The Chant of Savant

Wednesday 13 June 2012

Kikwete na aibu za kujitakia



TAARIFA kuwa Rais Jakaya Kikwete amezuiliwa kuwasilisha taarifa ya Mpango wa Kujitathmini wa Umoja wa Afrika (APRM) ni aibu kwa Ikulu yake na taifa kwa ujumla.
Kisa hiki kimemkuta Rais Kikwete kutokana na Tanzania kushindwa kuwasilisha ada yake kwa Umoja wa Afrika (African Union - AU) dola 100,000 kwa mwaka. Tanzania imeatamia deni lake hadi kufikia dola 800,000 ambazo ni malimibikizo ya miaka minane mfululizo.
Inashangaza kuona nchi inayoweza kusamehe wawekezaji na hata wafanyabiashara wezi na majambazi kodi na pesa nyingine, kujisahau kiasi hiki! Pesa iliyoiaibisha Tanzania ni sawa na pesa aliyolipa kashi waziri wa zamani wa Maliasili na Utalii, Ezekiel Maige kununua nyumba.
Pesa hiyo ni tone ikilinganishwa na ujambazi wa EPA au iliyopaswa kulipwa kwa Kampuni ya Richmond.
Ni juzi juzi vyombo vya habari viliripoti kuwa mawaziri wa zamani wa utalii; Maige na Shamsa Mwangunga walilisababishia taifa hasara ya sh 300,000,000,000 ambazo ni mlima ikilinganishwa na vijisenti kidogo vilivyoliaibisha taifa kiasi hiki.
Habari hizi zinaonekana kuwa na ukweli kutokana na wahusika kutokanusha jambo ambalo linafanya zipate mashiko zaidi.
Hadi tunafikia hapa je tatizo ni nini? Ni kutojali au mazoea ya kufanya mambo ya hovyo ya maana na ya maana ya hovyo kama ilivyozoeleka? Inashangaza kuona rais na washauri wake kujiandaa kwenda kwenye mkutano wa AU huku wakijua wazi hawajatimiza wajibu wao.
Je, kwani rais na wasaidizi wake hawakujua kuwa bila kulipa hiyo pesa wasingekuwa na haki wala hadhi ya kutoa taarifa husika? Je, walichanganywa na kupenda kusafiri badala ya kulipa madeni yao au ni yale yale ya kula bila kulipa kama ambavyo imekuwa tabia sugu ya serikali?
Rejea serikali kutolipa mashirika kama TANESCO, mamlaka za maji nchi nzima, kuwakopa walimu huku ikiwasamehe kodi wafanyabiashara wakubwa.
Huu ni ushahidi kuwa nchi yetu ni maskini wa mawazo, lakini si pesa, na rais wetu si makini ingawa ni pigo kwa taifa.
Bila hivyo, Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje hakuwa na kazi tena. Kwa rais mwenye kujali hadhi ya mamlaka yake na nchi, Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje alikuwa amepoteza kibarua siku kashfa hii ilipotokea.
Kwa vile Rais Kikwete si mtu wa kujifunza, waziri ataendelea kupeta huku wanaoona uoza huu wakionekana wabaya na maadui wa Kikwete na waziri husika.
Rejea kitendo cha rais kusaini tangazo la kusudio la kuanzisha Wilaya ya Butiama hapa tarehe 5 Septemba 2011 wakati eneo alilodai kuwa Butiama lilikuwa Nyamisisi. Hii maana yake ni kwamba rais na watendaji wake hawakuwa makini kama ilivyotokea kwenye kashfa hii ya AU.
Nani mara hii kasahau kitendo cha rais kusaini mswada feki kuwa sheria bila hata kuusoma ukiachia mbali ile kashfa ya kumteua mkuu wa wilaya na kumtimua hata kabla ya kuanza kazi?
Vituko vya Kikwete haviishii AU. Nani kasahau alivyowahi kupokea cheki iliyokosewa maandishi na asijue yeye wala wasaidizi wake? Funga kazi ilikuwa ni pale Kikwete alipodaiwa kuidhinisha ongezeko la posho za wabunge halafu akaruka kimanga ghafla na kuwaacha Waziri Mkuu na Spika wa Bunge wakiaibika.
Ukitaka kuandika vituko vya Kikwete unaweza kujaza kitabu. Nani mara hii kasahau Kikwete alivyomteua rafiki na mshirika wake, Edward Lowassa, Waziri Mkuu aliyefurushwa na kashfa ya Richmond pamoja na kushauriwa asifanye hivyo?
Ingawa Lowassa aliachia ngazi, hakuacha kumtaja Rais Kikwete kama mhusika mkuu wa Richmond. Kama huu ni uongo Kikwete anaendelea kumlipa Lowassa kama waziri mkuu mstaafu mamilioni ya shilingi bila stahiki kwa msingi gani? Heri pesa hii ingelipwa AU na kuepusha aibu.
Serikali ya Kikwete inaingia kwenye vitabu vya historia kama iliyoruhusu wizi wa ajabu kwenye wizara zake na serikali za mitaa kiasi cha kumfanya hata Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kuvumilia na kuchoka hadi akalianzisha na kusababisha Bunge kuwatimua mawaziri sita mwaka huu.
Hata katika kashfa hii ambayo kimsingi ilimhusu Kikwete kutokana na kuwateua wale mawaziri, ni ile hali ya kushindwa kuwawajibisha mawaziri wengine waliotuhumiwa, mfano George Mkuchika, Adam Malima na Lazaro Nyalandu.
Hii nayo ni kashfa kwa rais kuwa si makini. Ukitaka kujua undani wa hili, rejea malalamiko ya waziri wa zamani wa Maliasili na Utalii, Ezekiel Maige ambaye hivi karibuni alikaririwa akitabiri kiama cha Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Hata ukichunguza kutimuliwa nafasi ya uenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) kwa Masauni Yusuf Masauni baada ya kutofautiana na mtoto wa kigogo, utabaini kutokuwa makini kwa Ikulu.
Kwa ufupi ni kwamba, rais wetu amepata aibu hii kwa kujitakia mwenyewe.
Chanzo: Tanzania Daima Juni 13, 2012.

No comments: