The Chant of Savant

Friday 7 October 2011

Hili la Dowans na vibaraka wao litatufilisi


WATANI wake humwita Jiwe Kubwa (JK). Mie huko siko maana huyu mhusika si mtani wangu bali mtesi wangu. Ataachaje kuwa mtesi wangu iwapo ananifanya ninywe kama samaki kwa kukimbia mazonge na adha zitokanazo na vitu vyake na wenzake?

Zamani nilizoea kulewa kahawa. Siku hizi baada ya mambo kuzidi hasa mgao, nimevamia gongo kiasi cha kuchengua akili yangu. Wakati nikiendelea na masahibu yangu binafsi kama bi mkubwa kuniona mtoto si riziki, walevi nao wana yao. Wanaishi kizani kama mende huku wakiendelea kuaminishwa kuwa hayo ndiyo maisha yenyewe-maisha bora!

Juzi kijiwe kilikaa na kutafakari mambo mbali mbali likiwamo la kunitaka nigombee urahisi ili niwakomboe walevi wahangaika wa Danganyika ya Bongolalalaland.

Yote haya yasingetokea kama siyo mapilato kutangaza kuwa sasa kaya inaamriwa kuwalipa wezi wa Dowanis mabilioni ya madafu. Mwenzenu natamani kunyotoa roho au kuvaa mibomu na kuwavamia hawa washenzi wa Dowanis na watumwa wao wanaotumika kuifilisi kaya yangu.

Sitaki niitwe gaidi. Badala yake sasa natangaza rasmi kuwa nitagombea urahisi ili kuwakomboa wanakaya walevi wanaoendelea kuhangaika. Hatuwezi wote kuwa woga. Lazima nijitokeze kidume niwakabili hawa majambazi wakubwa wapendao kujionyesha kama waheshimiwa wakati ni wezi wakubwa tu wa kawaida.

Nimegundua kumbe nami mlevi naweza kuwa rahisi nikatawala watu na wanyama hata kama ni kwa sanaa bila sera wala uchungu nao! Naweza kuwa rahisi kirahisi kutokana na kuwahonga wapiga kura kahawa na kashata kama siyo ubwabwa kama ilivyotokea hivi karibuni kule Igunguli. Nitashindwaje kuwa rahisi iwapo walevi wanachojali ni hongo badala ya haki zao? Kwani urahisi unasomewa?

Pia siku hizi urahisi auhitaji elimu wala uadilifu bali ujanja na lugha tamu ya kuvulia kura za kula. Kwani nitakuwa wa kwanza kufanya usanii huu iwapo wasanii kibao wamejaa kwenye maulaji hadi kukuu ambako kumegeuka pango la wezi kama Dowanis AIPITIELO, Richmonduli na majambazi wengine kujivulia pesa ya walevi?

Kwa vile kaya yetu imevamiwa na njaa kiasi cha kusababisha utapiamlo wa mawazo, naamini nikiingia jukwaani na mishale na pinde watanipa tu. Nitawatishia kama yule al shabaab Rege alivyowafanyia jamaa wa Igunguli. Mikwara ya Rege ikishindikana natumia ile ya Hayaishi na Ulaya walioamua kuzifyatua ndude zao ili kuwatisha wagawa kura ya kula. Mpo hapo washirika? Mie sitatumia bastola bali mishale na pinde. Mie sitajaza masanduku ya kura za wizi bali madeli ya kahawa na makapu ya kashata tayari kuwahonga.

Katika kampeni zangu nitahimiza kuondoa njaa ya ubongo na maadili nikiwekeza kwenye madili ya uchukuaji wa rasilimali za walevi ili watanue vizuri. Ukiachia mbali njaa ya ubongo, nitapambana na njaa ya matumbo ambayo, kutokana na utawala dhalimu yamegeuka vichwa. Kila mtu siku hizi isipokuwa mimi, anafikiri kwa masaburi na utumbo. Lazima nianze na kampeni za kufufua vichwa nikizika njaa na kupiga marufuku kufikiri kwa masaburi.

Katika kampeni zangu nitawafungua macho walevi kuwa lazima wawe na mwanga badala ya kuishi kwenye kiza kiasi cha bongo zao kujaa kiza. Bila kufanya hivi kaya itaangamia naona halafu kesho Mwenyezi Mungu aniweke motoni bure kwa kushindwa kutumia kipaji change.

Kwa vile naona njaa kila kona na kila mmoja, nitahuburi siasa za ukombozi huku nikiwataka walevi wawajibike kujipigania badala ya kusubiri wajomba toka mbinguni kuja kuwapigania. Najiuliza. Kwanini wengine wameweza kuwatimua wezi wenye madaraka wakati kwenye kaya yetu wanalelewa na kuenziwa?

Ni nani huyo amuabudiaye chatu asimmeze? Jamani, niseme mara ngapi na kwa lugha gani rahisi mnielewe enye walevi wapumbavu? Nani aliwaroga nyinyi ambao kila kitu kiliwekwa wazi mbele yenu na nabii Musa bin Mchonga aliyekataa kushiriki makufuru haya?

Nani aliwaroga nyie mnaodhani kuwa kiza kinaweza kuwa zana ya ukombozi? Tazama mnakazana kuzaa watoto wenye kiza kichwani.

Je, hawa watawasaidia nini baadaye? Heri kuacha kuzaa kama mimi mkapambana na kiza na waleta kiza wanaochota mabilioni kukinunua kiza.

Hakika hizi ndizo siasa uchwara alizosema Rosti Tamu la Aziz ambazo kila uchao zinamlipa mabilioni. Kwenye Kagoda alihomola mabilioni. Baada ya kunogewa akaanzisha Richmonduli akishirikiana na Ewassa. Baada ya kustukiwa akiegeuza kuwa Dowanis ambayo sasa inaingiza mabilioni kila uchao. Ama kweli wajinga ndiyo waliwao!

Wakati upuuzi huu ukiendelea utawaona mashehena waliosheheni njaa na majoho yao pamoja na wachunaji wa kondoo waitwao wachungaji wakipanua midomo yao michafu kutetea uoza huu kwa kuingiza imani zao na ibada za vitu na utajiri. Hawa nawambia wazi kuwa nikipata madaraka nawatia panga bila kujali haki za binadamu au wadudu. Kwani hawa wanaoteswa na mabwana zao si binadamu?

Juzi niliwaona mashehena njaa wakimtetea mama wa kikatoliki aliyevuliwa kilemba wao wakakiita hijab. Acheni njaa na ulimbukeni. Mnamtetea mama yule utadhani nyanyaenu, mnapiga mikelele utadhani nyie ndiyo mliovuliwa hijab. Mbona Nchembela alimvua mke wa shehe nonihino Guest House na hamkumlaani au kwa vile wote ni chama moja?

Nasema wazi kuwa nikishinda uchaguzi sitaruhusi wabunge au Waishiwa kuhongwa na Jero na mic kuhongwa posho za makalio. Serikali yangu itatoa posho ya kufikiri na kuwajibika vilivyo. Mie si mpumbavu wala limbukeni.

Nitahakikisha raslimali za walevi zinaliwa na walevi wenyewe. Hata kama kutakuwa na madili kwenye serikali yangu, yatashughulika na kile Wazungu huita mpowerment na siyo disillusionment kama ilivyo sasa.

Leo sitaki niseme mengi zaidi ya kutangaza rasmi kuwa nataka kuwa rahisi wa kutawala na si rahisi wa kuwaibia walevi.

Naona umeme umekatika. Acha nikavamie ofisi ya Dowanis na kumkata shingo Dowanis mwenyewe. Sitampa nafasi ya kujivua gamba kama danganya toto kwa walevi.
Chanzo: Tanzania Daima Oktoba 5, 2011.

No comments: