The Chant of Savant

Tuesday 29 January 2013

Maoni yangu; Mbwa wa rais awe rais wa mbwa wote


BAADA ya walevi kupewa nafasi ya kutoa maoni yao juu ya kuandika Katiba Mpya, wamekuja na baadhi ya mapendekezo ambayo yatafanya taifa letu kuwa la pekee duniani katika utawala na ulaji bora.
Kwa vile hatukupewa nafasi kutoa maoni mbele ya Tume ya Walibora kutokana na kutokuwa na uzito wa kutosha, nimetumwa mzito wao niende kule kutoa maoni yangu na yao.
Tofauti na wazito wenzangu wenye maulaji yao, mie sitatoa maoni kama mimi bali nitawakilisha walevi wote. Pia nitakapokuwa nikitoa maoni vyombo vya umbea na habari havitaripoti kwa vile sina uzito wa kujaza kurasa zao.
Hivyo, nitatoa maoni yangu, ya bi mkubwa na walevi wenzangu. Wale walevi wakubwa watatoa maoni yao kikubwa wakati sisi tukitoa yetu kichovu. Katika kutafakari jinsi katiba inavyopaswa kuandikwa, wanakijiwe wamekuja na maoni yafuatayo:
Mosi, kama alivyosema Joni Malisera, ulaji wa rais usiguswe, tunasema uongezwe hadi kuruhusiwa kushea madaraka na bi wakubwa zake. Kama wanashea bedroom kwanini wasisheee na madaraka? Hii itasaidia kuondoa lawama kwa bi mkubwa na kufanya mambo kwa kificho.
Mfano, kama first lady atakuwa rais mwenza, hatakuwa na haja ya kujificha kwenye Asize au NGO ili kuweza kutengeneza mshiko na kupata ujiko. Hakutakuwa na malalamiko hata atakapopokewa kwa mizinga ishirini na moja na zuria jekundu.
Walevi wameona hili liwe hivi ili kuepuka matumizi mabaya ya madaraka ambapo bi mkubwa anaweza kuonekana kama mwizi na mfujaji wa madaraka na njuluku za umma asiyelindwa na katiba kama wengine. Nani anataka unyemelezi iwapo katiba inaweza kuondoa hili? Nani hapendi kuona kidosho wake aki-enjoy maulaji yake?
Pili, walevi wanapendekeza kuwa vitegemezi vya rais navyo viwe rais wa vitegemezi vyote kwenye kaya. Hata mbwa wa rais awe rais wa mbwa wote na viatu vyake viwe rais wa viatu vyote.
Hii itaondoa uwezekano wa vitegemezi kuiba sana kwa vile vinajua havina madaraka kikatiba. Pia, rais awe na mamlaka ya kutumia rasilimali zote za nchi atakavyo. Hili litaondoa kadhia kama hii tunayoshuhudia kule Ntwara ambapo badala ya kulikomboa taifa gesi inataka kulikomoa.
Tatu, walevi wanapendekeza rais kuwa anaandamana na baraza zima la mawaziri, wabunge hata marafiki na jamaa zake kwenye ziara zake ughaibuni ili kuonesha ufahari wa kaya yetu.
Pia, rais ahakikishe anatumia muda wake mwingi madarakani kufanya ziara ughaibuni ili kuomba mshiko wa kutosha kuwalisha walevi na mwingine wa kubakiza kule Uswizi kwenye akaunti zao.
Hili litaepusha watu wa karibu naye kuiba kwa tamaa wakiogopa kukamatwa kwa vile watakuwa wanalindwa na katiba. Pia, orodha ya watakaokuwa wanaandamana na rais kwenye matanuzi iwe top secret.
Uzoefu tulioupata kwa Joji Kichaka Obamiza ni walikoruhusu bangi ivutwe kisheria, ni kwamba ukihalalisha baadhi ya jinai, unapunguza ushabiki na ushiriki wake. Hivyo, kwa kuwapa maulaji kisheria walaji wote walioko mgongoni mwa rais, wataweza kula kistaarabu na si kifisi kama ilivyo sasa.
Pia, rais aruhusiwe kuandamana na waganga wa kienyeji wa kumkinga na maadui hasa usawa huu ambapo maadui wamegundua uchawi wa polonium. Hata mawaziri waruhusiwe kuweka tunguli kwenye magari na ofisini ili kufanya kazi bila hofu ya kurogwa au kupigwa zongo.
Walevi wamependekeza kuwa rais asilazimike kutaja mali zake kisheria. Kwani mali za rais ni top secret ya usalama wa taifa. Hata taarifa na hali ya afya yake isitangazwe kwa vile wachawi wanaweza kumroga bure. Hata akianguka asiripotiwe.
Tano, rais asilipe kodi. Akilipa kodi atakuwa na ubahiri wa kuzitumia na kufanya nchi ionekane kama ya mabahiri. Sorry achia hapo. Uzoefu umeonesha kuwa marais wanaolipa kodi huwa mabahiri katika matumizi. Mfano, hawaendi kutanua nje, jambo ambalo hufanya nchi zao zisiheshimike hasa ughaibuni.
Pia, imebainika kuwa marais wanaolipa kodi huwabania hata ndugu zao kiasi cha kutowapa ulaji hasa vyeo vya kujuana kulipana fadhila na mengineyo. Hili huchangia kwa rais kuchukiwa na ndugu zake. Hivyo, walevi wasingependa rais wao abanwe kiasi cha kuwabania ndugu zake na waramba viatu wake kiasi cha kuchukiwa bure.
Sita, walevi wanataka rais awe na mamlaka kuliko masultani na wafalme wa Kiarabu ambao hutanua sana kiasi cha kuzoa sifa kuliko nchi yetu.
Hivyo, rais atapaswa aruhusiwe kisheria kwenda benki kubwa na kuchota kiwango cha fweza atakacho kwa ajili ya hata matumizi binafsi.
Hii itaepusha aibu na kashfa kama vile HEPA. Hakutakuwa na haja ya kuibia benki kubwa wakati anao uwezo wa kwenda au kuagiza uchotaji wa ndalama atakazo. Wasiojua ndalama ni njuluku.
Saba, rais aruhusiwe kikatiba kuwa na idadi yoyote ya nyumba ndogo atakazo kama alivyowahi kusema mwandishi mmoja aitwaye Plinsi Bagenda kuwa kupenda wanawake ni ujogoo na sifa ya Kiafrika. Walevi wamepata sayansi hii ya kumfurahisha rais kutoka kwa mfalme Mswatie wa kule Uswazini.
Nane, ili kuepuka kumchukiza, rais awe Jaji Mkuu mwenye madaraka ya kuwahukumu kifo watakaofanya u-babu-seya wa kunyemelea totoz wake. Hii itamfanya rais awe na furaha na asiwe na hofu, hivyo, kutawala vyema.
Tisa, kwa vile kumekuwa na viherehere wanaowaandama bi wakubwa zetu kuwa hawakupiga skuli, tunataka katiba itamke wazi kuwa si lazima bi mkubwa kuwa msomi. Hii itaondoa aibu ya wahusika kuona aibu pale wanapokuwa ni wale walioogopa umande kama bi mkubwa yule ambaye akisoma hotuba za Kiingereza hutoa jasho kama vile anapiga push ups.
Kumi, rais awe na mamlaka ya kutoa adhabu ya kifo kwa yeyote hasa wale wanaomchokonoa. Awe na uwezo wa kuamuru ndata kupiga mtu risasi bila kuhitajika kutoa maelezo au kushitakiwa. Hii italeta nidhamu ya hali ya juu. Ila ndata wasiruhusiwe kuwabughudhi watu wa mihadhara kwa vile wanafundisha madili mema.
Onyo: Power tends to corrupt, and absolute power corrupts absolutely. Great men are almost always bad men. Tafsiri kesho! Kumbe bangi na gongo vimeniishia! Ngoja niwahi kwa mama muuza nipate misokoto kama mia hivi!
Chanzo: Tanzania Daima Januari 30, 2013

No comments: