The Chant of Savant

Wednesday 11 April 2012

Tukifanya mambo 10, tuna uwezo wa kulipana kama wabunge


HIVI karibuni madaktari walikuwa wakidai walipwe mshahara wa zaidi ya shilingi 7,000,000 kwa mwezi huku walimu wakidai kiwango chini ya hapo. Nadhani kiwango hiki kilifikiwa na madaktari baada ya kugundua kuwa kumbe wabunge wanalipwa kiasi hiki.
Isitoshe, si wabunge peke yao wanaolipwa mshahara mkubwa ikilinganishwa na wengine. Kwanini, kwa mfano, TRA, benki kuu na hata makampuni ya kigeni yaliyowekeza nchini yana uwezo wa kulipa mishahara mikubwa lakini nchi ishindwe? Je, si ubaguzi kwa wafanyakazi wa serikali kulipwa kwa ubaguzi kama kinachofanyika TRA na Bandari?
Je hiyo pesa wanayolipwa si inatoka kwenye serikali ile ile? Hivi TRA wana utaalamu gani kuliko madaktari kwa mfano kama siyo wizi wa mchana?
Kimsingi, huu ni ubaguzi ambao ni kinyume cha katiba na haki za binadamu. Kuendelea kufanya hivi licha ya kuweza kusababisha matatizo mengi yatokanayo na kutoridhika kwa wafanyakazi wengine, kunasababisha kukata tamaa kwa wale wasiolipwa vizuri au sawa na wengine.
Tujiulize swali rahisi, hivi madaktari na wabunge nani huduma yake inahitajiwa na wananchi kwa kiasi kikubwa kuliko nyingine? Tuzingatie ukweli kuwa wabunge wetu wamekuwa wakipitisha vitu vya ajabu ajabu kama vile kuridhia kuendelea kuwa na mikataba ya kijambazi inayowaumiza watu wetu.
Badala ya kuruhusu watu wetu wasio na hatia kupoteza maisha kutokana na mvutano kuhusiana na malipo ambayo serikali imekuwa ikikataa kutoa kwa kisingizio cha kutokuwa na pesa, tunaweza kufanya yafuatayo na kuhakikisha kuwa wote tunalipwa mishahara kwa viwango sawa ukiachia mbali tofauti kidogo ya baadhi ya wataalamu.
Mosi, kupunguza ukubwa wa serikali, wizara, mikoa na wilaya za kisiasa. si uzushi kuwa pesa yetu nyingi inaishia kwenye shughuli za kisiasa ambazo si muhimu ikilinganishwa na huduma za lazima.
Kwa mfano, kwanini watendaji wa serikali kama vile mawaziri na hata wabunge wajiendeshe wakati sisi tunaajiri madereva kwa wabunge na mawaziri wa nchi ombaomba?
Kwanini wabunge na mawaziri wetu wasijiendeshe kama ilivyo kwa wenzao wa nchi tajiri? Pia kwanini kwa mfano tunakuwa na utitiri wa wilaya mikoa hata wizara tofauti na hali yetu ya uchumi? Kimsingi, vyeo vingi vya kisiasa vilivyomo nchini mwetu havina faida yoyote zaidi yakutumiwa na wenye mamlaka kulipana fadhila au kutoa ajira kwa marafiki, jamaa na waramba viatu wao.
Pili, kupiga vita ufisadi, rushwa, hasa wizi wa pesa ya umma inayoibiwa kila mwaka mawizarani, serikali za mitaa. Kama tutakuwa na serikali yenye kuwajibishwa kwa wananchi kikatiba, hili linawezekana. Mbona nchi tajiri zimeweza?
Tatu, kurejesha maadili ya utumishi wa umma na hata maadili kwa umma. Kwa mfano mtu analala maskini na kuibuka tajiri, hakuna sheria wala mamlaka yanayombana aeleze alivyopata pesa yake. Imefikia mahali hata viongozi hawataji mali zao.
Nne, kupunguza safari za rais na watendaji wake nje na katiba itamke wazi kuwa alipe kodi na watu wake.
Tano, kujenga mazingira ya kufanya kazi kwa bidii kwa kuwatuza wanaoonyesha bidii na mafanikio badala ya kutuza ufisadi na kujuana kama ilivyo sasa. Hivi, kwa mfano, waziri waliotimuliwa kwa kashfa kama ya Richmond, wanalipwa marupurupu ya ustaafu kwa stahiki na sababu ipi kama si kutuza uharifu?
Sita, kuwa na sheria za kutunza raslimali zetu, kuacha kutoa misamaha ya kodi kwa wawekezaji na kuingia mikataba ya kijambazi. Bila kuwa na serikali inayowajibika kikatiba kwa umma, tutaendelea kuibiwa na kikundi kidogo cha watu.
Saba, kupiga vita matumizi mabaya ya fedha na mali za umma. Rejea serikali ilivyofilisi Shirika la Umeme kwa kutolipa bills zake ukiachia mbali kubeba wakezaji majambazi kama Richmond-Dowan na IPTL kutaja baadhi.
Ukienda kwenye ofisi za umma utakuta viyoyozi, simu, magari, maji na umeme vikitumika hovyo na hakuna anayejali wala kuwajibika. Ni mara ngapi magari ya umma yameonekana kwenye shughuli za watu binafsi na hakuna aliyewahi kuwajibishwa? Ni mara ngapi watuhumiwa wa ubadhirifu na ufisadi wanalindwa na serikali? Wako wapi kina Chavda na wengine ambao wanaendelea kukaa kwenye ofisi za umma?
Nane, kujenga utamaduni wa kuwajibika kwa wale wanaovurunda bila kuangalia vyeo vyao wala ukaribu wao na wakubwa. Maana siyo siri kuwa Tanzania kuvurunda kunalipa. unashangaa kwa mfano mawaziri kama William Ngeleja, Adam Malima, Stephen Wassira (bingwa wa usingizi), William Lukuvi, Makongoro Mahanga, Celina Kombani, Mary Nagu, Dk. Hussein Mwinyi, Ezekiel Maige, Mustapha Mkullo, na wengine wengi ambao ama wizara zao zimefanya vibaya au wanakabiliwa na kashfa kubwa ikiwa ya kughushi, wanangoja nini kwenye ofisi za umma?
Hawa wanapaswa kuwajibishwa bila kujali ni marafiki au waramba viatu wa rais. Bahati mbaya rais wetu hana macho wala masikio maana kashfa hizi zimeishaandikwa zaidi ya mara elfu na hachukui hatua yoyote.
Tisa, kupiga vita na kuzuia wahamiaji haramu hasa wale wa kiuchumi wanaoletwa na wawekezaji kwa kisingizio cha utalaamu wakati si wataalamu bali wamachinga wanaokimbia shida kwao.
Nani hajui kuwa Tanzania ina wingi wa matapeli na wezi wanaoingia kirahisi huku wengi wao wakitumiwa na wakubwa wavivu wa kufikiri kufanya ufisadi kama ilivyokuwa kwenye wizi wa EPA na ununuzi wa rada na ndege ya rais?
Kumi, kuhakikisha kuwa mipaka ya Tanzania inalindwa na kutotoa uraia wa Tanzania kama njugu. Hakuna ubishi kuwa mipaka yetu si salama. Nani atailinda iwapo wahusika wako bize kutafuta utajiri wa haraka kama ambavyo tumeona kwenye mikataba ya uwekezaji ambapo wawekezaji wamefikia kuwa na viwanja vya ndege wakitorosha madini yetu na hata wezi wengine kutumia viwanja vyetu vya ndege kutoroshea wanyama walio hao.
Hapa hatujagusia mipaka yetu inavyotumika kuingizia mihadarati, madawa feki na hatari na pesa chafu.
Chanzo: Tanzania Daima Aprili 11, 2012.

No comments: