The Chant of Savant

Wednesday 19 September 2012

Tendwa chagua moja, ukuwadi au ujaji

MATAMSHI ya hivi karibu ya Msajili wa Vyama vya Siasa, John Tendwa, licha ya kuhatarisha amani na usalama wa taifa, ni aibu na pigo kwake binafsi na ofisi yake.
Ni hasara kwa walipa kodi ambao kodi zao zinatumika kumweka ofisini, tena katika hali ya starehe na maisha ya hali ya juu.
Akihojiwa na kituo kimoja cha redio, Tendwa alijigamba kuwa ana uwezo wa kufuta chama chochote hata kama kina wabunge 100.
Hili lilichukuliwa kama tishio linalolenga kuwanyamazisha wapinzani, hasa wale wanaoonekana kuwa mwiba kwa chama tawala. Hii ni baada ya kutokea mauaji ya mwandishi wa habari Daudi Mwangosi na serikali kukitupia lawama Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) wakati ukweli ukijulikana kuwa waliofanya hivyo ni polisi.
Matamshi ya Tendwa na baadhi ya matendo huko nyuma yaliacha maswali mengi kuliko majibu. Je, huyu ni mlezi wa vyama au mlevi wa siasa za chama kimoja anayetumia ufungamano wake na CCM kuitumikia huku akiviua vyama alivyoapa kuvilinda?
Je, Tendwa kuonesha upendeleo si kukiuka kiapo chake cha kutopendelea wala kuumiza upande wowote?
Hii inafanya wengi wapate shaka na ujaji wake unaomtofautisha na mwamuzi wa mpira ambaye pia ni mchezaji.
Tendwa hata angelinganishwa na mwamuzi wa soka, bado hawezi kuchezesha mpira wakati akiwa na kadi ya CCM mfukoni. Mwamuzi wa namna hii, ni wa ajabu maana amejaza kadi nyekundu tupu kwa ajili ya kuwapa timu kinzani. Huu siyo uamuzi wala ujaji, bali ujahili.
Ni vizuri kumpa Tendwa ushauri nasaha wa bure kuwa, lazima atambue na kukubali kuwa vyama vya siasa haviishi kwa hisani ya CCM wala Tendwa, wala polisi, wala rais. Hivyo, kudhani kwa namna yoyote kuviweka rehani ni kujidanganya, tena mchana.
Pia, ni vizuri kumshauri Tendwa aachie ngazi kabla ya kuchafuka zaidi. Maana wale anaopaswa kuwalea na hata kuwaamua hawana imani naye tena.
Hana udhu tena. Aihitaji shahada ya sheria wala fikhi kujua kuwa Tendwa amevunja sheria.
Si lazima uwe umesoma misahafu kama Katiba, Biblia, Korani, Mgana Carta, Mahabharata, Bhavagad- Gita, Shastra, Sri Guru Granth Sahib na Dasam Granth wala vitabu ya akina Socrates, Upanishad au Jean-Jacques Rosseau kujua kuwa Tendwa amevunja sheria, hasa kiapo licha ya kupoteza imani kwa umma.
Wala haihitaji elimu ya juu, bali welewa wa kawaida kujua kuwa “uhuni” anaofanya Tendwa ni balaa kwa taifa kama hatashughulikiwa au kudhibitiwa haraka.
Ni mchezo mchafu na hatari kwa mtu anayeitwa jaji na mwenye kufaidi mahanjumati na marupurupu yatokanayo na hadhi hii kutumia busara ya chama kimoja ndani ya mfumo wa vyama vingi.
Huu ni ushahidi wa kupitwa na wakati na mawazo mgando ambayo hayawezi kutusogeza mbele kwenye jukwaa la jamii na taifa lenye kufuata demokrasia, haki na misingi ya haki za binadamu.
Tendwa anapaswa kujifunza kufikiri na kusoma alama za nyakati badala ya kuishi kwenye sanduku liitwalo CCM. Litamponza na wanaweza kuliponza taifa kwa “busara” yao hii.
Mlezi wa kweli wa vyama vya siasa hapaswi kujiruhusu au kujirahisi kuonekana kama mlevi wa siasa au mtu anayetumiwa na upande mmoja dhidi ya mwingine.
Hii siyo sifa ya mlezi hata kidogo. Hii ni sifa ya kuku anayekula mayai yake. Kuku ni hayawani.
Nisingependa mzee wangu Tendwa ninayemheshimu sana afikie hapo. Wala nisingependa mkunga au mlezi aina ya manesi na wakunga wanaowapiga wazazi kutokana na kutojua hadhi na mipaka ya kazi na nyadhifa zao ukiachia mbali kuwajengea wazazi mazingira ya kutoa rushwa.
Je, ni busara kwa vyama vya upinzani na umma wa Watanzania kuendelea “kumdekeza Tendwa” kama alivyosema Freeman Mbowe au ni wakati muafaka kumwajibisha atake asitake, hata wale wanaomlinda?
Je, ofisi anayoaibisha ni mali yake binafsi na wale wanaomlinda au ya umma? Jibu liko wazi kuwa lazima Tendwa aondoke haraka sana kwa usalama wake na wa taifa.
Tendwa hata kama ni project (mradi) wa CCM wa kuua vyama, anapaswa aondoke ingawa hili kwake haliingii akilini.
Lazima vyama vihakikishe anafunga virago na kwenda kunakomfaa - kwao CCM.
Wengi wenye busara walidhani Tendwa angeona mauaji ya Mwangosi kama uvunjaji wa kutisha wa haki za binadamu ambao usingeweza kuungwa mkono na hata hayawani achia mbali mtu mwenye akili.
Kushabikia ushenzi na unyama kama huu ni ushenzi na unyama wa kutosha unaomuondolea mtu ubinadamu wake.
Lazima Tendwa ajitofautishe na kujitenga na watu kama Said Mwema, Emmanuel Nchimbi na Michael Kamuhanda na wale waliowatuma kutekeleza mauaji hayo ya kinyama na kishenzi.
Lazima Tendwa ajitenge na uhuni na wahuni kwa vile yeye ni jaji na siyo mbabaishaji anayepaswa kulindwa kwa vile kaoa au kuoza kwa fulani ukiachia mbali kuonekana kama ‘robot mtu’ anayetumia mitulinga badala ya akili. Asiwe kuwadi wa CCM.
Hata hivyo, mapungufu ya Tendwa yametuachia somo moja kubwa na kuu: Mlezi na msajili wa vyama hapaswi kuteuliwa na ‘mungu mtu’ mmoja au chama bali vyama vyote.
Hili linapaswa kuingizwa kwenye katiba yetu mpya tunayotarajia kuiandika kama haitachakachuliwa na mabingwa wa kuchakachua waliochakachua kura za uchaguzi uliopita na kutupachikia watu kama Tendwa.
Akichaguliwa na vyama vyote, ataepukana na najisi, utumwa, kashfa, hatari na aibu ya kutumiwa na chama kimoja kama ilivyo. Hii ndiyo njia pekee ya kuhakikisha kuwa kuna uwajibikaji na utendaji haki.
Maana vyama visiporidhika na viliyemchagua vinamtimua wakati wowote. Kwa upande wa Tendwa, kama anapenda siasa basi avue joho la ujaji ajitose kilingeni badala ya kujificha nyuma ya ujaji na kupendelea chama chake kama njia ya kulipa fadhila kwa kupewa ulaji.
Chanzo: Tanzania Daima Septemba 19, 2012.

No comments: