The Chant of Savant

Sunday 29 January 2012

Nimemkumbuka mzee Yusuf Makamba


Ingawa tulijua kuna siku moja ataachia ngazi, wengi tulipenda katibu mkuu wa zamani wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mzee Yusuf Makamba (Mpayukaji) aendelee kuwa katibu mkuu ili aendelee kuvurunga na kuidhoofisha zaidi CCM. Tutamkumbuka Makamba, katibu mkuu aliyeondolewa madarakani kwa aibu kama mtu aliyekitia aibu CCM. Makamba atakumbukwa kwa kupwaya kwake kiasi cha kuonyesha udhaifu wa kuteuana kwa ushabiki urafiki. Makamba anakumbukwa kwa kutumia sanaa badala ya sera na taratibu katika utendaji wake akilalia sana kusoma na kuitafsiri vibaya biblia ima kutokana na kisomo kidogo au ajenga zake za siri za kisiasa.

Kwanini tumemkumbuka Makamba wakati tukijua hakalii tena kiti muhimu cha mtendaji mkuu wa chama? Tunamkumbuka kwa sababu aliyemrithi, licha ya kufunikwa na kunywea anaonekana kuwa ataleta madhara makubwa kwa chama zaidi ya hata mzee Makamba na vituko na udhaifu wake.
Si uzushi. Katibu mkuu wa sasa wa CCM, Wilson Mukama, aliingia kwa mbwembwe sana madarakani akipania kuwashikisha adabu watuhumiwa wa ufisadi almaarufu magamba. Hawa si wengine bali Edward Lowassa, waziri mkuu wa zamani aliyefurushwa na kashfa ya Richmond, mwanasheria na waziri wa zamani Andrew Chenge almaarufu mzee wa Vijisenti na Rostam Aziz aliyejitoa mwenyewe baada ya kuona ukweli wa shutuma zilizokuwa zikimkabili. Akiwa na siku chache tangu kuteuliwa, Mukama alilihakikishia taifa na dunia akishirikiana na kinara wa vita dhidi ya magamba wakati ule Katibu wa itikadi Nape Nnauye kabla ya kuzimwa, kuwa angewashikisha adabu wahusika. Muulize leo kama amaewashikisha adabu watuhumiwa au kashikishwa adabu yeye. Je Mukama alilazimishwa kujiapiza kuwashughulikia wahusika au alizimwa? Kama alizimwa alizimwa na nani na kwa nini? Je Mukama alitoa kauli hizi ili kutafuta umaarufu kirahisi rahisi au hakujua aina ya maji aliyokuwa akiyavulia nguo? Ni bahati mbaya kuwa sasa CCM imetekwa zaidi na mafisadi hasa magamba kiasi cha kujifanya hamnazo na kutokumbuka kuwa iliwaahidi watanzania kujivua gamba. Chini ya Mukama sawa na Makamba, magamba yanazidi kutuna na kutuna na kutuna na kutuna zaidi hadi kukimeza chama na nchi kwa ujumla.

Ingawa Mukama aliikuta CCM pabaya, sasa anaipeleka pabaya zaidi ya alipoikuta mikononi mwa Makamba hasa kutokana ima na ukimya wake au kuramba matapishi yake kwa kushindwa kushinikiza watuhumiwa wa ufisadi wawajibike kwa kuachia nyadhifa zao kama walivyotakiwa na vikao vya juu vya chama anachoongoza Mukama. Kama Makamba asingekuwa na maslahi na jamaa hawa, nimjuavyo angewabutikia angalau kulinda hadhi yake. Mukama hili limemtoa knockout maskini!

Jaribio rahisi lililoonyesha kuwa CCM ilikuwa pabaya wakati Mukama akiingia ni ile hali ya kuona aibu kumwangukia Philip Mangula katibu wa zamani wa CCM aliyekiimarisha chama, kwenye uchaguzi wa Igunga ambapo CCM iishinda kwa mbinde.

Wengi wanaojua mikiki mikiki na nafasi ya katibu mkuu wa chama tawala wanashangaa ukimya na kupwaya kwa Mukama kiasi cha kumkumbuka Makamba pamoja na udhaifu wake wa kufanya mambo kienyeji na kukurupuka. Je CCM inangoja nini kutafuta mtu mwingine wa kumrithi Mukama ambaye ameonyesha kupwaya tena kwa muda mfupi hasa wakati huu ambapo chama kinahitaji uongozi dhabiti? Kwa wapenzi wa mageuzi, hata hivyo, kama ilivyokuwa kwa Makamba, wanaomba Mungu Mukama aendelee kukalia kiti cha katibu mkuu wa CCM ili avuruge zaidi. Hii itarahisishia upinzani kunyakua dola kwenye uchaguzi ujao.
Wengi wanashangaa. Yule Mukama wa jiji la Dar es salaam aliyeteuliwa na Charles Keenja ametimkia wapi? Je ni yale yale ya siasa na umaarufu wa msimu kama wa akina Augustine Lyatonga Mrema, maalim Seif Shariff Hamad na Keenja mwenyewe? Je Mukama amezibwa mdomo baada ya kuwagusa wasioguswa au amelainishwa kama alivyosema hivi karibuni mwenyekiti wa makampuni ya IPP, Reginald Mengi kuwa wapambanaji dhidi ya ufisadi wamenyamazishwa kiasi cha kutosikika? Yuko wapi Mukama atupatie japo jibu au maelezo? Amezidiwa na Nape ambaye pamoja na kujitoa kimasomaso kwenye vita yake dhidi ya ufisadi angalau amekuwa akijitokeza mara chache kutoa ufafanuzi juu ya mambo muhimu! Ningekuwa Mukama ningejitokeza na kuondoa kiwingu hiki. Maana ukiachia mbali kuonekana juzi akiwa nchini Ujerumani, Mukama kwa sasa ni sawa na hayupo. Hii si kawaida ya mtendaji mkuu wa chama kilichoko madarakani ambaye lazima mara kwa mara atoe ufafanuzi kuhusiana na sera na mipango ya chama chake na serikali yake.

Mukama amepwaya sana kiasi cha kuzidiwa hata baadhi ya wenyeviti wa CCM wa mikoa ambao siku za hivi karibuni walifikia kukipasua chama wakiwapigia debe “mabwana” zao yaani watuhumiwa wa ufisadi. Ajabu Mukama hakujitokeza kuwashikisha adabu. Angewashikishaje adabu iwapo amewashindwa watu wao ambao hawana hata mamlaka zaidi kwa sasa ikilinganishwa na wenyeviti hawa?

Ingawa Makamba alisifika kwa vitu vidogo kama vituko na mambo mengine ambayo hayakuwa muhimu kwa nafasi yake, kwa udhaifu wa Mukama, tuna kila sababu ya kumkumbuka komredi Mgosi Yusuf Makamba almaarufu mzee wa biblia.
Chanzo; Dira Januari 2012.

No comments: