The Chant of Savant

Tuesday 23 October 2012

Tatizo letu si udini, bali uduni


BAADA ya kunuka au kuumana hivi karibuni kwenye kaya yetu ya amani, mzee mzima nimeona nitoe busara na elimu bure ili kuepuka kujitia kitanzi kijinga na kipofu.
Laiti ndata wasingekuja Kijiweni na kutulipulia mibomu yao ya michozi wadhani ningenena?
Ningewaacha wamalizane kwa vile wamefugana na kufuga ujinga na ujanja ujanja wao wenyewe huku wakitudharau sisi ambao hatuhusiki na ligi yao ya kuaminisha walevi imani zao.
Ni juzi tu watoto wawili wameonesha utoto wao na ushirikina unaoashiria mafunzo mabaya kutoka kwa wavyele wao.
Si mitoto mitukutu ilibishana kuwa mmojawapo akikojolea msahafu atageuka mjusi au kufa. Kutokana na ukosefu wa busara si mitoto ikaamua kufanya kweli. Wallahi naapa angekuwa kijogoo wangu siku hiyo ningemfungia kwenye gunia kwa muda ili ajifunze kufikiri.
Nisingekurupuka na kuanza kuchoma ma-church wala kudhani kuwa Manaswara ndiyo maadui zangu. Nisingefanya hivyo kwa vile adui alikuwa nyumbani mwangu saa nyingine mimi mwenyewe kumfundisha mwanangu mambo yasiyoingia akilini.
Haya ya watoto tuyaache. Huo ndiyo utoto wenyewe. Leo nalonga na wakubwa wenzangu hasa wale walioshika maulaji na madaraka kulea ujinga umaskini na ufisadi kiasi cha watu wetu kuanza kuwa na imani mfu na hatari.
Laiti watu wetu wangelikuwa wamepiga shule wangejua kuwa kwa mfano misahafu ni makaratasi yaliyotengenezwa na binadamu ili kuwawezesha kujitawala vizuri.
Wangejua kuwa miili yao ina thamani kuliko makaratasi. Wangeoogopa hata kuchoma vibaka kuliko kuogopa hata kuwa tayari kutoana roho kwa ajili ya makaratasi.
Kijiweni tulishangaa kusikia eti watu wanafia misahafu. Hawakusoma hawa? Huwezi kunajisi misahafu. Ukijitahidi kufanya hivyo utanajisi kitabu lakini si ujumbe wa Mwenyezi Mungu Subhana Wa, taala. Misahafu siyo tabu bali ujumbe wenyewe.
Kwani mnadhani kipenzi chake Allah Sayyidna Muhammad (SAW) alikuwa juha kama nyinyi siyo? Mnajua ni kwanini hadi anafariki hakuwa ametoa idhini ujumbe wake uandikwe kwenye makaratasi zaidi ya mioyo?
Alichelea uvivu wa kusoma kusababisha watu waache kuhifadhi na badala yake wategemee matabu ambayo sasa yanawagombanisha.
Mnadhani Mtume alikuwa zoba kama nyinyi siyo? Kwanini hakuacha amejenga misikiti ya bei mbaya ilhali alijua hekalu la mfalme Suleiman? Niwasaidie, alitaka dini isiwe mzigo bali nyenzo ya kuwafanya watu kuishi kwa furaha na si karaha na kuchukiana. Ukimchukia mwenzio elewa huna dini tena.
Kweli aliyewaita Bongolaland hakuwaonea. Mnagombea nadharia huku mkiogopa hata kugombea mambo yanayowahusu kila uchao? Mbona hatuoni jazba kwenye kupambana na ufisadi na dhuluma?
Ni walevi wangapi wanalanguliwa na wenye mbavu za mbwa mnazoita nyumba ambao wengi wao tena huapa kila mara bila kujali kuwa wana dini? Je, wezi wa namna hii wana dini au mauza uza? Nikimuona mama mwenye ubavu wa mbwa wangu anavyoapa hovyo hovyo na matendo yake nachukia hizi imani kusema ukweli.
Leo mmeruhusu wahuni wahuburi maangamizi na matusi hata bila kuwaonya! Hao mashehena wanaojifanya walimu na magwiji wa dini hasa Ugalatia walisomea wapi kama siyo kuendeshwa na njaa? Wengi hawana hata kazi achia mbali elimu zaidi ya kupiga mikelele.
Mbona hakuna mahali mtume alihubiri ubovu wa Baibulo la moyo wa chuluka jamani? Si aliikuta na kuiacha? Msitupigie kelele na uongo na ujinga wenu.
Mnadhani tunapenda hiyo mikelele na mikesha yenu? Tafuteni kazi au njooni Kijiweni tuwape misheni ya jinsi ya kupambana na ukwe.. na ukapa huu tulio nao.
Tukikwambia kuwa tunapata bangi ili kuondoa mawazo mnatuona makafiri wakati nyinyi ni wabaya kuliko sisi.
Maana bangi zetu tunavuta wenyewe wala hatulazimishi na wengine kuvuta bangi zetu kama nyinyi.
Hivi kama mwili wote ungekuwa sikio jicho lingekuwa wapi? Kila mtu anatuhubiria uzuri wa dini yake wakati tunaona matendo yao ya kutisha.
Kama mmeshindwa kutatua tatizo la kitoto kama hilo mtatatua matatizo yetu au mnataka kutuingiza kwenye matatizo yenu.
Nyinyi mnapata wapi? Kwanini mnatuletea bidaa mchana kweupe halafu mnataka kutumia bidaa zenu kutugawana. Mshindwe na mlegee nasema.
Wabongolalalanders wana matatizo yao mengi. Wanakabiliwa na ukapa na ukwe.. We stop! Wanasumbuliwa na ufisi na ufisiahadi na siasa za Uhujumaa na Kujimegea.
Kwanza, wengi wa wabongolalalander hawana dini na kama wanayo basi si nyingine bali kutafuta utajiri.
Hamuwaoni wale wachunaji wanaojiita wachungaji au mashehena wanaojiita mashehe. Shehe aweza kuhubiri vita na upuuzi au mchungaji miujiza na kuwadai watu sadaka? Acheni njaa zenu na wazimu wenu tujenge kaya.
Juzi nilisikia wajinga fulani wakisema eti Bongolalaland inatawaliwa kwa mfumo Christ! Toba! Mfumo Christ chini ya shehe! Mnamdanganya nani jamani? Mijitu iliyolewa chuki eti inasema lazima tutangaziane vita! Hivi vita mnaijua au mnaisikia?
Tukianza vita wajua tutakufa si kwa matundu ya risasi bali njaa? Mijitu yenyewe makapuku ya kunuka?
Hamna tofauti na mipumbavu inayokula nyama kila siku halafu ikaanza kulalamika eti haipati maharage.
Wenye nazo wakianza kupanda mipipa kwenda kuishi ng’ambo nyie mtanukia kwenye mbavu zenu za mbwa.
Hivi umaskini au maradhi na ujinga vinajua dini? Mbona kwenye mbavu za mbwa za kupanga hambaguani isipokuwa kwenye vichwa vyenu wana hizaya nyie?
Jamani tupeni fursa tupambane na matatizo ya kweli badala ya haya ya kuumba.
Tuondolee mbu na uvivu wenu wa kufikiri jamani tupambane na umaskini tuliotengenezewa na mafisadi ambao dini yao ni utajiri. Tena kabla ya kusahau.
Mbona mafisadi wote wana dini moja ingawa majina yao ni ya Kizungu na Kiarabu?
Waijua dini ya mafisadi? Inaitwa Almight Money bin Senti bin Fwedhaa. Wamjua Mungu wao?
Matumbo na tamaa zao. Leo mnajitia kiranga halafu ndata wakiamua kuwatia adabu mnaanza kulalamika. Acheni mauza uza tufanye mambo ya maana.
Acha niwape vipande vyenu. Tatizo la Kaya yenu si dini bali uduni na ujinga. Nasikia mibomu. Sijui nani kakojolea nani tena?
Chanzo: Tanzania Daima Oktoba 24, 2012.

2 comments:

Anonymous said...

aise unachafua hali unaweza ondowa hiyo msg hapo

Anonymous said...

msg gani iondolewe