The Chant of Savant

Wednesday 18 January 2012

Kibanda anaongelea Mwalimu Seif yupi?


INGAWA mwandishi Absalom Kibanda, kwa sababu anazojua mwenyewe pamoja aliyempamba, makala yake imenivutia kwa kunitoa mafichoni.

Makala hiyo ilitoka kwenye gazeti la Tanzania Daima Jumatano la Januari 11, 2012 ikiwa na kichwa, “ Zama za Maalim hazijakoma Zanzibar.”

Nampongeza kwa hili ingawa sikubaliani na alichoandika kuhusiana na rafiki yake mpya, Seif Sharrif Hamad, Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF) ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar.

Japokuwa hoja za Kibanda si nyingi kiasi cha kushughulisha akili sana, amefanikiwa kumpamba “mtu” wake kiasi cha kusahau ukweli.

Kwanza, si kweli kuwa Maalim Seif ni mwanasiasa ambaye amefanya mengi kuliko yeyote aliyewahi kutokea visiwani. Hii ni kumkosea heshima hata kumchukia, kwa mfano, aliyewahi kuwa rais wa Zanzibar na muungano mzee Ali Hassan Mwinyi ambao viatu vyake vyaweza kummeza maalim Seif ukiachia mbali mentor wake, mzee Aboud Jumbe.

Pili, sijui Kibanda kama alisoma historia. Na kama aliisoma basi huenda hakusoma ya Tanzania na kama alisoma historia ya Tanzania basi alisoma iliyokuwa imepotoshwa kwa makusudi sawa na ile ya kina Rebman, Carl Peters, Mungo Park, Bathromew Diaz na wengine.

Kama amesoma historia ya kweli ya Tanzania basi hakuielewa na kama aliielewa basi ameamua kuipotosha kwa sababu anazojua mwenyewe.

Katika makala hii sitapoteza muda wala mwelekeo kumlinganisha Seif na mzee Mwinyi kwa vile hana hata chembe moja ya sifa wala uzito kukaribia hata nusu yao acha kuwa sawa nae. Ingawa kusifia au kutosifia mtu ni haki ya mtu binafsi, kuna haja ya kuepuka kupindisha ukweli.

Leo makala hii itaaangalia upande wa maanguko na kupwaya kwa Seif. Tunafanya hivyo kutokana na Kibanda kumaliza kazi ya kupamba na kuficha haya tutakayodurusu bila kupendelea wala kuonea.

Huwezi kumlinganisha Seif kwa mfano, na Mwinyi hata kwa chembe kwani Mwinyi hajawahi kuuza chama chake na kuingia mikataba ya siri kwa kutaka maslahi binafsi yaani kupewa uongozi kama ilivyotokea kwa Seif.

Cha mno Seif ametumia chama kutafuta riziki binafsi bila kujali sera na malengo ya chama kiasi cha kuamsha ari ya uasi unaokiandama chama kwa sasa.

Anajiona yu bora kuliko chama na wanachama wake kiasi cha kuwafukuza wanaomkosoa na kumtaka arudi kwenye mstari. Hii siyo sifa nzuri kwa kiongozi hasa wakati huu wa demokrasia na mabadiliko makubwa kisiasa.

Kiongonzi wa kupigiwa mfano, kwa mfano, hawezi kufanya mambo hovyo hovyo hadi kufikia hata kudharau amri ya mahakama na mawazo tofauti na yake. Kibanda aliogopa kulisema hili.

CUF, kwa madudu iliyoifanya juzi, imejiondoa hadhi ya kuwa chama cha wananchi zaidi na kugeuzwa nyenzo ya viongozi wawili yaani Katibu wake mkuu Maalim Seif Shariff Hamad ambaye kimsingi ndiye CUF na CUF ni yeye kwa sasa na Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba kuusaka ulaji hata kwa kusaliti malengo na dira vya chama.

Madudu aliyotenda Seif kwa kuwafukuza wakosoaji amefuta mpaka baina yake na viongozi waliokwishaonyesha wazi wasivyo madarakani kwa ajili ya chama bali wao kuendelea kuongoza kama James Mbatia, Augustine Mrema na John Cheyo kutaja kwa uchache. Kiongozi wa namna hii hana cha mno cha kutoa kwa jamii hata tumpende na kumpamba vipi.

Ukiachia mbali watajwa hapo juu kutumia chama kama NGO na kampuni yao, wamekaa kwenye madaraka muda mrefu.

Chukulia mfano Hamad, amekuwa akigombea urais wa Zanzibar tangu mwaka 1995 hadi sasa huku Lipumba akigombea nafasi hiyo sambamba kwa upande wa bara huku wote wawili wakibwagwa na CCM.

Wale waliogombea nao toka CCM walishakaa madarakani na kustaafu wakati wawili hawa wakiendelea kung’ang’ania usukani wa chama. Seif kwa kulijua hili vilivyo aliamua kupwakia umakamu wa rais ili angalau asiondoke mikono mitupu.

Kibanda ameliona hili ingawa amelipindisha. Hebu angalia nukuu hii: “Ingawa ndani CCM na hata akiwa CUF hajapata kutawazwa kuwa Rais wa Zanzibar kwa sababu za kufitiniwa kisiasa, Maalim Seif ameendelea kuwa mwanasiasa mwenye mvuto mkubwa na wa kipekee kisiasa na kiuongozi ndani na nje ya visiwa hivyo.”

Kama alifitiniwa bila shaka na CCM, imekuwaje akajirejesha huko huko na baada ya kuzawadiwa cheo? Je, alifitiniwa au wenzake wa CCM walimjua alivyo na tamaa ya madaraka kiasi cha kumhonga madaraka kirahisi na akaachia kile alichokuwa akidai?

Ziko wapi ahadi zake kuwa kama kura zake zingeibiwa Zanzibar kusingekalika? Hii maana yake ni kwamba hakuna kura iliyoibiwa kiasi cha Seif kukosa pa kushika na kisingizio akaridhia kupewa umakamu wa rais wakati alikuwa akiutaka urais.

Hebu tuangalie nukuu nyingine ya Kibanda, “Heshima aliyojijengea kama kiongozi wa watu aliye na ushawishi na nguvu kubwa kwanza katika Kisiwa cha Pemba na kisha Unguja ndiyo ambayo kwa upande mwingine imemfanya ajikute akizalisha maadui wengi wa kisiasa.”

Je, kama Seif ni kiongozi wa watu tena mwenye nguvu kama Kibanda anavyosema, ni kwanini hajawahi kuchaguliwa kuwa rais wa watu?

Najua atasema ushindi wake umekuwa ukiibiwa. Kama kweli umekuwa ukiibiwa, hao watu wake wanaompenda na kumheshimu walifanya nini kuondoa dhuluma hii kama kweli ipo zaidi ya kuwa sanaa za CCM na Seif mwenyewe?

Kawaida unapoongoza chama kuelekea kwenye uchaguzi, unaposhindwa unawaachia wengine waingie na mawazo na mipango mipya ya kuwezesha chama chako kunyakua madaraka.

Ukiwauliza wawili tajwa hapo juu hili sana sana, kwa upande wa Hamad, amefanikiwa kuingia madarakani si kwa nguvu za chama wala wananchi bali kukiweka chama rehani. Maana ukiuliza mantiki ya kuteuliwa kuwa makamu wa rais wa Zanzibar zaidi ya ulaji binafsi hana jibu la maana.

Kwa wale wanaokumbuka wale waliopoteza maisha wakipigania haki ya Wazanzibari hasa wapemba, wanashangaa alikopata mshipa na jeuri kukalia kiti hicho akikitosa chama kwa maslahi binafsi.

Hii maana yake ni kwamba damu ya ndugu zao ilimwagika kwa ajili ya kupalilia ulaji binafsi wa Hamad. Kwa msingi huo, baadhi ya wanachama wa CUF wameona mbali kiasi cha kustukia usaliti uliofanywa na viongozi wao na kupanga kuwaengua ili kuepuka kuua chama.

Vurugu na umwagaji damu vilivyoshuhudiwa hivi karibuni kule Manzese vinaonyesha ni kwa kiasi gani viongozi husika walivyoishiwa kwa kila hali chamani mwao. Je, wanangoja nini? Je hawa wanaweza kuleta demokrasia kitaifa wakati wameshindwa kuitekeleza chamani mwao?

Kwa vile makala husika ilikuwa wimbo wa sifa, leo tunaachia hapa kwa kushauri mhusika afikiri upya upande wa pili wa wimbo wake wa sifa.

Chanzo: Tanzania Daima Januari 18, 2012.

No comments: