SUNDAY, APRIL 22, 2012

KANUSHO LA HABARI POTOFU KATIKA TANZANIA DAIMA AMBALO LEO LINA KICHWA CHA HABARI KISOMEKACHO "JK.ALINDA MAWAZIRI"






TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI


Gazeti la Tanzania Daima la leo Jumapili Aprili 22, 2012 lina habari katika ukurasa wake wa mbele yenye kichwa cha habari ‘JK alinda Mawaziri’, inayodai kumekuwa na mazungumzo baina ya Rais Jakaya Mrisho Kikwete na Waziri Mkuu Mhe Mizengo Pinda kuhusu hatua inayopaswa kuchukuliwa dhidi ya mawaziri waliotakiwa kujiuzulu.


Habari hiyo imedai kuwa Mhe. Pinda anataka mawaziri wanaokabiliwa na tuhuma waondoke ili kuleta uwajibikaji serikalini, lakini, imeendelea kudai habari hiyo, “Rais Kikwete amesema mawaziri hao waachwe waendelee na kazi zao, kwa kuwa suala hili ni la upepo tu, liachwe litapita”.


Tunachukua nafasi hii kuweka bayana kwamba habari katika hilo hazeti la Tanzania Daima Jumapili si za kweli, bali ni za uzushi na upotoshaji mkubwa.
Mheshimiwa Rais Jakaya Mrisho Kikwete, ambaye alikuwa katika ziara ya kikazi nchini Brazil, amerejea jana Aprili 21, 2012 jioni. Hajaonana wala kufanya mazungumzo na Waziri Mkuu, Mhe. Pinda.