The Chant of Savant

Thursday 11 October 2012

Sumaye unakaribishwa Kijiweni


 Freddie Tuwahi Sumaye,
KWANZA habari za siku nyingi? Vipi shem Ester hajambo? Maana naona amepotea sana. Nilijaribu kwenda pale Wama kumuulizia wakasema hawana taarifa zake.
Maana baada ya kujua kuwa Wama imejaa wake za vigogo nilidhani naye angekuwa anakula mikuku pale kwa mgongo wa kuwahudumia akina mama wakati ni kujihudumia.
Pia nilikwenda kule mafichoni kwenye ofisi za Fursa Safi kwa Walaji ya Anna Makapu Tamaa. Nako sikumpata. Hayo tuyaache ila msalimie sana.
Leo nimetumwa kukuandikia kukujulisha kuwa umepewa mwaliko wa kujiunga na Kijiwe ili ikiweza tuongee vizuri nami mwenyekiti nikupishe ugombee urahisi. hii ni kutokana na wale uliodhani ni wenzako na kuonesha kuwa si wenzako.
Najua ulidhani kuwa CCM ina wenyewe na wenyewe ni nyinyi usijue wenye CCM sasa ni mafisadi. Nadhani sasa unaelewa tunachosema hasa ikizingatiwa kuwa mambo yamebadilika na kuharibika. Naomba usinielewe vibaya. Ninaposema CCM namaanisha Chama Cha Machakachuaji siyo kile chako cha Mapinduzi ya kuelekea nyuma.
Pia inabidi niseme wazi kuwa Kijiwe kinaamini utajiunga nacho kwa vile, kwa nafasi na tabia yako, hutakuwa kama akina Sam Sixx na Dk Haris Mwakiwembe waliojiharibia kwa kuzugwa na kuzuzuliwa na uwazahili badala ya kuangalia kesho. Najua wewe kwa sasa, kutokana na yaliyokukukuta, unaweza kuona mbali kama umeelewa somo.
Huwezi kuamini kuwa juzi Kijiwe kilikaa na kukujadili kwa kirefu. Kwanza, kinakupa pole kwa kudondoshwa na mama wa kughushi shahada Meri Nyago. Na pili tunakukaribisha kujiunga na Kijiwe ili kuleta ukombozi.
Pia Kijiwe kiliandika waraka kwenda kwa Sumaye ili kumpongeza na hata kukulaumu kutokana na baadhi ya matamko yako.
Mfano, Kijiwe kilikupongeza kwa kusema kuwa wale waliopata madaraka kwa mtutu wa bunduki wanaweza kuishi kwao. Kadhalika Kijiwe kilikulaumu kwa kujiandalia msiba kwa maneno yako kuwa ukitaka mambo yako yakunyokee jiunge na Chama Cha Maulaji (CCM). Wanakijiwe walihoji kama hukuwa umelewa madaraka kwanini sasa mambo yako yamepinda badala ya kunyooka wakati bado uko huko huko CCM?
Kijiwe kilikusimanga kidogo kwa kusema: Mbona Freddie uko CCM siku zote na mambo yako hayakunyooka kwenye kugombea ulaji wilayani mwako? Freddie ndugu yangu hebu nipe siri ya matamshi yako. Je siku ile ulikuwa umeutwika au ndo maroroso ya ukubwa? maana nakumbuka hata jamaa yako Ben alikuwa na kaugonjwa haka ka kujisemea kana kwamba ulaji wake haukuwa na mwisho.
Naona siku hizi amenywea akilindwa na jamaa yake aliyemsaidia kuanzisha mradi maarufu wa HEPA. Umenikumbusha nyodo za Benny yule bosi wako akisema watu wana wivu wa kike asijue anawatukana wanawake! Je, alitaka wawe na wivu wa kiume? Nadhani bila wivu wa kike Meri Nyago asingekuangusha. It is sad and shameful to be defeated by a rookie you groomed.
Did you think that she was warming your chair sir? Again, given that money is now talking and money does talk, whom to blame between you and her?
He who lives by the sword dies of the sword. If you are to join our Kijiwe or Chakudema do it in situ. Pole sana Freddie. Anyway, hayo tuyaache tusizidi kukutia joto bure.
Kijiwe kimependekeza kubadili kauli mbiu yako. Sasa tunataka iwe: Ukitaka mambo yako yakunyookee ondoka CCM uje Kijiweni ili ufundishwe elimu ya ukombozi. Maana kwa jinsi mambo yalivyoborongeka huko CCM ambapo maadili yameuawa na mahali pake wameweka madili yaani ufisi na ufisadi, watu wenye udhu hawawezi kupenya.
Kabla ya kusahau, Kijiwe pia kimenituma nikwambie kuwa ukumbuke kuwa ukiwa na madaraka kila mtu anajifanya anakupenda na kukuheshimu; kila kitu kinakwenda utakavyo. Lakini madaraka yakishakutoka unakuwa kapuku tena nuksi.
Laiti wenzako walioko kwenye ulaji wangeliona na kulijua hili wasingepata yanayokukuta leo huko tuendako. Leo ukiwa na madaraka unaweza hata kuwaweka mke na watoto wako madarakani kama nilivyofanya kwenye Kijiwe.
Lakini siku madaraka yakikutoka hao watu wako watadondoka kama kupe kwenye mgongo wa ng’ombe. Usishangae sasa ukienda pale PPF kuchukua mkopo huwezi ukapewa. Pia kama kutakuwa na viwanja vinavyogawiwa maeneo ya Mtibwa ukiomba sasa huwezi kupewa. Kutokana na hali hii, Kijiwe kiliongoea na mgosi Machungi akutafutie shamba Ushoto ili ujenge karibu na Ben na mfaidi hali ya hewa shwari hasa kwenye maeneo ya View.
Turejee kwenye mwaliko wa kujiunga na Kijiwe. Ingawa tumekupa mwaliko hatuna maana uje kugombea urais vinginevyo unikatie chochote kitu ili nikupishe. Maana juzi nilisikia wanoko fulani wakikupendekeza wasijue kuwa nami nautaka urais ili nile dezo na kujirusha majuu na shosti wangu kama sina akili nzuri.
Unadhani nami sipendi kutembelea nchi za Magharibi angalau naweza kupewa kimwana cha kizungu. Mie nikitembelea nchi za majuu sitakubali upuuzi mdogo mdogo kama jezi na vinyago. Mie nina akili kuliko akina Mangungo wa kileo wanaouuza kaya na watu wake kwa zawadi ya upuuzi. Mimi siko tayari kuuza vito halafu nikaenda kujidhalilisha kuombaomba hao ninaowagawia vito vya Kaya. Anyway, hayo tuyaache.
Pia Kijiwe kimenituma kukwambia kuwa kama kitakupitisha kugombea urais na ukashinda hakitataka nyodo za zama zile ulizoonyesha kipindi kile ulipotembelea kwa Joji Kichaka kabla ya Septemba 11 ukatumia milioni za madafu zaidi 500 na kusema eti ni pesa ndogo hiyo.
Kaka Freddie, naona nimechonga sana kiasi cha kusahau kuwa una majonzi ya kubwagwa na mafisi na mafisadi. Hivyo, naomba kwa taadhima nimalizie hapa kwa kukushauri ujikaze. Maana huo ndio ukubwa hasa baada ya kutema ulaji.
Nawahi ndege kwenda kwenye mkutano wa UN ambako nitapitia zangu Ukanada lau nione kama watanijalia kibuti cha kuchezea kandanda. Du! Kumbe sijala! Njaa bwana!
Chanzo: Tanzania Daima Oktoba 10, 2012.

No comments: