The Chant of Savant

Wednesday 23 January 2013

Tulivyojinoma Paris Ufaranseee!


Najua habari hii haitawafurahisha walevi walio wengi hasa wanaopondwa na matatizo ya ukapa wa kutengenezwa na sisi wenye maulaji yetu. Wapo watakaoniona kama najidai na kuwakoga. Hawa nawashauri wakajinyonge maana kutesa ni kwa zamu. Wapo watakaoniona kama limbukeni na mtu wa kushangaashangaa. Pia, wapo watakaoniona mtu wa watu na wa maana hasa wale wanaoandamana nami kwenye matanuzi yangu. Wapo watakaoniita Vasco da Gama yule habithi wa kireno aliyekuja pwani yetu akavamia miji yetu na kupora na kuishia zake Ureno. Yote poa tu mradi kelele za mpangaji hazimnyimi usingizi mwenye nyumba kama alivyowahi kusema jamaa yangu Njaa Ka... we koma! Wapo watakaoniona kiherehere kama vitoto vya shule vinavyopachikwa mimba kama alivyowahi kusema mkulu.
Kwa vile mimi ni kichwa maji nisiyejali wala kusikia, sasa nawapa utamu wa jiji la Paris. Wenyewe wafransii huliita Pari au Parie. Sisi tuliosomea hapa huwa tunasema kwa kifransii, “Paris est la mere de tous capitales mondiale.” Yaani Paris ni mama wa majiji yote duniani.
Hakuna kitu kilinichekesha kama bi mkubwa wangu alipotaka kubonga kifransii kwa lafudhi ya ki-matching guys. Badala ya kusema Bonjour Monsieur Presidaa alisema, “Banjua plizidaa,” Ilibidi mwenyeji wetu acheke kwa chati kama vile alifurahi wakati alikuwa akishangaa inakuwaje bi mkubwa hakupiga shule angalau ya kumwezesha kuzinyaka concepts nyepesi haraka kama salamu. Watasha huwa hawana dogo. Si alinipa laivu kuwa kwa vile amegundua kuwa bi mkubwa wangu hajapiga shule hivyo angempa nafasi kwenye shule moja lau apigwe msasa. Nilivimba kwa hasira ingawa nilichekacheka kama kawa. Huyu angejua bi mkubwa wangu asivyopenda kusoma asingeniudhi kwa kutoa wazo kama hilo. Asome kupata nini iwapi NGO yake inamuingizia mshiko wa kutosha kiasi cha kuajili wasomi wanaomtumikia kama mke wa mfalme? Wenzetu bado wanadhani elimu ni ufunguo wa maisha. Hii ni kwao. Kwetu pesa na mamlaka ni ufunguo wa maisha. Simpo! Nilimjibu nini Monsieur Normal? Top secret as usual.
Twende kwenye mada ya mose wa lero. Kama kawa, niliondoka kwenye kaya nikiwa nimeandama na bi mkubwa ili naye akashangae shangae na kujipiga viwalo vipya. Yeye pia aliandamana na mashoga zake ili nao wafanye first shopping bab kubwa. Kitu kimoja kilimkera bi mkubwa hadi akanilalamikia ingawa niliogopa kumwambia rais kwa vile huu si ustaarabu wao. Kilichomkera ni ile hali ya kwenda kufanya shopping kwenye mitaa ya Rue St. Honore, Loire Valley,Mont St. Michel , Faubourg du Roule, Marais Republique na mingine mingi yenye majina magumu bila barabara kufungwa kama Uswazi. Bi mkubwa na mashoga zake waliwaacha hoi wafaransee kwa kulipa cash tena kwa dorali na si madafu. Hakuna mtaa niliupenda kama ule wa Marais Republique. Nina mpango wa kununua bungalow pale ili nikistaafu nikumbuke urais wangu wa kijiwe. Hayo tuyaache.
Pia wapo jamaa zangu ambao sikutaka watajwe kwa vile walevi wanaweza kuanza kuhoji uhalali wa kuandamana nao. Najua hapa wanoko wataanza kusema niliandamana na washikaji zangu, vitegemezi na nyumba ndogo. So what? Kutesa kwa zamu na maulaji siku hizi ni mali ya familia. Au siyo? Hivyo, wale wanoko waliongojea kusikia majina ya nilioandamana nao kwenye utalii wangu jijini Paris walie na kusaga meno. Mie siyo kama akina Mchonga waliozoea kutaja orodha ya watu waliokuwa wakiandamana nao. Hivyo, niliandamana na walaji wangapi na akina nani ni top secret. Tusameheane. You know what? Ukila na kipofu usinshike nkono.
Wengi wanauliza kwanini nilipenda kutembelea jiji la Paris. Kwanza Paris ni karibu na Uswizi hivyo akina Mbwa Mwitu na Mgosi Machungi wenye vijisenti vyao Uswizi waliweza kuchukua High speed train na kuchungulia akaunti zao haraka haraka. Wengine walipata fursa ya kufungua akaunti mpya kwa vile tulishaonyesha wazi kuwa hatutakubali kusikia wambea wanaosema eti tuwakamate walioweka vijisenti Uswizi wakati ni maendeleo kwa kaya.
Sababu nyingine ya mashiko iliyofanya nitembelee Fransee ni ukweli kuwa nilisoma na bwana nkubwa Francois Hollande kwenye chuo kikuu cha L’ Institut d'études politiques de Paris (Paris Institute of Political Studies), wakati ule nikisomea mambo ya siasa baada ya kutoka zangu Kivukoni. Pia yeye ni rika langu ingawa yeye ni dogo kwangu kwa miaka minne. Kitu kingine kilichofanya tuwe washikaji na huyu jamaa ni ile hali ya kupenda totoz wakati ule tukisoma. Nani angeamini kuwa bado mshirika wangu Hollande anaishi na mchumba na si mke? Yeye ni mtu wa totoz. Huwa hakawii kupenda na kuacha. Haya ndiyo mambo ya kisasa. Sitaki niseme mengi ingawa hayo machache yanatosha kuonyesha ushikaji wetu ambao haukuanzia barabarani. Hivyo, tuna mengi tunayofanana.
Jiji la Parii usipime! Siyo kama hii mikweche ya majiji uchafu mtupu. Barabara zake ni mikeka mitupu. Hakuna misongamano wala vurugu kama Uswazi. Kwa nilivyopenda jiji hili la Paris kuna siku nitahamia kule baada ya kugundua kuwa sina jinsi ya kubadili mikangafu yetu ya miji. Nadhani ningekuwa mkulu ningefunga mtu aitwaye meya. Ila kwa vile wote wana uvivu wa kufikiri nani amfunge nani? Heri kuwafunga wanaodai gesi ibaki umachingani.Ili sisi tule nini na tupate ten percent wapi? Senzi kabisa!
Huwa nashanga watu wanaopenda kulalamika kuwa deni la kaya ya kijiwe linatuna ila uchao. Yaani kuongezeka kwa tutrioni kumi na ushei watu wanapiga kelele utadhani jambo la ajabu. Hivi kazi ya ukuu ni nini kama siyo kutumia kama huha akili nzuri? Nani kawaambia kuwa mali ya umma inauma? Kwanini lisitune iwapo matumizi na matanuzi ndiyo fasheni kwetu sisi wenye maulaji? Hivi mnadhani kwenda nje namna hii tunatumia mawe? Tunatumia pesa yenu jamani na mlitupa ulaji ili tule migongoni mwenu. Ila nawashauri msikonde kwani mwaka 2015 sitagombea ukuu wa kijiwe wala kaya. Hivyo, nakula vya mwisho mwisho kwa usongo wa hali ya juu nikijua kuwa ulaji ukishanitoka maulaji kama haya nitayasikia kama siyo kuyasoma magazetini.
Lo! K umbe niko kwa Mfugambwa siyo Pariii! Kumbe naota! Ukisoma stori hii usiipe uzito maana ni ndoto! Acha niamke!
Chanzo: Tanzania Daima Januari 23, 2013.

No comments: