The Chant of Savant

Thursday 13 September 2012

Ushikaji wa Kikwete unalea udini nchini



Zoezi la sensa linaloendelea limetupa mafunzo, na kufichua mambo mengi mojawapo ikiwa ni serikali yetu kutumia vibaya madaraka yake. Kwa mfano, kuna kikundi cha kidini eti kinachosema bila kuweka kipengele cha dini kwenye dodoso za sensa hakitashiriki zoezi hili kana kwamba sensa ni kwa ajili ya kujua idadi ya waumini. Sensa dhumuni lake ni kujua idadi ya watanzania ili kuweza kupanga mipango ya maendeleo kulingana na idadi ya watanzania. Heri wanaopinga kushiriki sensa wangetoa sababu kuwa serikali haiwahudumii ipasavyo kwa vile imegubikwa na ufisadi, wangeeleweka na hata kupata uungwaji mkono. Kwa mfano, wakazi wengi wa vijijini hawana huduma yoyote toka serikalini zaidi ya kuwatoza kodi. Wangedai kujua pesa sensa imetoka wapi na inatumika vipi kutokana na serikali yetu kuwa mahiri katika ufisadi. Rejea ripoti ya CAG kila mwaka kufichua madudu ya kutisha na wahusika wasichukuliwe hatua za kisheria.
Turejee kwenye kikundi kinachopinga sensa. Kikundi hiki chenye kila dalili za kuwa haramu kinakwenda mbali zaidi hata kuwagomesha wananchi eti wasihesabiwe na serikali inaangalia tu! Inashangaza kuona serikali ikipata mshipa wa kuwapiga wapinzani kila waendapo lakini inaogopa kuwaadhibu watu wachache wanaotumiwa na mabwana zao kuichafua nchi. Je serikali inafaidika nini na hali hii? Je kuna wakubwa serikalini walioasisi mpango huu lakini wanajifanya hawajui? Hebu tuangalie kwa mfano maneno ya rais Kikwete.
Akizungumzia umuhimu wa kushiriki sensa na madai ya kuingiza kipengelea cha dini, rais Kikwete alisema yafuatayo, “Katika mazungumzo yangu na baadhi ya viongozi wa Waislamu niliwaambia kuwa naelewa sababu na hoja za wao kukasirishwa na kutokuzikubali takwimu hizo. Vile vile, niliwaeleza kuwa takwimu hizo si za Serikali bali ni za mashirika hayo.”
Je hizo sababu ambazo rais alizifanya siri ni zipi na waliongelea wapi lina na akina nani? Kumbe rais na hawa jamaa wanaelewana na ndiyo maana hawashughulikii? Je huku si kulea udini na upendeleo wa kidini? Rejea alivyoongelea suala hili kwa upole tofauti na alivyowahi kuongelea maandamano na migomo tena baada ya kutoa polisi wakaua na kutesa kama ilivyotokea Arusha mwaka jana na kwenye mgomo wa madaktari. Kwa vile hawa ni wenzake, hatukuona akiwaita “wazee” wa Dar Es Salaam kulaani wapuuzi hawa wanaotaka kujenga chuki za kidini kwa sababu wanazojua wenyewe.
Ingawa rais amewaomba watanzania kushiriki sensa, bado ameonyesha upole sijui au uungwana sijui uvumilivu, anajua yeye mwenyewe na sababu ya kufanya hivyo unaweza kuiona kwenye nukuu hiyo hapo juu. Lakini hii pia inatia shaka. Kwanini afanye uungwana kwa kikundi chenye kutumia lugha za kigaidi lakini ashindwe kufanya hivyo kwa wapinzani wanaofanya shughuli halali kisheria? Je kwa vile Kikwete ni muislamu haiwezi kujenga dhana kuwa anawapendelea waislamu wenzake? Je hawa watu wanapata wapi kiburi cha kushindana na serikali tena katika jambo halali na muhimu kama hili kama hakuna namna na Kikwete kuifahamu? Kwanini wakristo hawang’ang’anii kipengee cha dini au yao si dini? Je inawezekana kuweka kipengele cha dini kwa kusikiliza dini moja? Na hao wasio na dini hizi za mapokeo tunawaweka kundi gani? Nchi yetu ni ya watanzania kwanza waislamu wakristo na wengine baadaye. Wakati tukipigania uhuru, tulifanya hivyo kama watanzania na si kama waislam wala wakristo. Dini zinasajiliwa lakini utaifa hausajiliwi.
Inashangaza kuona watu wakijivika majoho ya dini na kufanya mambo ya kisiasa badala ya kufanya shughuli za kidini. Kwanini wasianzishe chama wakafanya siasa badala ya kujificha nyuma ya majoho na dini?
Imefikia mahali hata baadhi ya watu kuwaumiza wengine kama shinikizo la kupinga sensa. Habari zilizoripotiwa tarehe 29 Agosti toka Shinyana kwa mfano, ni kwamba mtu mmoja aitwaye Esther Zablon allipigwa na kuumizwa vibaya na mumewe aliyetajwa kuwa Ismail Yahya kisa eti alitoa ushirikiano kwa maafisa wa sensa. Kwa serikali inayowajibika huyu alipaswa kuwa somo kwa wengine. Je huyu aliyempiga mkewe kwa sababu ya sensa angefanya hivyo kwa vile mkewe ametoa ushirikiano kwa CCM dhidi ya wapinzani angefanywa nini? Kwa kusindwa kushughulikia watu wanaoleta chokochoko kwa taifa, inajenga dhana kuwa wahusika ima ni wenzake rais au wanamdharau kiasi cha kumfanya aonekane kama mtu wa kuogopa hata vikundi visivyo na kichwa wala miguu. Ni ajabu kuwa anakuwa mwepesi wakushguhulika na hata kuongelea mambo yasiyo muhimu kwa taifa. Rejea alivyoshindwa kutoa tamko kuhusu mgomo wa madaktari akakimbilia kwenye mazishi ya Kanumba. Si ajabu kusikia Kikwete akiongelea mipira ya Barcelona lakini huwezi kumsikia akiongelea migomo iliyotomalaki na kuuliwa na mahakama kwa shinikizo la serikali.
Kwa namna rais alivyoshughulikia suala la kipengee cha dini katika sensa ameonekana kuwa legelege kama alivoonyesha kuanzia kupambana na ufisadi, udini, uvivu, matumizi mabaya ya raslimali na fedha za umma. Je kazi ya rais ni ipi iwapo mambo yanaharibika wakati yeye akiangalia? Anatufaa nini rais Kama huyu ambaye anaishi kwenye dunia yake huku umma ukizidi kuteketea kutokana na kila mtu kujifanya atakavyo? Leo kikundi cha dini kinapinga wazi wazi shughuli za umma. Kesho kitataka hata tubadilishe bendera ya taifa au wimbo wa taifa vinginevyo kitaingia msituni. je namna hii hatukaribishi nyenzo za kulibomoa taifa letu? je rais anapolea udini anauangalia mstakabali wa taifa letu au wa dini yake?
Chanzo: Tanzania Daima Septemba 12, 2012.  

1 comment:

Jaribu said...

Jamaa IQ yake ni ndogo, anafikiria vitu basic tu. Kula, mpira, safari nje, labda na nyumba ndogo. Anatumia dini kujustify his existence.