The Chant of Savant

Wednesday 1 August 2012

Rais Kikwete vunja Bunge nawe utimke vile vile




KUNA taarifa kuwa wabunge ingawa si wote wanahongwa na makampuni yanayotafuta kuwekeza nchini. Ukweli huu umefichuliwa na mbunge mwenyewe na si waandishi wa habari wala nani.
Kwa mujibu wa Mbunge wa Rombo, Joseph Selasini, baadhi ya wabunge wetu ni mafisadi wanaowakilisha matumbo yao badala ya wananchi. Wanahongwa udoho udoho na ubuge ubuge kiasi cha kuaibisha hadhi ya nafasi ya ubunge. Bahati mzuri Selasini alipotoa shutuma zake, wahusika hawakukanusha. Hii maana yake ni kwamba alichosema Selasini ni ukweli mtupu.
Selasini alikaririwa akisema, “Mheshimiwa mwenyekiti baadhi ya makampuni ya mafuta yalikuwa hapa Dodoma na kutoa chochote kwa wabunge na hili si kwa upande wa serikali ya CCM bali wabunge wa pande zote tukiwemo wapinzani. Msione watu wanazungumza kwa nguvu hapa kutetea, hawa wamepewa chochote.”
Kwa maneno ya Selasini ni kwamba tuna wabunge wa hovyo na waroho kama mafisi hata mbwa! Yaani pamoja na kulipwa maslahi na marupurupu mengi na makubwa bado wabunge wetu wanajiruhusu kuweka mifukoni mwa watu na makampuni binafsi! Inatisha na kukatisha tamaa.
Ukihesabu pesa inayotumika kumpata mbunge mmoja kwenye uchaguzi na kulinganisha na upuuzi huu wanaofanya, unaweza kuomba kuwepo na mamlaka za kidikteta kama zina udhu.
Ni hasara kiasi gani taifa kutumia pesa nyingi kiasi hicho kuwapa wezi fulani ulaji hata kama siyo wote? Hii ni kashfa iliyopaswa kulivunja Bunge kama ingetokea kwenye nchi zilizoendelea. Kwa vile hii imetokea Tanzania kwenye zizi la ng’ombe nani anajali?
Taarifa zilizopo ni kwamba kuna ufisadi wa kutisha, kutoana kafara na kupendeleana kwenye wizara ya Nishati na Madini. Kama kawaida yake, wizara hii pamoja na ile ya Maliasili na Utalii zimekuwa vinara wa wizi na ufisadi nchini. Nani mara hii kasahau utoroshaji wa wanyama tena hai uliofanyika mchana kweupe huku serikali ikijifanya hamnazo na haijui? Je, hili lilikuwa dili la wazito wa serikali au serikali yenyewe? Hayo tuyaache.
Kwa mjibu wa gazeti hili la tarehe 25 Julai ni kwamba wabunge walipania kuhakikisha wizara hii inagomewa bajeti yake hadi Waziri profesa Sospiter Muhongo na Katibu Mkuu wa Wizara, Eliakim Maswi wawajibishwe kwa ufisadi wao ambao waliulinganisha na ule wa Richmond uliomfurusha waziri mkuu wa zamani Edward Lowassa mwaka 2008. Lakini hili halikufanyika ima kutokana na tabia ya kulindana, kigeugeu cha baadhi ya wabunge, kuhongwa au kukomoana.
Sakata hili lilianza pale mkurugenzi mkuu wa Shirika la Taifa la Umeme (TANESCO) William Mhando na wasaidizi wake waliposimamishwa baada ya kudaiwa kulikuwa na ufisadi kwenye shirika hilo.
Hata hivyo Mhando na wenzake pamoja na kusimamishwa, hawakwenda kimya kimya. Walijaribu kujieleza kupitia barua moja iliyomnukuu Mhando akiwasiliana na katibu wa wizara akikanusha kuvunja sheria yoyote hasa kutangaza mgao wa umeme. Mwanzoni kosa la Mhando ilikuwa ni kutangaza mgawo bila idhini ya katibu mkuu wa wizara. Taratibu limegeuka ufisadi na mengine mengi.
Sakata lote lilianza pale wabunge walipohoji kusimamishwa kazi kwa Mkurungenzi wa TANESCO William Mhando na wasaidizi wake. Ingawa kweli Mhando anaonekana kuwa sehemu ya tatizo, serikali, kimsingi, ndiye mchawi mkuu wa TANESCO.
Kama TANESCO wangeamua kumwaga mtama utakuta kuwa deni la serikali na wizara yake ni kubwa kiasi cha kuifanya TANESCO, kama lingelipwa shirika moja tajiri. Hakuna ubishi kuwa serikali zote ya muungano ya Zanzibar, majeshi na mashirika mengine wamekuwa wakitumia umeme tena hovyo bila kulipa.
Namna hii hata angeletwa mchumi toka mbinguni TANESCO itaendelea kuwa bomu. Ikibinafsishwa italeta tija baada ya wawekezaji watakaokuwa wameipata kuisamehe serikali kulipia ankara zake huku mzigo wakitwishwa walaji.
Suala la TANESCO limeiacha serikali na chama vikiwa hoi na kugawanyika vibaya huku mengi machafu yakifichuka. Mbunge wa Simajiro, Christopher ole Sendeka (CCM) alikaririwa akihoji mantiki ya kutoana kafala na kunusuriana hasa baada baadhi ya wabunge kuja na hoja mfu kuwa waangalie maslahi ya chama badala ya nchi.
Sendeka alihoji: “Mbona katika sakata la Richmond iliundwa kamati iweje hivi sasa isiundwe wakati kosa la Maswi linafanana na la Lowassa?”
Ingawa jibu kwa hoja ya Sendeka lilikuwa la hovyo na kifisadi, ajabu CCM iliridhika nalo na kuendelea kutenda makosa zaidi. Aliyetoa jibu kwa swali na hoja ya Sendeka ni Anne Kilango, Same Mashariki (CCM) aliyenukuliwa akisema, “Tulimtosa Lowassa, baadaye ukweli umejulikana, na sasa makosa yetu yanaigharimu serikali na CCM. Tusirudie makosa yale yale, tuwaache hawa kwa maslahi ya CCM,”
Anna Kilango eti naye huyu anawekwa kwenye kundi la wanaopambana na ufisadi! Huu ni ufisadi wa kiwango cha kutisha. Badala ya anayejiita na kuitwa mpambanaji dhidi ya ufisadi kukaripia ufisadi anauunga mkono kwa kuangalia maslahi ya chama!
CCM itapita lakini Tanzania haitapita. Hili halihitaji shahada ya political science kulijua. Kinachojidhihirisha hapa ni kwamba msemaji ni manafiki anayejitambulisha na wanaopinga ufisadi wakati ana ufisadi kimawazo.
Ni bahati mbaya kuwa CCM imekuwa na wanachama wanaofanana na wafu wawili wanaokokotana. Wameweka mkokoteni mbele ya punda wakitarajia kufika waendako. Watafika, maana kuzima hakuna gharama.
Kuna haja ya wananchi kushikiza wabunge wote wanaohongwa waachie ngazi ili wenye udhu na uwezo wachukue nafasi zao. Yaani tumegeuka taifa la mafisadi, mafisi, majambazi na vibaka hivi hivi! Hakika hili si Bunge bali balaa la kitaifa.
Chanzo: Tanzania Daima Julai 1, 2012.

2 comments:

Anonymous said...

nO cOmmEnt

Ndugu Nkwazi N Mhango said...

Sometimes no comment is a comment in itself. Thanks for your comment.