The Chant of Savant

Wednesday 6 June 2012

Uamsho wamewasha moto mchafu


KUTOKANA na wimbi la kuchoma ma-church huko visiwani Zenj, Kijiwe kimekaa kama kamati maalumU kujadili hali hii huku kikitupia lawama pande zote husika yaani Lisirikali na wanaojiita wana Umsho ambao kimsingi ni uangusho.
Bila kuchelewesha Dk. Mgosi Machungi analianzisha, “Dk. Mpemba naona kwenu kimewaka hadi kikaumana,”
Dk. Mpemba al maarufu Ami anajibu, “Wamaanisha nini na nini hicho kimewaka halafu kikaumana?”
Dk Machungi, “Namaanisha kie kikundi cha mashehena kinachosema eti hakitaki muunganiko wa Danganyika na Zaainzibaa. Badaa ya kuchoma muunganinko kinachoma ma-church ili iweje?”
Dk. Mipawa anaingilia haraka, “Umesema kweli Dk. Mgosi, hawa siyo mashehe bali mashehena. Kwanini hawavai magwanda wakaingia majukwaani na kugombea ubunge ili waondoe kero yao kwa njia ya kisheria badala ya vurugu?”
Dk Mpemba anachomekea, “Wallahi kama wao wajitenga nasi twajitenga tuone. Juzi niliona waraka wasambazwa ukisema eti wapemba tufukuzwe Unguja. Mie nsilamu lakini sikubali ona watu watumia dini vibaya kwa manufaa yao. Ajabu watu wengi wawaunga nkono wasijue watumiwa kam vile tulivyotumiwa na maalimu. Yu wapi sasa wakati ala kuku kwa nrija?”
Watu hatuna mbavu kwa jinsi anavyobukanya kipemba.
Kabla ya kuendelea Profesa Dk. Msomi Mkatatamaa almaarufu Mfilisophe anavaa daruga na kukwanyua mic, “Dk. Mpemba umesema sawa kuwa kama watataka kujitenga nanyi mjitenge nao. Ila kumbuka umoja ni nguvu. Kuhusu huu waraka hata nami niliuona. Nadhani hapa kuna mchezo mchafu wa siasa za magamba at work.”
Anakatua kashata na kujiweka vizuri kwenye benchi na kuendelea, “Wanaotaka kuvunja muunganiko hawaoni mbali. Hivi tukiamua kufukuzana kati ya wabara na wa visiwani si visiwa vitazama kutokana na kuwa na watu wengi walioko bara kuliko visiwani? Je, hawa wachache wasioona hili hawana ajenda ya siri kweli? Ndoto nyingine tena za mchana ni balaa.”
Anapiga tama kwenye kombe lake na kuendelea, “Kwa upande wa pili wa shilingi ni kwamba na lisirikali lina makosa. Badala ya kutumia mbinu za mwituni, kuna haja ya kuruhusu wanakaya wajadili aina ya muunganiko wanaotaka. Maana huu uliopo licha ya kuzeeka, ulikuwa ni baina ya watawala lakini si watawaliwa.”
Akiwa anajiandaa kuendelea, Dk Mpemba anaingilia, “Usemayo Profesa Daktari ya kweli. Mie hapa bara tangu niishi nimezaa sana. Nilipokuja wala sikuwa na duka. Sasa nina maduka. Mkitakafukuza na mie ntenda vipi na mali zangu? Isitoshe sie tu wengi huku bara Wallahi.”
Dk Mgosi Machungi anakwea mic kabla ya Dk Mpemba kuendelea, “Mpemba umesema kwei. Sisi Ushoto tuna mpemba mmoja mwenye duka. Mpemba huyu kwa kupenda kutongoza wake za watu! Kama siyo kumtishia kumpiga zongo huenda angeweza kuhaibu ndoa nyingi.”
Profesa Dk. Mfilosophe anapuuzia mashambulizi dhidi ya wapemba na kuja picha kubwa kuliko hiyo. Anakwanyua mic na kusema, “Kimsingi, sisi kama Kaya hatupaswi kuanza kushambuliana kwa dini au kabila. Hapa kuna kosa ambalo limetendwa na sehemu mbili.
Kwanza, lawama zinapaswa kwenda kwa lisirikali ya mapindu… malizia, kwa kuruhusu hawa jamaa kuanzisha genge la kuhatarisha amani. Ingawa wana haki kisheria kuelezea mawazo na hisia zao, wanapaswa kufanya hivyo kwa kufuata sheria. Waanzishe chama na kushiriki siasa badala ya kujificha nyuma ya majoho. Kimsingi hapa ni vita baina ya majoho na magamba kutokana na wote kuwa na ajenda za siri.”
Anaangalia huku na kule na kuendelea, “Upande wa pili wa kulaumiwa ni hawa wanaotumia imani kuhubiri siasa. Ingawa vitu hivi viwili ni kimoja, sheria zetu zimefanya viwe viwili na tulifanya kosa kukubali. Hivyo, kuanzisha harakati zozote za kisiasa kwa kutumia imani ni makosa ingawa wanasiasa wanatumia dini kufanya siasa kama Ewassa ambaye sasa anasifika kutumia pesa yake kwenye ma-church. Hayo tuyaache.”
Kabla ya kuendelea, Dk. Mbwa Mwitu anachomekea, “Msomi ulipaswa kuwa jaji. Maana unavyopangua hoja na kutoa hukumu umenikuna.”
Kabla ya kuendelea Dk Maneno anaingilia, “Amekukuna wapi?”
Dk Mbwa Mwitu anajibu, “Wewe unadhani amenikuna wapi? Jamani tuache utani kwenye mambo mazito kama haya.”
Profesa Dk. Mfilosophe kapata upenyo. Anachomekea, “Na hii ndiyo imekuwa tabia ya kaya yetu. Watu wazima na akili zao tena wengine wasomi wanafanya uhuni na hakuna anayewazuia. Umesema vema Dk. Mbwa Mwitu. Nilistahiki kuwa jaji. Lakini nani ataniteua wakati simo kwenye mtandao wowote au siwezi kutoa rushwa yoyote?’
Inaonekana ujaji haumpendezeshi Dk Mgosi Machungi. Anakwanyua mic na kulonga, “Tate nane yaekea Dk Mbwa Mwitu humpendi Poofesa Mfiosofe. Yaani achaguiwe jaji kunyonga watu? Hei angeteuiwa wazii kama kijana wetu Jan Makambae. Hamumuoni anavyoanza kutesa? Juzi niimuona na dada yake wakipiga picha ya pamoja kwenye kampuni ya teefoni ya baba yao.”
“Una maanisha ile kampuni ya nonihinotel ni ya baba yao?” Anauliza Dk Mipawa kwa mshangao.
“Nani anajua kwenye kaya hii ambapo kia mtu ni kibaka na anachukua chake mapema?” Anajibu Dk. Mgosi Machungi.
“Dk. Mgosi tuombe msamaha. Unasema kila mtu ni kibaka ukimaanisha na madaktari kama sisi?” Aliuliza Dk. Maneno.
“Simaanishi nyinyi. Hamuoni watu wanavyouza wanyama na kupoteza mabiioni na mkuu hawagusi. Hamjui wanakula naye? Shauri yenu. Sisi tinajua kia kitu ingawa tunamezea.” Anajibu Dk Mgosi Machungi. “Hapo nimekupata vizuri Dk Mgosi,” Alijibu Dk. Mbwa Mwitu.
Dk. Mgosi hakuridhika. “Dk Mbwa huwa sipendi utani hasa kwenye mambo mazito. Wewe unaweza kunipata mimi wakati mimi ni umui wa baba yako au hujui kuwa mama yako tuicheza wote michezo ya kujificha?”
Dk. Mpemba ambaye alikuwa msikilizaji kwa muda mrefu anatia guu, “Yakhe mambo mengine si ya utani jamani. Wallahi mie yaniuma sana kuona watu wanavotaka vunja muunganiko. Hawajui bila muunganiko visiwani kusingekuwa na amani?”
Mambo yalivyokuwa yakianza kunoga si kunguru akamnyea Dk. Mpemba na kikao kikavunjika!
Chanzo: Tanzania Daima Juni 6, 2012.

No comments: