The Chant of Savant

Wednesday 28 March 2012

Baada ya mchezo huu mchafu Tanzania itabaki nini?

SI uzushi wala uchochezi. Tanzania inaelekea pabaya tena sana.
Tangu kuingia kwa mchezo mchafu wa kikundi cha watu tena wachache kujihudumia na kutafuta utajiri kwa kuwauza wenzao, Tanzania si salama ingawa hakuna milio ya bunduki.

Uliza. Yako wapi mapambano dhidi ya ujambazi, ufisadi (ugamba), biashara ya mihadarati, kurekebisha mikataba ya kijambazi ya uwekezaji ambao ni uchukuaji na uwajibikaji? Si siri.
Kwa sasa Tanzania iko mikononi mwa maharamia tuseme majambazi hasa kiuchumi. Imefikia mahali majambazi yaitwayo wawekezaji yanakuja na kutuibia mchana kweupe kwa kushirikiana na wenzetu waroho wachache tuliwaamini.

Uliza uwekezaji kwenye Shirika la Reli uliishia wapi ilipoingia kampuni ya Kihindi iitwayo RITES?
Mijitu inakuja bila hata senti halafu eti inawekeza kwa kuilazimisha serikali iwape mikopo ili waendeleze mradi! Ni wawekezaji wangapi wanakuja na briefcases zao na makaratasi na kurejea kwao wakiwa na magunia ya dola?

Uliza. Ni wawekezaji wangapi hasa kwenye madini wanamiliki ndege na viwanja binafsi vya ndege wanavyotumia kutoroshea madini yetu bila kukaguliwa?
Ni wangapi wanachafua mazingira na hakuna anayewawajibisha?
Hebu zidi kupiga mbizi kwenye uchafu huu uone mengi. Hakuna ujambazi wa wazi kama unaofanywa na makampuni ya simu kwa sasa.

Wanakuja na kuweka mitambo chakavu halafu wanawatoza Watanzania viwango vya juu vya kutumia simu.
Huwa najiuliza. Inakuwaje kupiga simu, kwa mfano, kutoka Canada kwenda Kenya nitozwe senti tano za dola na Tanzania nitozwe senti 27 za dola kwa dakika?

Wakati viwango vya Kenya ni vidogo, mawasiliano baina ya Kenya, Uganda, Rwanda hata Burundi ni bora na rahisi wakati Tanzania ni utapeli mtupu.
Mtu unapiga simu unaambiwa ongeza salio, mara namba ya simu haipo, mara simu inatumika mara hili mara lile.

Kwanini hatusikii upuuzi huu tunapopiga nchi tulizotaja hapo juu kama hakuna namna?
Ajabu ya maajabu, kila mwaka makampuni ya simu yanabadilisha majina ili kuendelea kufaidi msamaha wa kipuuzi wa kodi.

Angalia mahoteli yenu yanavyobadili majina na wamilki kila baada ya miaka mitano ili kuendelea kufanya biashara bila kulipa kodi. Angalia watu wanavyouziana makampuni waliyookota Tanzania kwa bei ya kutupwa.

Anayebishia hili ajikumbushe Richmond ‘ilijiuza’ kwa Dowans kwa bei gani ikilinganishwa na bei ya maandishi tu bila kulipa pesa iliyoianzishia biashara hii hewa.
Leo tunaambiwa kuwa pesa tunayoilipa IPTL, kwa mfano inatosha kununua na kujenga mitambo bora na mikubwa kuliko tunayolipia.

Je, kwanini tunaona kujikomboa ni dhambi wakati tukiabudia maangamizi kama haya ya IPTL na makampuni mengine mengi ya nishati.
Je, hapa hakuna rushwa na ufisadi vya wazi? Je, wahusika hawajulikani? Nani anawagusa wala kuwashughulikia? Tunakwenda wapi?

Imefikia mahali watu wakiuliza ni kwanini uchafu huu unaendelea wakati kuna mamlaka, wanakufa kwenye mazingira ya kutatanisha. Jiulize. Mbunge wetu mmoja alipatwa na nini baada ya kuhoji ni kwanini alikuwa akiona watumiaji wa mihadarati hadharani ambao wangeweza kutuonyesha wanakonunua madawa.

Tufikie mahali tuambiane ukweli bila kuogopana wala kufichana. Bila kufanya hivyo na kubadilika nchi yetu itaishia pabaya.

Ni juzi juzi serikali ya Mali imeangushwa kutokana na hasira za jeshi kushuhudia wauza unga wakiwa ndani ya serikali na serikali isifanye kitu kwa vile wakubwa zake walikuwa wakinufaika na uchafu huu.

Je, sisi tu salama na hawa wauza unga na majambazi wa kiuchumi waliotapakaa nchini mwetu? Je, wananchi wataendelea kugeuzwa mbuzi wa shughuli kila mwaka?
Huwa siachi kusema kuwa Watanzania ni viumbe wa ajabu hata kama hawana mikia au macho kisogoni.
Maana ukiangalia kwa mfano, rasilimali zao zinavyoibiwa, wanavyolanguliwa huduma kama vile umeme, simu na mahitaji mengine na wakaendelea kuvumilia unashangaa hawa ni watu wa namna gani.

Nani kwa mfano anakumbuka na kuhoji ile kashfa ya utoroshaji wanyama iliyotokea Novemba 24, 2010 ambapo ndege ya kijeshi ya Qatar ilifanikiwa kutorosha wanyama mbali mbali 130 kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro?
Je, kama KIA wana uwezo wa kutorosha wanyama hai na wengi kiasi hiki wanashindwa nini kuingiza maelfu ya tani za unga?

Ukitaka kujua nini namaanisha, watafute wafanyakazi wadogo na wa kawaida viwanja vya ndege uone walivyo matajiri wa kutupwa.

Unadhani pesa hii wanaipata wapi kama si kuruhusu uchafu na jinai kama ile ya KIA?
Nenda TRA, Bandari, Uhamiaji. Mambo ni yale yale. Uchafu, uchafu mtupu. Nani anajali iwapo wanaofaidika wameweka watu wao kufanya kazi hiyo? mfano, vituo vyetu vya mipakani vimegeuzwa maduka ya wezi wachache kupitisha wamtakaye na wakitakacho bila kuulizwa na yeyote?

Je, namna hii nchi itakuwa salama? Je, namna hii tunaweza kujisifu kuwa yaliyotokea Mali hayawezi kutokea huko tuendako ambapo wahusika wasiporekebisha hali hii wananchi katika hali yoyote wataamua ‘enough is enough’.

Tumekuwa taifa la hovyo linalowazawadia watenda maovu!
Uliza waliotimuliwa madarakani kwa kashfa wanalipwa pesa ya umma kwa kazi gani zaidi ya kupaswa kuwa mahakamani hata magerezani? Tumegeuka taifa la watenda maovu na waovu kirahisi hivi?

Je, baada ya mchezo huu mchafu Tanzania itabaki nini? Tunaviandalia nini vizazi vijavyo iwapo tunafanya mambo kama mataahira kutokana na kufikiri kwa matumbo badala ya vichwa?
Chanzo: Tanzania Daima Machi 28, 2012.

No comments: