivuvumua na kulipa akidai kuwa alikuwa akicheza mchezo wa akina mama wa upatu. Je ni upatu au upato ambapo wenye nazo hupata toka kwa vitu vyetu tusio nazo? Je ni wangapi yameishawakumba au yatawakumba usawa huu ambapo ukapa na ukete vimealikana kutunyotoa roho? Huwa nikiangalia haya yote huwa natamani niwe kama wale jamaa wanaojitoa mhanga kwa kujifunga mabomu na kuwalipua wabaya wao. Mie kwa hasira nilizo nazo, kama nikiamua kuwa gaidi, nitakuwa radhi hata kujifunga bomu kumlipua kuku wako achia mbali wewe. Yaani jitu linatumia vijisenti vyake kumpata mke wa mnywa gongo! Inauma wajameni.

Sisi wanywa gongo tuna masahibu we acha tu. Si juzi jamaa yangu Shemtashua alimtaliki mke wake baada ya kudanganywa na mganga kuwa ana nuksi hivyo akienda naye faragha nuksi itamtoka. Bila kujua kuwa hakuna cha nuksi bali siasa nuksi jimama nalo likaachia na kuambulia talaka. Hayo tuyaache yana wenyewe.

Nirejee kwenye safari yangu ya kwenda hospitali. Baada ya kupakizwa kwenye kijimkweche ambulansi bajaj mara dereva akaondoa bajaj kwa fujo. Kwa vile barabara zenyewe zimejaa mikweche na mashimo, ilibidi akatize mitaa ya Mwembechai upande wa Makulumla. Kufika mitaa ya Kiyungi si akakutana na ngalangala linalotoka Uzuri kwenda Kariakoo likiwa wangu wangu. Kilichofuatia usiniiulize maana sijawahi kusimuliwa. Baada ya kufungwa piopio na kupata fahamu, pamoja na masahibu yangu hasa kukaa muda mrefu bila kuonja, nilianza kujiuliza maswali. Je hali hii itaendelea hadi lini? Je nchi hii ni ya nani kati ya sisi tunaoambiwa ni yetu wakati si yetu?

Hakuna kitu kinanisumbua kama ile pesa niliyolipiwa na mke wangu. Maana pamoja na kudhalilika kote huko, nilikuja kuponea kwa mchua mfipa na si hospitalini nilikotoka na ukurutu na kunguni kibao.

Kama kuna kitu kimeongezeka kwangu licha ya mihasira kutokana na urafiki wa bi mkubwa na muuza genge ni ile hali ya kusikia wanasiasa uchwara na matapeli wakijidai eti wameleta maendeleo. Haya ni maendeleo ya kwenda mbele au kurudi nyuma? Wakati wao wakihomola na kuwa matajiri wa mijumba, migari, mifugo na miakaunti nje, wamenimegea kunguni niliotoka nao kwenye hospitali ya kueneza badala ya kutibu magonjwa. Kibaya ni kwamba unalipia magonjwa haya na kunguni!

Nimalizie kwa kuwaletea habari njema kuwa nina mpango wa kwenda Pakistan kujifunza kujifunga mabomu ili nije niwalipue wanaosababisha upuuzi huu.
Msinichulie serious. Natania.

Chanzo: Dira Septemba 2011.

No comments: